Mgogoro wa Ukraine: Macron anasema makubaliano ya kuepusha vita yanaweza kuafikiwa

TH

Chanzo cha picha, EPA

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema anadhani makubaliano ya kuepusha vita nchini Ukraine yanawezekana na kwamba ni halali kwa Urusi kuibua wasiwasi wake wa kiusalama.

Kabla ya mazungumzo mjini Moscow na Rais wa Urusi Vladimir Putin siku ya Jumatatu, Macron alitoa wito wa kuwepo kwa hatua za kulinda mataifa ya Ulaya na kuifurahisha Urusi.

Urusi imepeleka wanajeshi wengi kwenye mpaka wa Ukraine lakini inakanusha kuwa ina mpango wa kuvamia.

Moscow imetoa matakwa kadhaa, ikiwa ni pamoja na kwamba muungano wa kujihami wa Nato uondoe uwezekano wa Ukraine kuwa mwanachama, na kwamba ipunguze uwepo wake wa kijeshi mashariki mwa Ulaya.

Nchi za Magharibi zimekataa hili, badala yake zimependekeza maeneo mengine ya mazungumzo, kwa mfano mazungumzo ya kupunguza silaha za nyuklia.

Bw Macron aliliambia gazeti la Journal du Dimanche kwamba lengo la Urusi si Ukraine, lakini ufafanuzi wa sheria na Nato na pia Muungano wa Ulaya.

Alisema anatumai mazungumzo yake na rais wa Urusi yatatosha kuzuia mzozo wa kijeshi, na kwamba anaamini Bw Putin atakuwa tayari kujadili masuala mapana zaidi.

Bw Macron, ambaye pia alizungumza na Rais wa Marekani Joe Biden siku ya Jumapili, alionya dhidi ya kutarajia Urusi kuchukua hatua za kupunguza hali hiyo na kusema Urusi ina haki ya kueleza wasiwasi wake yenyewe.

Lakini alisema kuanzisha mazungumzo na Urusi hakuwezi " kutegemea kudhoofika kwa taifa lolote la Ulaya".

"Hii lazima ifanyike wakati wa kuiheshimu Urusi na kuelewa kiwewe cha watu hawa wakuu na taifa hili kubwa."

Safari ya kuelekea Moscow na kisha mji mkuu wa Ukraine Kyiv siku itakayofuata inaratibiwa na washirika wa Ujerumani na Marekani.

Kuonekana kwa Bw Macron katika masuala ya kimataifa pia kunakuja kabla ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa mwezi Aprili.

Rais wa Ufaransa ametoa wito wa kuanzishwa upya uhusiano na Urusi hapo awali, na mwezi Januari alisema Muungano wa Ulaya unapaswa kuanzisha mazungumzo yake na Urusi, badala ya kuitegemea Marekani.

TH

Chanzo cha picha, TASS/GETTY IMAGES

Wakati huo huo, serikali ya Marekani imeonya tena kwamba Urusi inaweza kuivamia Ukraine wakati wowote.

Siku yoyote sasa, Urusi inaweza kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Ukraine, au inaweza kuwa wiki kadhaa kutoka sasa," mshauri wa usalama wa kitaifa wa White House Jake Sullivan aliambia Fox News siku ya Jumapili.

Maafisa wawili wa Marekani hapo awali waliliambia shirika la habari la Reuters kwamba Urusi imekusanya takriban asilimia 70 ya uwezo wa kijeshi unaohitajika kwa ajili ya uvamizi kamili wa Ukraine.

TH

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alionekana kupunguza tishio la uvamizi, akiandika kwenye twittter siku ya Jumapili: "Msiamini utabiri kwa sababu miji mikuu tofauti ina matukio tofauti, lakini Ukraine iko tayari kwa hatua zozote."

Mvutano kati ya Urusi, Ukraine na nchi za Magharibi unakuja karibu miaka minane baada ya Urusi kuiteka rasi ya Crimea kusini mwa Ukraine na kuunga mkono uasi wenye umwagaji damu katika eneo la mashariki la Donbas.

Moscow inaishutumu serikali ya Ukraine kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya Minsk ambayo ni makubaliano ya kimataifa ya kurejesha amani mashariki mwa nchi, ambapo waasi wanaoungwa mkono na Urusi wanadhibiti maeneo mengi na takriban watu 14,000 wameuawa tangu 2014.