Bei za vyakula Kenya: Kwa nini zimepanda sana?

th

Chanzo cha picha, AFP

Wakenya wenye hasira wamekuwa wakijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kulalamikia gharama ya juu ya maisha nchini inayochochewa na ongezeko la gharama ya bidhaa za kimsingi zikiwemo chakula, umeme na mafuta.

Wakitumia alama ya reli #lowerfoodprices, Wakenya wameikosoa serikali kwa kukosa kuzuia kupanda kwa bei ya bidhaa za kila siku jambo ambalo wanasema limefanya maisha kuwa magumu.

Mnamo Januari mfumuko wa bei nchini ulipungua kidogo kwa mwezi wa pili mfululizo - hadi 5% - lakini bei za bidhaa za msingi za chakula kama unga wa mahindi na unga wa ngano, viazi, mboga na matunda ziliendelea kupanda - ambayo inaweza kuathiri vibaya watu wa kipato cha chini na kati .

Mfumuko wa bei ya vyakula kwa mwezi wa Januari ulifikia 9%, kumaanisha Wakenya wengi walitatizika kuweka chakula mezani.

Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya (KNBS) inasema familia maskini, ambapo chakula kinachukua takriban 36% ya jumla ya matumizi, mzigo ni mkubwa zaidi.

Watu wengi walishiriki orodha zao za ununuzi, wakieleza kwa kina jinsi bei za bidhaa za msingi za vyakula kama maziwa, mkate, sukari na unga wa mahindi zilivyopanda kwa kasi katika miezi ya hivi karibuni, na kufanya iwe vigumu kwao kumudu milo mitatu kwa siku.

Lakini wakati mafadahaiko kwenye mitandao ya kijamii yalikuwa ya pamoja, kubanwa na uhaba wa fedha ni jambo la kibinafsi zaidi .

Benandine Munira, mfanyabiashara katika soko la wazi la Toi la Nairobi, anasema anatatizika kuweka chakula mezani kwani bajeti yake ya kila mwezi haiwezi kununua bidhaa kama ilivyokuwa miezi michache iliyopita.

"Bei za bidhaa kwa kweli zimepanda. Hatuwezi kuvumilia zaidi. Miezi michache iliyopita kujaza tena silinda ya gesi ya kupikia yenye uzito wa kilo 6 ilikuwa kati ya $5 [£3.50] hadi $6. Leo hii ni takriban $13," asema.

"Hapo zamani, ukiwa na bajeti ya ununuzi ya $26 ungeondoka na sanduku lililojaa bidhaa. Leo kiasi hicho hicho kinakupa vitu vichache tu."

TH

Kwa nini bei zimekuwa zikipanda?

Kuongezeka kwa gharama ya maisha kunaweza kuhusishwa na mchanganyiko wa mambo ya nje na ya ndani.

Chini ya shinikizo kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuongeza mapato zaidi, serikali imeongeza ushuru kwa bidhaa za kila siku za nyumbani kama vile gesi ya kupikia, mafuta na chakula.

Kwa mfano, kodi ya ongezeko la thamani (VAT) haikutumika kwa gesi ya kupikia kwa miaka mingi lakini ushuru wa 16% ulitozwa Julai 2021.

Kwa kiasi fulani kwa sababu ya athari za Covid-19, ambayo iliathiri utalii na mauzo ya nje, shilingi ya Kenya imekuwa ikipoteza thamani - kwa takriban 6% tangu Mei 2021 - ikipandisha bei ya bidhaa zote zinazoagizwa kutoka nje.

Janga hilo pia limetatiza misururu ya usambazaji wa kimataifa, na kuifanya kuwa ghali zaidi na ngumu kupata na kuhamisha bidhaa na huduma kuvuka mipaka.

Nikhil Hira, mtaalam wa ushuru katika kampuni yenye makao yake makuu Nairobi ya Kody Africa LLP, anasema: "Hakuna shaka kwamba leo gharama ya maisha imepanda kupita udhibiti.

"Na ni ngumu haswa kwa wale ambao wanaishi kwa ujira wa kila siku, na bila ujira huo wa kila siku hawawezi kula usiku."

Nje ya jiji, hali ni mbaya zaidi. Ukame wa muda mrefu kaskazini mwa nchi hiyo umewaacha takriban watu milioni 2.8 wakikabiliwa na njaa kali.

Je, serikali inaweza kufanya lolote?

Kwa muda mfupi, serikali inaweza kuleta ahueni kwa kupunguza VAT kwa bidhaa za kawaida za nyumbani kama vile gesi ya kupikia, mafuta ya kupikia na chakula. Lakini lazima itengeneze sera mpya ya ushuru ambayo inaendana na mabadiliko ya mahitaji.

Wizara ya petroli tayari inafanya mpango wa ruzuku kuruhusu serikali kuwafidia wafanyabiashara wa mafuta kwa kupanda kwa bei ya petroli, ili kuwakinga watumiaji.

TH

Chanzo cha picha, AFP

Wizara ya Nishati pia imekuwa ikitekeleza punguzo la asilimia 30 la gharama za umeme tangu Desemba mwaka 2021 ili kuwapunguzia gharama watumiaji.

Suala la kupanda kwa bei ni lazima lichukue nafasi kubwa katika uchaguzi mkuu wa Agosti.

Mmoja wa wanaopendekezwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, Naibu William Ruto, anaahidi taifa lenye usalama wa chakula.

Akiwa kwenye kampeni mwezi Desemba, alisema: "Tutaweka fedha za kutosha katika kilimo, tutazalisha chakula cha kutosha, tutapunguza gharama za mbegu na gharama ya mbolea, tutapunguza gharama za chakula ili tuweze kushusha gharama za maisha nchini Kenya, ili tuhakikishe kila Mkenya anaweza kulisha familia yake."

Huku mpinzani wake mkuu, Raila Odinga, akiahidi mpango wa ulinzi wa kijamii unaolenga takriban Wakenya milioni mbili wasio na ajira na walio katika mazingira magumu, ambao watapokea takriban dola 55 kwa mwezi.

Lakini Wakenya wanapaswa kukumbuka kuwa Bw Kenyatta mwenyewe alitoa ahadi sawia mwaka wa 2013, alipozindua kampeni yake ya urais: "Janga la umaskini na ukosefu wa ajira bado linakumba taifa letu, na kupora matumaini ya mamilioni ya watu. Asilimia 70 ya vijana wetu nchini Kenya hawana kazi. Tunahitaji kutengeneza ajira kwa vijana wetu itakuwa kipaumbele changu."

Benki ya Dunia inakadiria kwamba uchumi wa nchi utakua kwa asilimia 5 mwaka wa 2022, lakini zaidi ya takwimu hizi za vyombo vya habari, wakenya wanataka kuhisi ukuaji huo wao binafsi.