Wagner: Mwanawe Gaddafi akumbwa na tishio la kukamatwa kuhusu mamluki wa Urusi

hl

Chanzo cha picha, Getty Images

Waendesha mashtaka nchini Libya wametoa waranti ya kukamatwa kwa Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya marehemu Muammar Gaddafi, juu ya tuhuma za uhusiano na mamluki wa Urusi.

Uchunguzi wa BBC umebaini uhusiano kati ya shughuli za kikundi cha Wagner huko Libya na uhalifu wa kivita uliofanywa dhidi ya raia wa Libya.

Wapiganaji wa Urusi walionekana kwa mara ya kwanza nchini Libya mnamo 2019 walipojiunga na vikosi vya jenerali muasi, Khalifa Haftar, kushambulia serikali inayoungwa mkono na UN katika mji mkuu Tripoli. Mzozo huo ulimalizika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano mnamo Oktoba 2020.

Kikundi cha Wagner kiligunduliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2014 wakati kilikuwa kikiunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi katika mzozo mashariki mwa Ukraine. Tangu wakati huo, kundi hilo limehusika katika mizozo ya Syria, Msumbiji, Sudan, na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Amri ya kukamatwa kwa Saif al-Islam Gaddafi ilisambazwa ndani kwa vyombo vya usalama vya Libya na mwendesha mashtaka Mohammed Gharouda mnamo 5 Agosti, lakini ilitangazwa kwa umma tu baada ya uchunguzi wa BBC .

Saif al-Islam Gaddafi ni nani ?

Kwa muda mrefu Gaddafi alishukiwa kuwa na uhusiano na Urusi.

Kabla ya ghasia za 2011, aliaminiwa na wengine kuwakilisha matumaini ya mageuzi ya taratibu nchini Libya, ambayo ilitawaliwa na baba yake Muammar tangu 1969.

Mzungumzaji mzuri wa Kiingereza ambaye alisoma katika Shule ya kifahari ya London school of Economics , kwa muda mrefu alionekana kama mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa nchini, na mrithi wa baba yake.

sa

Chanzo cha picha, Reuters

Walakini, mara tu maandamano dhidi ya serikali yalipoanza Libya mwanzoni mwa mwaka wa 2011, Gaddafi alijiunga na msako dhidi ya waandamanaji waliopinga serikali ya babake

Baadhi ya wanafamilia yake mwishowe waliuawa au kukimbia nchi. Gaddafi, wakati huo huo, alikamatwa na waasi mwishoni mwa mwaka 2011 na kupelekwa katika mji wa Zintan, kusini magharibi mwa Tripoli. Aliachiliwa na wanamgambo waliomshikilia miaka sita baadaye.

Wakati akiwa kizuizini, alihukumiwa kifo akiwa hayupo na korti huko Tripoli juu ya mauaji ya waandamanaji mnamo 2011.

Anatafutwa pia na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa wakati wa ukandamizaji.

Ingawa hajaonekana hadharani kwa miaka, Gaddafi alitoa mahojiano na New York Times mnamo Julai, ambapo alizungumzia mipango yake ya kurudi kwenye siasa.

Kulingana na vyanzo vya habari huko Tripoli, kuna uwezekano bado anajificha huko Zintan.

Saif na Urusi

Wakati wa utengenezaji wa makala ya BBC juu ya shughuli za kikundi cha Wagner huko Libya, BBC ilikutana na maafisa wa ujasusi wa Libya ambao walizungumza juu ya uhusiano mkubwa wa Gaddafi na Moscow na kumuelezea kama "mgombea anayependelewa na Urusi kutawala Libya".

Maafisa wa ujasusi walikuwa wakimchunguza Maxim Shugaley, raia wa Urusi ambaye alikamatwa mjini Tripoli mnamo Mei 2019 kwa mashtaka ya ujasusi.

Maelezo ya video, Mamluki nchini Libya: 'Huu ni ufalme wa mlengaji shabaha wa Urursi'

Alishtumiwa kwa kumfanyia kazi Yevgeny Prigozhin, mfanyabiashara tajiri aliye na uhusiano wa karibu na Rais Vladimir Putin, kama sehemu ya kampeni ya kuingilia uchaguzi iliyoundwa kumweka Gaddafi kama mtawala wa Libya wakati wa mashambulizi ya Jenerali Haftar dhidi ya mji mkuu.

Bwana Shugaley, na mkalimani wake wa Kiarabu ambaye alikamatwa pamoja naye, waliachiliwa mwishoni mwa mwaka wa 2020.

Kulingana na ripoti, Bw Shugaley alikuwa amekutana na Gaddafi wakati alipokuwa Libya. Urusi hata imetoa filamu mbili juu ya kukamatwa kwa Bwana Shugaley, ambazo zimechapishwa kwenye YouTube na zinaonyesha Gaddafi kama "mwokozi wa Libya" na Bw Shugaley kama "shujaa wa Urusi".

Afisa mmoja wa ujasusi wa Libya aliambia BBC: "Ikiwa Urusi ingekuwa na uwezo , tungekuwa na Saif [al-Islam] Gaddafi akitoa hotuba yake ya ushindi katika Uwanja maarufu wa Mashahidi wa Tripoli.

Libya - Muongo wa machafuko

Kuanguka kwa utawala wa Gaddafi mnamo 2011: utawala Kanali Muammar Gaddafi wa zaidi ya miongo minne unaishia katika ghasia baada ya mapinduzi ya Kiarabu. Anajaribu kukimbia lakini anakamatwa na kuuawa

Mgawanyiko wa nchi: Baada ya 2014, vikundi vikubwa vyenye silaha vinaibuka mashariki na magharibi

Waaasi waelekea Tripoli mnamo Aprili 2019: Jenerali Haftar, kiongozi wa vikosi vya mashariki, aelekea kuuteka mji wa Tripoli na serikali inayoungwa mkono na UN huko. Pande zote mbili zinapata msaada wa kijeshi na kidiplomasia kutoka kwa mamlaka tofauti za kieneo, licha ya zuio la silaha la UN

Vita kusistishwa mnamo Oktoba 2020:Mwanzoni mwa 2021 serikali mpya ya umoja yachaguliwa na kuapishwa, kupeleka taifa kwenye uchaguzi mnamo Desemba. Wapiganaji wa kigeni na mamluki walipaswa kuondoka, lakini maelfu wanasalia nchini humo