Miss Rwanda 2022: Jinsi Jeanette Uwimana alivyopata ujasiri wa kuingia katika mashindano ya Malkia wa urembo

Chanzo cha picha, Miss Rwanda
"Ni kama nilizaliwa na ulemavu wa kutosikia. Mama yangu anakumbuka kuwili. Nilipelekwa katika hospitali mbalimbali baadaye wakabaini kuwa sisikii " anasema Uwimana Jeannette
Akiwa na umri wa miaka 26, Bi Jeanette ndiye msichana wa kwanza mwenye ulemavu wa kutosikia na kuzungumza aliyepiga hatua katika mashindano ya ulimbwende nchini Rwanda maarufu kama Miss Rwanda, na sasa a niwe mukobwa napambana na wasichana wengine 70 wanaowania taji hilo.
Alisoma elimu ya msingi na sekondari katika shule ya walemavu HVP-Gatagara na anatarajia kuendelea na masomo katika chuo kikuu. Hata hivyo ameiambia BBC kuwa changamoto kuu ya wenye ulemavu kama wake ni kuwasiliana na wenzake kwasababu lugha yao ni ya ishara ambayo wengi hawaielewi.
Akiwa msichana pekee katika familia ya watoto saba Uwimana ambaye anatoka katika mkoa wa Kusini mwa Rwanda, aliiambia BBC kuwa "nimekuwa na lengo la kufanya kazi kwa bidiii ili baadaye niwe mwanamke anayejiweza, bila kujali ulemavu wangu."
Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali linapopigania haki za watu wenye ulemavu Rangira Aimé Frederic, anasema kuwa ingawa mwaja jana sheria ilitangazwa inayozitaka taasisi zinazotoa huduma kusaidia katika mawasiliano ya watu wanapotumia lugha ya ishara, bado njia ni ndefu kwani bado hilo halijatekelezwa katika maeneo mengi.

"Kupitia katika Miss Rwanda, nataka kupigania haki sawa kwa wote na kuwaendeleza vijana wenye ulemavu'', anasema Bi Jeannete Uwimana. Zaidi ya hayo, vigezo vinavyopambaniwa, urembo, akili na utamaduni, ninaweza kukwambia kuwa vyote ninavyo ."
Changamoto anazotaka kuzishinda na kuzimaliza.
Alivyojitokea kuwakilisha mkoa wake wa Kusini alikuwa ndiye wa kwanza kugombea taji la Miss Rwanda mwenye ulemavu lilikuwa ni jambo jipya. Baada ya kujitokeza walemavu wengine wasiosikia na kuzungumza wawili kutoka maeneo mengine ya Rwanda.
Majaji sasa wanatakiwa kutumia wakalimani wao wanapowauliza maswali ili nao wawajibu.
Sio mara ya kwanza kwa Bi Jeanette kuwa na utashi wa kushiriki shindano hili. Anasema: "wakati wote nimekuwa nikitamani kushiriki lakini watu wengi, wakiwemo marafiki zangu wa karibu, wamekuwa wakinikatisha tamaa wakisema sina vigezo vinavyotakikana.
"Lakini mwaka huu nimeamua kwamba sasa ni lazima nigombee taji hili kama wengine wote."

Chanzo cha picha, Miss Rwanda
Wanaoshindania taji hilo kwa ujumla ni wasichana 70, baadaye watachujwa na kubakia wasichana 20 watakaopata mafunzo kwenye kambi na tarehe 18 Machi atatangazwa mshindi wa Miss Rwanda 2022.
Kufikia sasa Jeannette anasema kuwa hajapata tatizo alilolipata kwasababu ya lugha yake ya ishara, lakini katika maisha yake ya kawaida anasema wenye ulemavu kama wake kwa ujumla hukabiliwa na matatizo mengi.
"Utamaduni wa kututenga unatufanya tukabiliwe na umasikini, jambo jingine ni kwamba jamii inaona kuwa vijana walemavu hawahusiki na suala la ngono na hivyo kutunyima fursa ya kushiriki katika mazungumzo ya afya ya uzazi, jambo linalowafanya wasichana wengi wenye ulemavu kupata mimba za mapema."
Ameongeza kuwa wenye ulemavu sawa na wake wanapaswa kuwa na haki ya kupewa huduma kwa uhuru kama watu wengine.
Sheria mpya, njia ndefu
Sensa ya jumla iliyofanywa mwaka 2012 ilionyesha kuwa kuna jumla ya walemavu 33,000 wasiosikia na kuongea nchini Rwanda.
Baada ya juhudi za wanaharakati wanaopigania haki za walemavu wasiosikia na wasiozungumza, mwaka jana sheria mpya ilitangazwa kuhusu haki ya kutolewa kwa huduma ya lugha ya ishara kwa ajili ya walemavu hao, iliyoagiza huduma ya mawasiliano hayo itolewe katika ofisi zinazotoa huduma zote za umma nchini.

Chanzo cha picha, Miss Rwanda
Hatahivyo njia bado ni ndefu, kulingana na mkuu wa shirika la haki za walemavu nchini Rwanda - Rwanda Media for Deaf Rwanda -Rangira Aimé Frederic , ambaye anasema maeneo mengi ya huduma za umma bado hayaweza kutoa huduma ya mawasiliano ya ishara kwa walemavu.
Rangira anasema: "Inaonekana kuwa serikali ina utashi wa kuchukua hatua juu ya suala hilo, lakini tatizo tulilo nalo ni kwamba lugha ya ishara ni lugha ambayo haijakubaliwa rasmi, ndio maana tunajitahidi kuieneza."

Chanzo cha picha, Miss Rwanda
Mashindano ya Mlimbwende wa Rwanda- Miss Rwanda yameendelea kupanuka na kufungua milango kwa watu wengi wenye ulemavu sawa na alionao Bi Jeannette Uwimana, kama anavyosema Msemaji wa mashindano hao Meghan Nimwiza .
Nimwiza - ambaye pia alikuwa Mlimbwende wa Rwanda 2019 - anasema: "Wenye ulemavu wanaoshiriki shindano hili, hawamo kwasababu wana ulemavu au wamehurumiwa, wamo katika shindano hili kwasababu wanaweza ."
Meghan Nimwiza anasema aliyekuwa Miss Rwanda 2021 yalishirikiana na shule ya watoto walemavu ya HVP-Gatagara na hilo "liliongeza imani kwa wengi" wanaosoma katika shule hiyo.
'Tangu zamani alitamani kuwa Miss Rwanda' - Mama yake
Baada ya kupiga hatua ya kwanza na kuingia katika shindano hili, Jeannette Uwimana anasema kwamba kwa sasa watu wengi wanamuunga mkono, wakiwemo watu wa familia yake, marafiki zake, na watu wa Eneo anakozaliwa.

Mama yake Jeannete, Colette Mukabutera anasema kuwa tangu Jeannette alipokuwa mtoto mdogo alikuwa ni mchangamfu na alikuwa mwenye upendo kwa watoto, hasa wenye ulemavu.
"Alipokuwa akienda shule, alikuwa akiwanyanyua na kuwapakata na hata kuwaogesha watoto walemavu wasio na miguu. "Alikuwa pia mchangamfu sana, hata kama hakuweza kuzungumza, mahali alipo huwezi kuwa na upweke … na tangu zamani akiwa mtoto mdogo alipenda sana mambo ya fasheni na kuwa Miss." Alisema mama Mukabutera.
Licha ya kuwa Faïna Kabayiza, ni mkalimani wa Bi jeanette katika mashindano haya, ni rafiki yake wam uda mrefu tangu walipokutana kwa mara ya kwanza walipokuwa katika shule ya sekondari mwaka 2016.
Bi Kabayiza aliiambia BBC kuwa : "Jeannette ni msichana wa kipekee, anayechangamana na watu wengine kwa urahisi wakiwemo wenye ulemavu sawa na wake, si muoga na ni mcheshi.
Ni mtu anayetia bidii kufikia ndoto zake na msichana jasiri wa hali ya juu, anayejiamini, asiyekata tamaa."

Chanzo cha picha, Miss Rwanda
Bw Rangira A. Frederic anasema ni''jambo linalotufurahisha''kuona kwamba katika shindano la Miss Rwanda kuna wanaotumia lugha ya ishara kuwasilian, ni mfano mzuri kwa watoto wenye ulemavu "kwamba ndoto zao hazipaswi kufunikwa kwasababu ya ulemavu walionao ."
"Wazazi wenye watoto wenye ulemavu ule na pia wameona kuwa mtoto wao akipata msaada anaohitaji-ambao ni lugha ya mawasiliano pekee, anaweza kufikia mengi'' "Hahitaji kuhurumiwa, anachohitaji ni access ya lugha ya ishara, akiwa nayo hatakuwa na tofauti na mimi, anaweza kushindana sawa na wengine, popote pale."
Jeannette Uwimana aliiambia BBC kuwa iwapo atakuwa Miss Rwanda, atapigania kuomba sheria inayowatetea walemavu itekelezwe, ili wenyie ulemavu kama alionao waweze kuwa huru kupata huduma za umma, mashuleni, kwenye benki, hospitali na maeneo mengine ya umma…. "Nitaendelea kutoa uelewa kuhusu matatizo magumu ambayo yanawakabili watu wenye ulemavu kila siku ."













