Mzozo wa Ukraine: Marekani yashutumu Urusi kwa kupanga visingizio bandia vya uvamizi

Chanzo cha picha, Reuters
Urusi inapanga kubuni kisingizio cha uvamizi wa Ukraine, kwa kutumia uwongo kuwalaumu wanajeshi wa Ukraine kwa kuwashambulia watu wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi au Urusi yenyewe, maafisa wa Marekani walisema.
Chaguo moja ambalo Urusi inasemekana kuzingatia ni kuigiza na kurekodi shambulio la uwongo, na picha za mlipuko zikionyesha watu wengi waliouawa.
Ikijibu madai hayo, Urusi ilisema haina mpango wa oparesheni bandia.
Marekani na Nato wana wasiwasi kufuatia hatua ya vikosi vya Urusi kujikusanya karibu na Ukraine.
Urusi inakanusha kuwa inapanga kuvamia UKraine, ikisema kuwa wanajeshi wapo kwa ajili ya mazoezi. Kwa sasa wanafikia takriban 100,000.
Mvutano huo unakuja miaka minane baada ya Urusi kuiteka rasi ya Crimea kusini mwa Ukraine na kuunga mkono uasi wa umwagaji damu katika eneo la mashariki la Donbas.
Maafisa wakuu wa utawala wa Marekani walisema operesheni inayodaiwa, kupangwa na idara za usalama za Urusi, itaonyesha picha za majeruhi wa raia huko Donbas, mashariki mwa Ukraine, ili kuzua hasira dhidi ya mamlaka ya Ukraine.
Hatua ambayo inaweza kutumika kuhalalisha shambulio dhidi ya Ukraine, maafisa walisema.
Mpango huo unaweza kuhusisha kuigiza na kurekodi shambulio la uwongo, walisema.
Ingeonyesha maiti na maeneo yaliyoharibiwa, vifaa bandia vya kijeshi vya Ukraine, ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa Uturuki na waombolezaji wanaoigiza kuzungumza Kirusi, walisema.
Lakini maafisa hao walisisitiza kuwa hilo ni chaguo mojawapo tu ambalo Urusi ilikuwa inazingatia, na kuongeza kuwa wanaiangazia katika juhudi za "kuizuia Urusi kufikia hatua iliyokusudiwa".
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Liz Truss alisema ujasusi wa Marekani "ni ushahidi wa wazi na wa kushtua wa uvamizi wa Urusi ambao haukuchochewa na shughuli ya chinichini ya kuiyumbisha Ukraine".
"Nia hii mbaya kuelekea nchi huru, ya kidemokrasia haikubaliki kabisa na tunalaani kwa nguvu zote. Uingereza na washirika wetu wataendelea kufichua hila na propaganda za Urusi na kuzikemea," alisema katika taarifa.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alijibu ripoti hizo.
"Hii si ahadi ya kwanza ya aina yake [kutoa maelezo kuhusu uchochezi wa Urusi]," alisema, akinukuliwa na shirika la habari la Tass. "Kitu kama hicho kilisemwa hapo awali, lakini hakuna kilichotokea."
Wakati huo huo, Balozi wa Urusi katika Muungano wa Ulaya EU, Vladimir Chizhov, aliiambia CNN kwamba Moscow haikupanga operesheni zozote za uwongo za kuivamia Ukraine.
Taarifa za madai ya njama hiyo zinajiri siku moja baada ya Marekani kusema kuwa inatuma wanajeshi zaidi kwa washirika wa Nato barani Ulaya.
Urusi ilisema hatua hiyo ni "ya uharibifu" na ilionyesha kuwa wasiwasi wake kuhusu upanuzi wa Nato Ulaya mashariki ulikuwa wa haki.
Uhasama kati ya Urusi na Marekani, ambayo bado inamiliki silaha kubwa zaidi za nyuklia duniani, ulianza Vita Baridi (1947-89). Wakati huo Ukraine ilikuwa sehemu muhimu ya Muungano wa Kikomunisti wa Kisovieti.
Diplomasia kali iliendelea siku ya Alhamisi kujaribu kuzuia kile ambacho wataalamu kadhaa wa kijeshi wanahofia kuwa vita vikubwa barani Ulaya.
Wakati wa ziara yake katika mji mkuu wa Ukraine Kyiv, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alijitolea tena kuwa mpatanishi katika mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi.
"Uturuki iko tayari kutatua mgogoro," Bw Erdogan alisema. Uturuki ina uhusiano mzuri na Ukraine na Urusi.
Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alifanya mazungumzo ya simu na Rais wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky kujaribu kutuliza mvutano.



















