Uchaguzi Kenya 2022:Maeneo muhimu yatakayoamua mshindi wa uchaguzi wa urais Kenya

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, BBC Swahili
Huku ikisalia chini ya miezi sita kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 nchini Kenya , ramani ya uchaguzi nchini humo inazidi kuwa wazi huku baadhi ya maeneo yakijitokeza kama maeneo muhimu ambayo huenda yataamua ni nani atakayechaguliwa kuwa rais wa taifa hilo kumrithi rais Uhuru Kenyatta muhula wake utakapotamatika .
Miungano inayoendelea kuundwa kati ya wanasiasa mbali mbali na vyama vyao hadi sasa imezaa taswira ya miungano ambayo huenda ikapambana uchaguzini .
Hadi sasa kuna Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu wa rais William Ruto ambaye alipigwa jeki na kuwasili upande wake kwa Musalia Mudavadi wa ANC na Moses Wetangula wa Ford Kenya , Muungano wa Azimio la Umoja unaoungwa mkono na rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga na One Kenya Alliance unaoongozwa na Kalonzo Musyoka paoja na vinara wa vyama mbali mbali
.Hata hivyo muungano wa OKA unaripotiwa kuwa katika mazungumzo ya kujiunga na Azimio la Umoja ingawaje mazungumzo hayo yamepunguzwa kasi baada ya Kalonzo kudai kwamba kuna mkataba aliosaini na kinara wa ODM kwamba angemuunga mkono katika uchaguzi wa mwaka huu .
Maeneo yatakayokuwa na 'usemi' mkubwa uchaguzini
Kaunti za Magharibi, Kati mwa Kenya, Kaskazini Mashariki, Ukambani, Maa, Turkana, Meru, Nairobi na Pwani zinaibuka kuwa viwanja kuu vya makabiliano ya kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Raila, kulingana na kura za maoni za hivi punde.
Timu za Ruto na Raila zimekuwa zikifanya safari za mara kwa mara katika maeneo hayo muhimu kwa kura za urais kwenye misheni za kusaka kura huku Rais akisemekana kupanga mashambulizi makali katika eneo la Mlima Kenya ambalo limekuwa likimegemea upande wa Ruto, katika juhudi za kumgeuzia makali naibu wake.
Seneta wa Murang'a, Irung'u Kang'ata, ambaye ni mshirika wa Ruto, anasema mkakati wao ni kuepuka makabiliano dhidi Rais, badala yake wakichagua kuwafikia na kuzungumza moja kwa moja na wapiga kura.
Uchaguzi Kenya 2022:Unaweza pia kusoma
UNAYOFAA KUJUA:Uchaguzi Kenya 2022: Je Naibu wa rais wa Kenya William Ruto anakabiliwa na changamoto gani katika kumteua naibu wake wa rais?
Ruto alitanguliwa kusonga karibu na wapiga kura wa Mlima Kenya wakati wa kampeni zake kwa Uhuru kabla ya mzozo kuibuka kati yao na amekuwa akifanya safari nyingi katika eneo hilo ambapo anaendelea kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge.
Kaunti tano za eneo la Kati za Nyandarua, Nyeri, Kiambu, Murang'a na Kirinyaga zinakisiwa kuwa na jumla ya kura milioni 3.1.
Iwapo rais atafaulu kukitia makali chama chake cha Jubilee ili kumsakia Odinga kura katika eneo hilo huenda likawa muhimu sana katika mapambano ya kuamua rais ajaye wa Kenya .
Sintofahamu ya kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuhusu iwapo atajiunga na Azimio au kuzindua kampeni yake ya urais chini ya Muungano wa One Kenya Alliance imezifanya kaunti za Ukambani za katika eneo la Mashariki za Machakos, Makueni na Kitui kuwa katika hali ya kutojua zitaegemea wapi wakati wa kura
Kalonzo azifanya kaunti za Ukambani kubeba kura 'muhimu'
Utulivu haupo katika eneo la Ukambani na wengi watangoja ishara kutoka kwa Kalonzo ingawa magavana wa kaunti hizo wameafikiana kuunga mkono Azimio .
Jukumu la Kalonzo katika kutoa mwelekeo wa jamii litakuwa na mabadiliko fulani katika kipute cha urais . Inaonekana ana nia ya kumsukuma Raila ukutani ili kuweza kutia kibindoni donge zito kabla ya kukubali kuwa upande wake .
Ikiwa atajiunga na Azimio kinyang'anyiro hicho huenda kikapungua uzito kumpa afueni kiongozi wa ODM kwani atakuwa na hakikisho la kujizolea kura nyingi kutoka kaunti za Ukambani dhidi ya Ruto .

Chanzo cha picha, KALONZO MUSYOKA/FACEBOOK
Hata hivyo endapo ataamua kuendelea na kampeni zake kuwania kiti cha urais huenda mambo yakawa mazito na wadadisi wanasema hilo ni mojawapo ya chaguo lake iwapo hatojiunga na mojawapo ya miungano miwili mikubwa katika uchaguzi wa mwaka huu .
Magavana Charity Ngilu (Kitui), Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni)wanauunga mkono Azimio na wamemtaka Kalonzo kuungana nao.
Ruto anaungwa mkono na wengi katika maeneo ya Meru, Tharaka Nithi na Embu kwa mujibu wa kura za hivi maajuzi za maoni lakini uamuzi wa Waziri wa Kilimo Peter Munya wa kutogombea dhidi ya Gavana wa Meru Kiraitu Murungi unaweza kubadilisha hali hiyo kwa Azimio.
Marsabit na Isiolo pia zipo kwenye darubini na huenda zikawa muhimu sana katika kuamua mshindi wa uchaguzi wa urais .
Rais Uhuru amekuwa akikutana na viongozi kutoka kaunti kadhaa za Kaskazini Mashariki na amekuwa akiwarai viongozi wa kaunti hizo kujiunga na Azimio .
Ingawaje kaunti za Kakamega na Vihiga magharibi mwa Kenya zilikuwa katika kapu la Raila katika uchaguzi uliopita, kujiunga kwa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang'ula na upande wa Ruto katika Kenya Kwanza kunaweza kufanya kaunti hizo mbili kuwa uwanja mkubwa wa makabiliano ya kura huku Bungoma ikielekea Kenya Kwanza.
Kando na Wetang'ula ambaye ni Seneta wa Bungoma, wabunge Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Mwambu Mabonga (Bumula), John Waluke (Sirisia), Didmus Barasa (Kimilili) na Majimbo Kalasinga (Kabuchai) wanaunga mkono Kenya Kwanza.
Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ameahidi kuhakikisha kwamba eneo la Magharibi linaweka kura zake katika kapu la Raila licha ya ushirikiano wa Musalia-Wetang'ula.
Mudavadi anayetoka Vihiga huenda akahama na idadi ya wapiga kura kwenye muungano wake mpya na Ruto, Kakamega na Busia zinaonekana kuegemea upande wa Azimio.
Baadhi ya watu wa jamii ya Luyhia imeshawishiwa vikali kuwa inaweza kutwaa kiti hicho baada ya urais wa Raila.
"Elijah Masinde, nabii wetu, aliwahi kutabiri kwamba siku moja uongozi wa Kenya utakuja Mulembe lakini utapitia Ziwa Victoria.
Siku hiyo inakaribia. Raila atatukabidhi uongozi 2027," Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa amenukulia akisema mwezi Februari .
Huko Nyanza, Kisumu, Migori, Homa Bay na Siaya zinachukuliwa kuwa zimetwaliwa na Raila, huku Kisii na Nyamira zikiegemea sana upande wa kiongozi huyo wa Azimio.

Chanzo cha picha, MUSALIA/FACEBOOK
Ruto amefanya ziara nyingi katika eneo hilo katika muda wa miaka mitatu iliyopita akiwa na matumaini ya kushinda wafuasi.
Huko Pwani, Raila amekuwa akifurahia kuungwa mkono na wakaazi wengi na eneo hilo linatarajiwa kumpendelea.
Lakini Ruto anategema kwamba safari zake nyingi katika eneo hilo litampa kura. Hili tayari limeshazaa matunda baada ya mgombea wake kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa Msambweni mwezi Desemba 2020.
Gavana wa Kwale Salim Mvurya tayari ametangaza kuunga mkono Ruto na hivi majuzi alipandishwa cheo na kuwa mojawapo ya viongozi wakuu wa Muungano wa Kenya Kwanza.
Kaunti zingine za Kilifi, Mombasa, Tana River na Taita Taveta bado zinachukuliwa kuwa na wafuasi wengi wa Raila.
Lamu inabaki kuwa katika mizani na uwezekano wa kwenda popote.
Huku Gavana wa Lamu Fahim Twaha akiunga mkono Azimio, Seneta Anwar Oloitiptip anamuunga mkono Ruto.
Katika Bonde la Ufa, Ruto anatarajiwa kupata asilimia kubwa ya kura katika kaunti za Bomet, Kericho, Baringo, Uasin Gishu, Nandi, Pokot Magharibi, Samburu na Elgeyo-Marakwet.
Hata hivyo, atalazimika kujitahidi sana katika kaunti za Nakuru na Laikipia ili kukabiliana na changamoto kutoka kwa magavana wa maeneo hayo Lee Kinyanjui na Ndiritu Muriithi ambao ni vigogo katika vuguvugu la Raila.
Huko Narok na Kajiado, wachanganuzi wanasema picha hiyo imefifia kwa sasa, wakiongeza kuwa bado ni jambo la kusubiri japo walibaini kuwa Narok ilikuwa akihama polepole kumuunga mkono Raila licha ya Jubilee kuvuna pakubwa katika uchaguzi uliopita.
Ruto amekuwa akitumia mbinu ya kuwaunganisha wagombeaji wa viti mbali mbali waafikiane kupitia demokrasia ya majadiliano ili kuzuia kugawanyika kwa kura za wafuasi katika mrengo wake .
Kaunti ya Turkana, inasalia kuwa mtihani kwa mirengo yote kwani wagombeaji wakuu kutoka eneo hilo wako kwenye kambi zinazoshindana.
Gavana anayeondoka wa Turkana Josphat Nanok anaongoza kampeni za Ruto kitaifa huku mpinzani wake, aliyekuwa Waziri wa Mafuta John Munyes, akitwikwa jukumu la kuleta kura za eneo hilo kwa kapu la Raila.
Huko Trans Nzoia, kuundwa kwa chama cha Democratic Action Party kinachoongozwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa bado kunaweza kutatiza mambo kwa Ruto.
Eneo la Kaskazini Mashariki linajivunia kura 600,000 na litakuwa na umuhimu mkubwa katika uchaguzi wa mwezi Agosti. Wanasiasa kadhaa kutoka eneo hilo walihamia Azimio na kuacha kambi ya Ruto katika eneo hilo kubwa.
Jijini Nairobi, kura za maoni za hivi punde zinampa Raila uongozi muhimu. Ushawishi wa Uhuru kwa wakaazi wa jiji, haswa athari za Mamlaka Jiji la Nairobi, unaweza kuwa muhimu katika kuamua wakaazi watampa nani kura zao .














