Israel yataka Uturuki kuwaachilia wanandoa wawili waliokamatwa kwa tuhuma za ujasusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Israel imetoa wito kwa Uturuki kuwaachilia wanandoa wa Israel walioshtakiwa na upepelezi kwa madai ya kupiga picha makaazi ya rais mjini Istanbul.
Natalie na Mordi Oknin, ambao ni madereva wa basi kutoka Modiin, walikamatwa wiki iliopita baada ya kuripotiwa na mfanyakazi mmoja wa mgahawa.
Jaji mmoja aliagiza kwamba waendelee kuzuiliwa huku wakisubiri kesi yao.
Wakili wao wa Israel alisema kwamba mashtaka hayo hayana msingi na Israel ikasisitiza kwamba hawakufanyia kazi kitengo chochote cha Israel.
''Hawa ni watu wawili wasio na hatia ambao wametuhumiwa kimakosa, alisema waziri mkuu wa taifa hilo Naftali Bennett siku ya Jumapili.
''Nilizungumza hapo jana na familia na tunafanya kila kitu kutatua tatizo hilo''.
Uhusiano kati ya Israel na Uturuki umezorota tangu shambulio baya la mwaka 2010 katika meli ya Uturuki iliokuwa ikijaribu kuondoa kizuizi cha kuingia Gaza.

Chanzo cha picha, ANADOLU AGENCY
Chombo cha habari cha Uturuki , Anadolu kiliripoti siku ya Ijumaa kwamba wanandoa wa Israel na raia wa Uturuki walikamatwa baada ya wafanyakazi katika mgahawa wa jumbea lenye urefu wa mita 369 la Camlica TV na Redio kuambia maafisa wa polisi kwamba wamekuwa wakipiga picha ya maakzi ya rais Recep Tayyip Erdogan.
Bwana na Bi Oknin walihojiwa na waendesha mashtaka kabla ya kupelekewa mahakamani , ambapo jaji mmoja aliwashtaki kwa upelelezi wa kisiasana na kijeshi na kuongezea kuzuiliwa kwao kwa takriban siku 20.
Wakili wa Israel aliyekuwa akiwasimamia wawili hao, Nir Yaslovitzh, alikataa madai hayo , na kuambia chombo cha habari cha Israel kwamba makosa yao ya pekee ni kupiga picha makazi ya rais Erdogan wakati walipokuwa wakisafiri kwa kutumia boti.
Alitambua jumba hilo kuwa lile la kasri la Waterfront Dolmabahce ambalo halijatumika kwa miongo kadhaa, licha ya kwamba upande mmoja wa jumba hilo unatumika kuwa afisi ya rais.

Chanzo cha picha, Facebook
Makaazi ya sasa ya rais katika jumba la the Huber Mansion,liko katika mji huo
Rais wa Israeli Isaac Herzog alisema kwamba ana uhakika kwamba wawili hao hawana hatia na kusisitiza kwamba hawajafanyia kazi kitengo chochote cha ujasusi cha Israel."
Siku ya Jumatatu, waziri wa masuala ya kigeni Yair Lapid alituma ujumbe wa twitter kwamba maafisa wa Israel walikuwa wakifanya kazi usiku kucha ili kuhakikisha wawili hao wanaachiliwa huru.
Wizara ya masuala ya kigeni pia ilitangaza kwamba mamlaka ya Uturuki ilikubali kuwaruhusu wanadiplomasia wa Israel ili kufanya ziara ya ubalozi wao nchini humo.
Mwezi uliopita, vyomba vya habari nchini Uturuki viliripoti kwamba watu 15 walikamatwa na mamlaka ya Uturuki kwa tuhuma za kulipelelezea shirika la Ujasusi la Mossad. Naibu mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo alikana kwamba walikuwa wapelelezi wa Israel.














