Maelezo ya video, Mambo matano makuu yanayotawala uchaguzi mkuu wa kenya mwaka huuMaelezo kuhusu taarifa
Author, Calvin Muga
Nafasi, Mchambuzi
Kenya inaelekea uchaguzi mkuu tarehe 9 Agosti mwaka huu na masuala makubwa katika uchaguzi huu ni ukosefu wa ajira,umaskini ,gharama ya juu ya maisha,ufisadi,ukosefu wa usalama na afya .
Lakini shina kubwa linalounganisha masuala yote haya yote ni uchumi .
Licha ya serikali kutoa takwimu zinazoonyesha kwamba hali ya uchumi nchini imeboreka ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka ya nyuma ,manufaa haya ama Ushahidi wa hilo haupo katika Maisha ya kila siku ya raia wengi wa kawaida .
Janga la Corona lilivuruga sekta nyingi za kichumi mojawapo ikiwa utalii hatua iliyosababisha wengi kupoteza ajira .
Pindi hali ilipoanza kuboreka na baadhi ya sekta kuanza kujikwamua ,vita vikazuka Ukraine na kusababisha hali iliyokuwa mbaya kuzorota na kuwa ngumu zaidi baada ya bei ya mafuta,gesi na vyakula kupanda .
Uchaguzi wa Kenya utafanyika chini ya mazingira hayo magumu kiuchumi na ndio mwanzo wa tathmini hii kuhusu mambo yanayotawala ndimi za wengi kuhusu uchaguzi wa Kenya mwaka huu .
Chanzo cha picha, AFP
Uchumi
Uchumi wa Kenya umeathirika sana kwa sababu ya mfumuko wa bei ya bidhaa . Hali ilizidishwa kuwa mbaya zaidi na janga la Covid-19 ambalo nusura lisitishe kila shughuli ya kuleta pato.
Wakati wa muhula wa kwanza wa Rais mstaafu Mwai Kibaki, uchumi ulikua kwa 7%, hili hata hivyo lilishuka kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 na 2008 pamoja na mfumuko wa bei, ufisadi na Covid-19 ambayo ilifanya hali kuwa mbaya zaidi na kushuka hadi 1% mnamo 2020.
Wagombeaji wawili wakuu wa kiti cha urais Raila Odinga na William Ruto wakiwa katika kampeni zao wameendelea kueleza Wakenya wanachonuia kufanya ili kujenga uchumi ambao umeathiriwa na mambo yaliyotajwa hapo juu.
Ruto ameelezea nia yake ya kuuboresha uchumi kutumia mfumo anaotumia katika kampeni wa 'Bottom up' -unaolenga kuwahamasiaha wafanyibiashara wadogo wadogo na ili wajiboreshe kuanzia chini na kuchangia muimariko utakaopanda hadi juu .
Inasuburiwa kwa hamu na wengi kufahamu kwa kina jinsi wagombeaji hao wanavyolenga kuboresha uchumi kwa namna itakayowafaa pia raia wa kawaida.
Ufisadi
Kulingana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Kenya hupoteza wastani wa Kshs 608 bilioni kila mwaka kutokana na ufisadi ambao unamaanisha 7.8% ya jumla ya bajeti.
Ili Kenya kutimiza ajenda yake ya maendeleo na kufikia Pato la Taifa (GDP) inayotarajiwa ya 5% kama inavyokisiwa na Fitch Solutions, viongozi wetu wanapaswa kuwa nia halisi ya kupambana na ufisadi.
Mmoja wa wagombea urais Raila Odinga kwa nyakati tofauti ameangazia jinsi anavyonuia kukabiliana na ufisadi ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya ufisadi na kuwachukulia hatua wanaohusika na ufisadi akiangalia kiwango kinachopotea kila mwaka.
Haya ni mazungumzo makubwa zaidi katika uchaguzi wa 2022 nchini Kenya.
Naibu wa rais William Ruto kwa upande wake amesema njia inayotegemeka ya kukabiliana na tatizo hilo ni kuboresha mifumo ya haki na mahakama ili pasiwe na muingilio wa kisiasa anaosema mara nyingi hulemaza viuta dhidi ya rushwa .
Nani yuko kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Kenya ?
Fahamu zaidi kuwahusu wagombea urais wa Kenya
Chagua mgombea ili kutazama wasifu wake
Raila Amollo Odinga
Muungano wa Azimio la Umoja
Mgombea huyo mwenye umri wa miaka 77 ni mhandisi aliyesomea Chuo Kikuu cha Ufundi cha Magdeburg (sasa kinajulikana kama Chuo Kikuu cha Otto-von-Guericke Magdeburg) nchini Ujerumani.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja One Kenya Coalition Party.
Hili litakuwa jaribio lake la tano baada ya kugombea katika: 1997, 2007, 2013 na 2017.
Bw Odinga alikuwa mmoja wa wapiganiaji wa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Alikamatwa, akafungwa na wakati fulani akaenda uhamishoni kwa sababu ya kupigania haki hiyo
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu, kuanzia 2008-2013.
Odinga alihusika kufanikisha miradi mikubwa iliyotekelezwa na serikali ya Kibaki, kama vile miradi ya umeme vijijini na barabara.
Kuafikia ukuaji wa uchumi wa tarakimu mbili kupitia uwekezaji katika biashara ndogo ndogo na sekta ya viwanda.
Utoaji wa huduma bora za afya kwa wote.
Utoaji wa vifaa vya michezo na burudani kwa ukuaji wa kimwili, kiakili, kijamii, kimaadili na maendeleo ya watu.
Kufuatia jaribio la mapinduzi ya Agosti 1, 1982, Raila Odinga alikamatwa na kukabiliwa na mashtaka kadhaa, yakiwemo ya uhaini ambayo alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka. Tume ya Ukweli ya Haki na Maridhiano iliambiwa mwaka 2011 kwamba Odinga alikuwa na mawasiliano na mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo. Odinga amekana kuhusika kila mara. - Makavazi ya Kitaifa ya Kenya.
William Samoei Ruto
Muungano wa Kenya Kwanza
Mgombea huyu mwenye umri wa miaka 55 ana Shahada ya Uzamifu/PhD katika Ikolojia ya Mimea na BSc katika Botany na Zoology kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Anawania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance ( chenye mafungamano na Kenya Kwanza).
Aliongoza Vuguvugu la vijana la Youth for Kanu '92 (YK'(92).
Wizara yake iliorodheshwa kama inayofanya bora zaidi serikalini alipokuwa Waziri wa Kilimo.
Alihudumu kama Naibu Rais wa kwanza wa Kenya chini ya katiba mpya ya 2010.
Alihudumu kama mbunge wa eneo bunge la Eldoret Kaskazini kuanzia 1997-2007.
Kutenga $424 milioni kila mwaka kwa biashara ndogo ndogo za kati.
Kuanzisha mfuko wa elimu wa kitaifa ili kukidhi gharama zisizo za masomo.
Tekeleza kikamilifu sheria ya usawa wa kijinsia ya thuluthi mbili katika uteuzi wa kisiasa na kutenga nusu ya baraza lake la mawaziri kwa wanawake.
Mnamo 2008, Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru Naibu Rais William Ruto kusalimisha shamba la ekari 100 na kulipa $ 62,500 kwa Adrian Muteshi, mkulima ambaye alimshtaki kwa kuchukua mali hiyo baada ya uchaguzi wa 2007. - Kenya Law
Mnamo 2011, Bw Ruto alikabiliwa na kesi kwa makosa matatu dhidi ya binadamu: Mauaji, uhamisho wa watu kwa lazima na mateso ya watu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu. Miaka mitano baadaye mahakama ilisitisha kesi hiyo kwa msingi kwamba - ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu. -ICC
George Wajackoyah
Chama cha Roots
Profesa huyo mwenye umri wa miaka 61 ana shahada ya uzamili katika sheria kuhusu maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Warwick na shahada ya uzamili , sheria (sheria za Marekani kutoka Chuo Kikuu cha Baltimore.
Bw Wajackoyah anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Roots Party.
Alihudumu kama Inspekta katika idara ya usalama ya Special branch wakati wa utawala wa marehemu Rais Daniel Moi kabla ya kulazimika kutorokea ng'ambo ili kuepuka kufunguliwa mashtaka na mamlaka.
Yeye ni mshirika katika kampuni ya mawakili aliyoianzisha mwaka wa 2018.
Alifunnza somo la sheria na uchumi katika vyuo vikuu vya Marekani, Uingereza na Kenya.
Kuhalalisha matumizi ya kiviwanda ya bangi
Badilisha siku za kazi hadi Jumatatu hadi Alhamisi.
Huduma ya afya ya bure na msaada kwa wazee, walio hatarini na wajawazito
David Mwaure Waihiga
Chama cha Agano
David Mwaure anawania kiti cha urais kwa tiketi ya Chama cha Agano.
Ni kiongozi wa Chama cha Agano.
Alihitimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na ana Shahada ya Uzamili katika masomo ya uongozi.
Yeye ni wakili mkuu na amehudumu kama mwanasheria kwa zaidi ya miongo mitatu.
Ana kampuni ya uwakili na amewania viti mbalimbali vya kisiasa.
Ilianzishwa chama cha Agano mwaka 2006.
Kupambana na ufisadi uliokithiri.
kuunda nafasi za ajira.
Kurejesha mali ya Kenya iliyofichwa nje ya nchi.
Pata maelezo zaidi kuhusu sera za wagombea urais hapa
Katika hotuba yake moja akiwa London,Ruto aliahidi kuhakikisha kwamba idara ya mahakama na asasi nyingine husika zinapata uhuru wa kweli na hata wa kifedha ili kuweza kutekeleza shughuli zao bila muingilio wa serikali.
Gharama ya Juu ya Maisha
Leo hii asilimia 16 ya wakazi wa Kenya wanaishi chini ya dola 1.9 kwa siku, kwa hivyo hii ina maana kwamba wengi hawawezi kupata mambo ya kimsingi kumudu maisha yao.
Gharama ya bidhaa imepanda sana kwa takriban mara dufu , kwa mfano, mwaka wa 2010 pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi ilikuwa ikiuzwa kati ya Kshs 60 hadi Kshs 70, leo inauzwa inauzwa kati ya Kshs 120 hadi Kshs 140, na ongezeko hilo bado linaendelea kupanda .Hali ni vivyo hivyo kwa msururu wa bidhaa nyingi za matumizi ya kila siku .
Wagombea wawili wakuu wa urais Raila Odinga na William Ruto wameendelea kuwafafanulia Wakenya wakati wa kampeni zao kuhusu jinsi wanavyonuia kushughulikia suala hili wakibainisha kuwa linagusa sehemu kubwa ya wakazi.
Ushuru wa Juu
Kenya ni mojawapo ya nchi zinazotoza ushuru wa juu kwa raia wake katika ukanda wa Afrika.
Ushuru huu hutoka kutoka kwa Pay As You Earn,(kwa walio katika ajira rasmi) hadi VAT(unaotozwa bidhaa), ushuru wa simu, ushuru wa biashara na hili limesababishwa na ongezeko kiwango cha kikomo cha bajeti ambacho kimeendelea kukua kila mwaka.
Katika mwaka wa kifedha wa 2021-2022, hazina ya kitaifa iliwasilisha bajeti ya Kshs 3.66 trilioni ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita 2012-2013 ambapo bajeti ilikuwa Kshs 1.45 trilioni.
Hii inamaanisha kuwa kadri bajeti inavyoongezeka ndivyo wigo wa ushuru unavyoongezeka.
Hili limeathiri Wakenya pakubwa. Utozaji ushuru huu unaolalamikiwa kuwa wa juu haujaepuka fikra za wagombeaji wawili wakuu wa urais huku Raila Odinga akieleza jinsi katika serikali yake vijana watapata afueni kwa msamaha wa kulipa ushuru kwa miaka 7. Hili ni suala zito la kampeni katika uchaguzi huu wa 2022.
Ukosefu wa ajira kwa vijana
Kulingana na sensa ya 2019, vijana walio chini ya umri wa miaka 35 wanasheheni 75% ya jumla ya watu Milioni 47.6. Vyuo Vikuu na na vingine vya mafunzo huwa na wanafunzi kati ya 15,000 hadi 30,000 kila mwaka kulingana na data ya 2019 ya Wizara ya Elimu.
Hali hii imefanywa kuwa mbaya zaidi na Covid-19 ambayo imeacha watu kadhaa bila ajira katika uchumi ambao haujaendelea sana kiviwanda.
Hili limewaacha zaidi idadi kubwa ya vijana wasio na ajira wakipigania fursa ndogo zilizopo jambo ambalo limewafanya kuwa hatarini zaidi kwa ghilba za kisiasa kama vile vurugu za uchaguzi.
Katika duru mbili za uandikishaji wapiga kura tuliona wagombeaji wawili wakuu wa urais Raila Odinga na William Ruto wakiwaasa vijana ili wajiandikishe kuwa wapiga kura na kushiriki uchaguzi mkuu ujao tarehe 9 Agosti 2022 huku kila mgombea akiahidi kushughulikia masuala yanayowahusu .
Odinga amahidi msamaha wa ushuru wa miaka 7 kwa vijana iwapo atachaguliwa kuwa rais huku William Ruto akiahidi kuwainua vijana kupitia usaidizi wa kifedha na uhamasisho wa kujitegemea kupitia mikopo kwa biashara zao .
Wawili hao pia wamefanya mikutano mingi inayolenga vijana ili kuwashawishi waapigie kura mwaka huu .