Virusi vya corona: Simulizi ya mlimbwende wa zamani wa Rwanda aliyepona virusi

Chanzo cha picha, VIVINE UWIZEYE/FACEBOOK
- Author, Dinah Gahamanyi
- Nafasi, BBC News Swahili
Mlimbwende maarufu nchini Rwanda Vivine Uwizeye, wiki hii ametangaza kuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kuugua na kupona ugonjwa wa Covid-19.
Bi Uwizeye al maarufu Miss Vivy alikua mlimbwende kitengo cha wanawake na wasichana wanene mwaka 2011.
'' Ilibidi nipimwe mara nne katika kipindi cha wiki mbili ili kubaini kuwa kweli nimepona virusi vya corona'', aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Yeye ndiye mtu maarufu zaidi nchini Rwanda aliyefahamika kuwa miongoni mwa watu wengine waliopata maambukizi ya virusi vya corona na taarifa ya ugonjwa wake imeenea na kuibua gumzo katika mitandao ya kijamii.
Katika mahojiano na BBC, Bi Uwizeye alisema binafsi ndiye aliyewaita maafisa wa afya baada ya kubaini kuwa alikua na dalili za ugonjwa wa Covid-19 ikiwa ni pamoja na kikohozi pamoja na maumivu ya kichwa, ambapo alitaka apimwe .
Anasema wahudumu wa afya walimkuta nyumbani kwake tarehe 16/04/2020 wakachukua vipimo, akaambiwa kuwa majibu atayapata kati ya saa 24 na 48; "Walipotoka nyumbani jioni hiyo niliugua sana nikaanza kushindwa kupumua, ndipo nilipowapigia simu kuwafahamisha, wakaja wakanipeleka hospitali ya rufaa ya CHUK nikaongezewa hewa ya kupumua, walinipima kubaini ikiwa nina magonjwa mengine, lakini hawakuyapata ". anasema Bi Vivine.
Anasema siku iliyofuata akiwa hospitalini ndipo alipofahamishwa kuwa alibainika kuwa na virusi vya corona. ''Ilikua ni taarifa iliyonitisha sana, niliogopa mno ''
Alitangazwa kuwa mgonjwa mahututi pekee
Tarehe 18/04/2020 Bi Uwizeye, ambaye ni mama wa watoto wawili, anasema alipelekwa katika hospitali ya Kanyinya iliyopo nje kidogo ya jiji la ambako wagonjwa wa virusi vya Corona wamekua wakihudumiwa.
Wakati huo wizara ya Afya ya Rwanda ilitangaza kuwa ndiye mgonjwa pekee aliye mahututi, jambo ambalo binafsi amekiri katika mazungumzo na BBC.
"Nilifuatiliwa sana kimatibabu, walitumia juhudi zote walizoweza za matibabu, wakanipa dawa zinazotakiwa zote, kundi la madaktari walikua wanakuja kwa pamoja kuangalia ni nini cha kufanya kunisaidia. Ni mimi pekee niliyekua mgonjwa mahututi wa virusi vya corona".

Chanzo cha picha, Vivine Uwizeye
'Sijawa na matatizo ya kiafya licha ya unene'
Licha ya kwamba mimi ni mnene sikupatikana na magonjwa yanayowapata watu wanene …hospitalini hawakunipata na ugonjwa mwingine wowote, na hii ni moja ya sababu mwili wangu uliweza kupona virusi'', anasema Mlimbende Vivine.
Madaktari hutijbu dalili za ugonjwa huu, halafu mwili unasaidia kupigana na virusi hivi, halafu kulingana na uwezo wa kinga yako ya mwili unaweza kupona, alielezea
Kulingana na maelezo ya mlimbwende Uwizeye katika kituo cha wagonjwa wa virusi vya corona cha Kanyinya, wagonjwa hupatwa na matatizo ya kisaikolojia kutokana na hofu ugonjwa huu, hupatiwa usaidizi ili kuwaepusha kupata magonjwa ambayo yanaweza kusababishwa na taarifa za kutisha juu ya ugonjwa wa corona.
''Huduma zote zinazojtolewa katika kituo kile, mgonjwa hawezi kulipia garama zake, kusema ukweli ninaona serikali ilikua imejiandaa vema kukabiliana na virusi vya corina'', anasema.
Wiki mbili baada ya kupona
Mwanzoni mwa mwezi huu ndipo matokeo ya vipimo vya kwanza yalipotolewa na kuonyesha kuwa amepona ugonjwa wa corona : "Wakati huo unakua umeingia katika awamu nyingine ya kupimwa vizuri zaidi ili kuangaliwa kama kweli umepona'', anasema.
Bibi Uwizeye anasema kuwa tangu wakati huo hadi aliporuhusiwa kwenda nyumbani kutoka hospitalini tarehe 13/05/2020 amepimwa mara nne ili kubaini kuwa kweli amepona virusi vya corona.
Uwizeye anasema Covid-19: ''Usipotibiwa mapema unaweza kufa, lakini kulingana na nilivyokua mahututi ninasisitiza kuwa mtu akiweza kufika hospitalini mapema naweza kupona ".

Chanzo cha picha, Vivine Uwizeye
Uwizeye anasema ugonjwa huu ni mgumu sana kujua jinsi unavyoenezwa: '' Kusema ukweli sijui nilivyoambukizwa virusi vya corona…ninachojhisi ni kwamba huenda niligusa mahali ambapo kulikua na virusi na kupata maambukizi '', anakumbuka.
Anasema, ''ingawa nimeweza kupona Covid-19, madaktari walinionya kuwa ninapaswa kuendelea kujikinga ili nisipate maambukizi ya virusi.
Bi Uwizeye alivalishwa taji la mlimbwende wa Rwanda baada ya kushinda mashindano ya Mlimbwende - kitengo cha wasichana na wanawake wanene mwaka 2011.
Tangu wakati huo mashindano ya aina hiyo hayajawahi kufanyika tena nchini Rwanda, kwa hiyo yeye bado ndiye mlimbwende wa kitengo hicho cha wanawake, Bi Vivine aliiambia BBC.













