Mossad: Mbinu,mikakati na kuwatumia wanawake katika shirika la ujasusi la Israel walipa ufanisi katika operesheni zake

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Je ni vipi taifa la Israel linavyomudu kusalia salama na kujilinda dhidi vitisho kutoka kwa nchi mbali mbali zinazopakana nayo?
Ni kweli kwamba shirika la ujasusi la Mossad linatumia mbinu zisizo za kawaida kuwaangamiza maadui wa Israel?
Kwanini kuna idadi kubwa ya wanawake wanaolifanyia kazi shirika la Mossad?
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo watu wengi huuliza lakini hawapati majibu .
Hata hivyo tathmini ya karibu kuhusu vitendo na matamshi ya waliowahi kulifanyia kazi shirika hilo itakupa taswira ya jinsi Mossad inavyofanya kazi .
Kwanza Mossad inatumia maajenti wa kipekee na waliopewa mafunzo kuweza kutimiza malengo yake katika operesheni zake kote duniani .Hizi hapa baadhi ya sababu zinazoifanya Mossad kuwa shirika la kipekee la ujasusi kwa Israel
Wanawake wana uwezo wa kipekee
Mnamo mwaka wa 2017 shirika la Mossad lilitoa tangazo kuwatafuta maajenti wa kike .
Tayari shirika hilo lina asilimia 40 ya wanawake wanaolifanyia kazi huku asilimia 24 wakishikilia nafasi za juu za uongozi ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinaeleza .
Wanawake wamesifiwa kama maajenti bora wa siri na mkuu wa zamani wa Mossad.

Tamir Pardo alisema mnamo 2012 kwamba maajenti wa kike "wana faida tofauti katika vita vya siri kwa sababu ya uwezo wao wa kufanya kazi nyingi" na "wanaficha tabia yao ili kufikia malengo," kulingana na The Jerusalem Post.
"Kinyume na maoni potofu, unaona kuwa uwezo wa wanawake ni bora kuliko wanaume kwa kuelewa eneo, hali za kusoma, ufahamu wa mazingira. Wakati unapopata walio bora , ni wazuri sana," mkuu wa shirika hilo wakati huo alisema.
Wakati wa tangazo hilo miaka mitatu iliyopita Tovuti ya Mossad iliwaambia wanaotaka kujiunga na shirika hilo kwamba "Sio kile ulichokifanya bali ni kuhusu ni wewe ni nani."
Mossad ilianzishwa lini?
- Kikosi cha kimataifa cha huduma ya ujasusi cha Israeli kilianzishwa mnamo 1949
- Ni moja wapo ya huduma za ujasusi za siri zinazoogopwa sana na za visa vingi ulimwenguni. Maafisa wake wote wamepongezwa kwa operesheni za kipekee na hata wanatuhumiwa kwa mauaji ya kinyama
- Kwanza ilithibitisha azma yake ya kufikia ulimwengu kwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita wa Nazi Adolf Eichmann mnamo 1960 huko Argentina
Iran yalalama
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iwapo kuna nchi ambayo inailaumu Mossad kwa kila mkosi unaoikumba ,basi Iran ni ya kwanza katika orodha hiyo . Imeilaumu Mossad kwa kuhusika na mauaji ya wanasayansi wake wanaoendesha mpango wake wa kuwa na silaha ya nyuklia .
Mnamo Januari 10 mwaka wa 2011 Iran ilitangaza kwamba imewakamata raia wake 10 kwa mauaji ya Profesa Massoud Ali Mohammadi.
Wizara ya Ujasusi ya Iran ilisema kuwa washukiwa 10 walifanya kazi kwa ushirikiano na Mossad.
Vituo vya runinga vya serikali vya Iran vilitangaza madai ya kukiri kwa mmoja wa wanaume waliokamatwa, aliyeitwa Majid Jamali Fashi.
Ajenti anayeshukiwa alionyeshwa akiongea kwenye chumba chenye kilichokuwa na giza.
Bwana Jamali Fashi alielezea kuwa, karibu miaka mitatu iliyopita, alitakiwa kwenda katika Ubalozi Mdogo wa Israeli huko Istanbul.
Sababu ya ziara hiyo haijulikani. Lakini alifanya hivyo, na akasema kwamba alihojiwa na maajenti wa Israeli.
"Waliuliza maelezo yote ya maisha yangu haswa. Na pia, walinipa hakikisho ili nishirikiane nao kwenye mipango yao na wakaniuliza nikusanye habari kutoka ndani ya Iran."
Huo tu ni mfano mmoja wa jinsi Mossad ilivyofaulu kuwafanya raia wengi wa Iran kuwa maajenti wake na kuanza kukusanya habari za kijasusi kwa niaba ya Israel .
Baada ya mafunzo ya miezi kadhaa, waliokuwa wakizugumza naye walimwambia kwamba alikuwa na kazi ya kufanya na kumuambia kwamba alifaa kumlenga - Massoud Ali Mohammadi, profesa katika Idara ya Fizikia katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Alielezea kwamba walitaka yeye atege bomu la pikipiki nje ya nyumba ya profesa huyo,na hivyo ndivyo alivyouawa mwanasayansi huyo wa Iran .

Chanzo cha picha, AFP
Tangia tukio hilo kumekuwa na visa vingi vya Wanasayansi wa Iran kuuawa katika hali za kutatanisha na kila mara Iran imekuwa ikiilaumu Israel kwa kuhusika na mauaji yao.
Jambo jingine ambalo limefanikisha ufanisi wa shirika la Mossad ni jinsi taifa la Israel linavyotetewa na Marekani .
Serikali ya Israel inafahamu jinsi inavyolindwa na Marekani kidiplomasia na hivyo basi imejipatia ukakamvu wa kuweza kufanya lolote bila kuogopa athari za kuidhuru.
Panapotokea lalama za nchi nyingine kuhusu operesheni za Mossad ama madai ya mauaji ,vikwazo vya kimataifa au hata kutoka kwa umoja wa Mataifa haviwezi kuelekezewa Israel kwasababu ya Marekani kuingilia kati na kuipa kinga .
Pia haisaidii kwamba Iran ambayo ina uhasama na Marekani imekuwa ikiilenga Israel kupitia makundi ya wapiganaji kama vile Hamas na Hezbollah .
Hilo linaifanya Marekani kuiona Israel na shirika lake la Mossad kuonekana kama chaguo bora la kutumiwa kukabiliana na vitisho vinavyotolewa na Iran kwa maslahi ya Marekani na nchi nyingine za magharibi.















