Mossad: Operesheni za mafanikio na zilizoshindwa za shirika la kijasusi la Israel

Chanzo cha picha, EPA, Getty, Maxar, BBC
- Author, BBC News Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Wakati Israel iliposhambulia vituo vya nyuklia vya Iran, kambi za kijeshi na makazi ya watu binafsi, hasa magharibi mwa nchi hiyo na karibu na mji mkuu Tehran- mwezi Juni mashambulizi hayo yakitokea angani, iilishukiwa kuwa shirika la ujasusi la Israel, Mossad, pia lilihusika katika kuwatafuta walengwa na kutelekeza operesheni kutoka ardhini.
Mawakala wa Mossad wanaaminika kutumia ndege zisizo na rubani zilizoingizwa Iran kinyemela kulenga mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran, na Iran ilikiri kwamba inashuku kuwa maafisa wa ujasusi wa Israel wameingia Iran.
Idadi kubwa ya wakuu wa jeshi na wanasayansi wa nyuklia walilengwa tangu mashambulio ya Israel kuanza tarehe 13 Juni.
Hizi ni baadhi ya operesheni za mafanikio za Mossad:

Chanzo cha picha, Anadolu via Getty
Kiongozi wa kisiasa wa Hamas, Ismail Haniyeh aliuawa kwenye nyumba ya wageni jijini Tehran tarehe 31 Julai 2024. Miezi kadhaa baadaye waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz alikiri kuwa Israel ndiyo iliyohusika na mauaji hayo.
Khalil al-Hayya, afisa wa ngazi ya juu wa Hamas, aliuambia waandishi wa habari kwamba kombora lilimpiga Haniyeh "moja kwa moja,'' akinukuu mashahidi waliokuwa pamoja naye.
Lakini ripoti ya gazeti la New York Times, ambayo inawanukuu maafisa saba, ilisema Haniyeh aliuawa kwa bomu ambalo liliwekwa miezi miwili kabla katika jengo hilo.
BBC haiwezi kuthibitisha lolote kati ya madai haya.
Haniyeh ni mmoja wa viongozi wengi wa Hamas waliouawa na Israel tangu mashambulizi ya kundi hilo kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, akiwemo kiongozi wa Hamas huko Gaza, Yahya Sinwar, kaka yake Mohammed, mkuu wa tawi la kijeshi la Hamas, Mohammed Deif, na makamu wake, Marwan Issa.
Vifaa vya Hezbollah

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tarehe 17 Septemba 2024, maelfu ya vifaa vya mawasiliano vililipuka kwa wakati mmoja kote Lebanoni, haswa katika maeneo yenye uwepo mkubwa wa wanachama wa Hezbollah. Milipuko hiyo ilijeruhi na kuua na kuzusha hofu.
Siku iliyofuata, redio za mawasilianoi zililipuka kwa njia hiyo hiyo, na kuua na kujeruhi mamia zaidi.
Wakati wa shambulio hilo, Israel na Hezbollah walikuwa wakirushiana makombora tangu Hezbollah ilipofyatua makombora kwenda Israel siku moja baada ya shambulio la Oktoba 7 la Hamas.
Miezi miwili baadaye, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikiri kuwa Israel ilihusika.
Katika mahojiano na CBS, maajenti wawili wa zamani walifichua kuwa Mossad ilificha vilipuzi ndani ya betri zinazotumia vifaa hivyo vya mawasiliano.
Hezbollah walinunua bila kujua vifaa hivyo zaidi ya 16,000 kutoka kampuni feki miaka 10 iliyopita, na baadaye walinunua vifaa vingine 5,000, CBS iliripoti.
Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu Volker Turk alitaja shambulio hilo kuwa uhalifu wa kivita.
Kuuawa Mohsen Fakhrizadeh

Chanzo cha picha, EPA
Novemba 2020, msafara uliombeba Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi mashuhuri wa nyuklia wa Iran, ulishambuliwa katika mji wa Absard, mashariki mwa mji mkuu, Tehran.
Fakhrizadeh aliuawa kwa kutumia bunduki iliyofyatuliwa kwa rimoti.
"Kutekeleza mauaji kwa njia kama hiyo dhidi ya mtu anayetembea bila ya raia yeyote kujeruhiwa kunahitaji akili," aliandika Jiyar Gol wa BBC Persian wakati huo.
Aprili 2018, Netanyahu alionyesha nyaraka kadhaa zinazodaiwa kuwa zinahusiana na mpango wa nyuklia wa Iran, ambazo alisema ziliibiwa miezi kadhaa hapo awali na Mossad katika operesheni kwenye kituo kilicho umbali wa kilomita 30 tu kutoka Tehran (hili lilithibitishwa baadaye na Rais wa Irani Hassan Rouhani).
Waziri mkuu wa Israel alimtaja Mohsen Fakhrizadeh katika kile alichosema ni mpango wa silaha za nyuklia ambao haujatangazwa.
"Dk Mohsen Fakhrizadeh ... kumbuka jina hilo," alisisitiza.
Hapo awali Iran iliishutumu Israel kwa kuwaua wanasayansi wengine wanne wa nyuklia wa Iran kati ya 2010 na 2012.
Kuuawawa Mahmoud al-Mabhouh

Chanzo cha picha, Getty Images
2010, Mahmoud al-Mabhouh, kiongozi wa kijeshi wa Hamas, aliuawa katika hoteli ya Dubai.
Mwanzo ilionekana kama kifo cha kawaida, lakini polisi wa Dubai hatimaye waliweza kuitambua timu ya mauaji baada ya kuchunguza picha za CCTV.
Polisi baadaye walifichua kwamba al-Mabhouh aliuawa kwa shoti ya umeme na kisha kunyongwa.
Ilishukiwa kuwa operesheni hiyo ilipangwa na Mossad, na ilizua hasira ya kidiplomasia kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wanadiplomasia wa Israel, hata hivyo, walidai hakuna ushahidi unaohusisha Mossad na shambulio hilo.
Maujai ya Yahya Ayyash

Chanzo cha picha, EPA
1996, Yahya Ayyash, mtengenezaji mkuu wa mabomu wa Hamas, aliuawa kwa simu ya mkononi ya Motorola Alpha iliyojazwa gramu 50 za vilipuzi.
Ayyash, kiongozi mashuhuri katika tawi la kijeshi la Hamas, alisifika kwa utaalamu wake wa kutengeneza mabomu na kupanga mashambulizi tata dhidi ya Israel.
Mwishoni mwa 2019, Israeli iliondoa udhibiti wa baadhi ya taarifa juu ya mauaji hayo, na Channel 13 TV ya Israeli ilipeperusha rekodi ya mazungumzo ya simu ya mwisho ya Ayyash na baba yake.
Operesheni Brothers

Chanzo cha picha, Raffi Berg
Mapema miaka ya 1980, Mossad - kwa maagizo ya Waziri Mkuu Menachem Begin - waliwasafirisha zaidi ya Wayahudi 7,000 wa Ethiopia hadi Israeli kupitia Sudan, kwa kutumia kituo bandia cha kupiga mbizi.
Sudan ilikuwa nchi, kwa hivyo Mossad walifanya kazi kwa siri, timu ya mawakala wa Mossad ilianzisha kituo cha mapumziko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu upande wa Sudan.
Mchana, walijifanya kuwa wafanyakazi wa hoteli na usiku waliwasafirisha Wayahudi, ambao walisafiri kisiri kutoka nchi jirani ya Ethiopia, kwa ndege na bahari.
Operesheni hiyo ilifanyika kwa miaka mitano, na ilipogunduliwa, maajenti wa Mossad walikuwa tayari wameshaondoka.
Mauaji ya Munich

Chanzo cha picha, Getty Images
1972, kikundi cha wanamgambo wa Palestina, Black September kiliwaua washiriki wawili wa timu ya Olimpiki ya Israel kwenye Michezo ya Olimpiki ya Munich na kuwakamata wengine tisa.
Wanariadha hao waliuawa baadaye katika jaribio la kuwaokoa lililofeli la polisi wa Ujerumani Magharibi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka iliyofuata, Mossad iliwalenga wale wanaoshukiwa kuhusika na shambulio hilo, akiwemo Mahmoud Hamshari.
Aliuawa na kilipuzi kilichotegwa kwenye simu katika nyumba yake mjini Paris.
Hamshari alipoteza mguu katika mlipuko huo na hatimaye kufariki dunia kutokana na majeraha yake.
Operesheni Entebbe

Chanzo cha picha, Getty Images
Operesheni ya Entebbe nchini Uganda 1976 inachukuliwa kuwa moja ya misheni ya kijeshi yenye mafanikio zaidi ya Israeli.
Mossad ilitoa taarifa za kijasusi, huku jeshi la Israel likifanya operesheni hiyo.
Wanachama wawili wa chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine na washirika wawili wa Ujerumani waliteka nyara ndege iliyokuwa inakwenda Paris na kuipelekeza Uganda. Waliwashika mateka abiria na wafanyakazi katika uwanja wa ndege wa Entebbe.
Makomando wa Israel walivamia uwanja wa ndege na kuwaokoa mateka 100 waliosalia wa Israel na Wayahudi.
Mateka watatu, watekaji nyara, wanajeshi kadhaa wa Uganda, na komando mkuu Yonatan Netanyahu (kaka ya Waziri Mkuu wa sasa wa Israel, Benjamin Netanyahu) waliuawa katika operesheni hiyo.
Afisa wa Nazi

Chanzo cha picha, Getty Images
Tukio la kutekwa nyara kwa afisa wa Nazi, Adolf Eichmann kutoka Argentina mwaka 1960 ni mojawapo ya mafanikio ya kijasusi ya Mossad.
Eichmann alihusika katika mauaji ya Holocaust, ambapo Wayahudi milioni sita waliuawa na Ujerumani ya Nazi katika Vita vya Pili vya Dunia.
Baada ya kukwepa kukamatwa kwa kuhama kati ya nchi kadhaa, hatimaye Eichmann aliishi Argentina.
Kundi la maajenti 14 wa Mossad walimfuatilia, wakamteka nyara, na kumpeleka Israel, ambako alishitakiwa na hatimaye kuuawa.
Licha ya oeresheni za Mossad kupangwa vyema, lakini si kila operesheni imefanikiwa.
Shambulio la Oktoba 7, 2023

Chanzo cha picha, AFP
Shambulio lililoanzishwa na Hamas kwenye miji ya Israel karibu na mpaka wa Gaza tarehe 7 Oktoba 2023 liliishangaza nchi hiyo.
Kushindwa kwa Mossad kutabiri shambulio hilo kunachukuliwa kuwa kushindwa kukubwa.
Shambulio la Oktoba 7 lilisababisha mauaji ya watu wapatao 1,200, wengi wao wakiwa raia. Wengine 251 walichukuliwa Gaza kama mateka.
Katika kukabiliana na shambulio la Hamas, Israel ilianzisha vita kwenye Ukanda wa Gaza, hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya 55,000, wengi wao wakiwa ni raia, kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas.
Vita vya Yom Kippur

Chanzo cha picha, Getty Images
Karibu miaka 50 iliyopita. Tarehe 6 Oktoba 1973, Misri na Syria zilianzisha mashambulizi ya kushtukiza kwa Israeli ili kurejesha Peninsula ya Sinai na Milima ya Golan.
Wakati wa shambulio la Yom Kippur, siku takatifu zaidi katika kalenda ya Kiyahudi. Majeshi ya Misri yalivuka Mfereji wa Suez, na kupata hasara ndogo tu, huku majeshi ya Syria yakishambulia maeneo ya Israel na kupenya hadi kwenye milima ya Golan.
Umoja wa Kisovieti ulitoa vifaa kwa Syria na Misri, na Marekani ilitoa msaada wa dharura kwa Israel.
Israel iliweza kuviondoa vikosi hivyo na vita viliisha tarehe 25 Oktoba - siku nne baada ya azimio la Umoja wa Mataifa la kutaka mapigano yasitishwe.
Mahmoud al-Zahar

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2003, Israel ilifanya shambulizi la anga lililolenga nyumba ya kiongozi wa Hamas Mahmoud al-Zahar katika mji wa Gaza.
Ingawa al-Zahar alinusurika katika shambulio hilo, lilisababisha kifo cha mkewe na mwanawe, Khaled, pamoja na wengine kadhaa.
Shambulio hilo la bomu liliharibu kabisa makazi yake.
Khaled Meshaal

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika operesheni iliyosababisha mzozo mkubwa wa kidiplomasia, Israel ilijaribu kumpa sumu Khaled Meshaal, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas, huko Jordan mwaka 1997.
Misheni hiyo ilishindwa pale maajenti wa Israel walipokamatwa, na kuilazimisha Israel kutoa dawa ya kuokoa maisha ya Meshaali.
Mkuu wa wakati huo wa Mossad, Danny Yatom, aliruka kwa ndege hadi Jordan kumtibu Meshaal.
Tukio hilo lilivuruga kwa kiasi kikubwa uhusiano kati ya Israel na Jordan.
Lavon Affair

Chanzo cha picha, Getty Images
1954, Misri ilitibua operesheni ya kijasusi ya Israel iliyojulikana kama Operesheni Susannah.
Mpango huo ulikuwa wa kutega mabomu katika vituo vya Marekani na Uingereza nchini Misri kuishinikiza Uingereza kubakisha vikosi vyao vilivyowekwa kwenye Mfereji wa Suez.
Tukio hilo lilijulikana kwa jina la Lavon Affair, lililopewa jina la Waziri wa Ulinzi wa Israel wakati huo, Pinhas Lavon.
Inaaminika kuwa alihusika katika upangaji wa operesheni hiyo.











