Mwanawe Gaddafi atangaza nia ya kutaka kuongoza Libya

Chanzo cha picha, MAHMUD TURKIA/AFP VIA GETTY IMAGES
Miaka kumi tangu kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muamar Gaddafi ,mwanawe wa kiume Saif al-Islam alijitokeza wiki jana na kusema anataka kurejea nyumbani na kuwania urais wa taifa lake .
Islam mwenye umri wa miaka 49, katika mahojiano na gazeti la Marekani la New York Times, alizungumza kuhusu mambo mengi yanayohusiana na nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika ya Libya na siasa.
Mnamo Agosti 2011, takribani muongo mmoja uliopita, waasi walidhibiti mji mkuu wa Libya Tripoli. Baada ya hayo, mnamo Oktoba 2011, Gaddafi aliuawa kwa kupigwa risasi .
Saif al-Islam, aliyewahi kufikiriwa kuwa mrithi wa baba yake, anasema viongozi wa Libya "hawajaleta chochote ila mateso" kwa watu nchini Libya katika miaka 10 iliyopita.
Islam , ambaye alionekana baada ya miaka mingi, alisema, "Sasa ni wakati wa kurudi nyumbani nchi inaangamia ... hakuna pesa, hakuna usalama. Hakuna maisha."
Alifanya mahojiano haya na New York Times ndani ya jumba la kifahari la ghorofa mbili .
Islam alisema katika mahojiano hayo kuwa sasa yeye ni mtu huru na anajiandaa kurudi tena katika siasa .
Alidai pia kwamba watu ambao walikuwa wamemfunga jela hapo awali sasa wamekuwa 'marafiki' zake.
Atakubaliwa kurejea Libya?
Hatahivyo, kurudi kwa Islam nchini Libya hakutakuwa rahisi. Sio tu kwamba anakabiliwa na shutuma za uhalifu wa kivita dhidi ya binadamu katika mahakama ya ICC, anakabiliwa pia na hukumu ya korti moja ya Tripoli
The New York Times iliandika kwamba licha ya haya yote, mtoto wa Muammar Gaddafi Saif al-Islam anaonekana kuwa 'thabiti'.
"Nina hakika masuala haya ya kisheria yanaweza kutatuliwa ikiwa watu wa Libya watanichagua kuwa kiongozi wao," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Islam aliongeza , "Nimekuwa mbali na watu wa Libya kwa miaka 10. Ili kurudi, nitalazimika kufanya kazi polepole kama mchezaji densi anayeitikia mirindimo ya muziki . Kucheza na akili za watu kidogo."
Mnamo mwaka wa 2011, wakati alikuwa akikimbia kuokoa maisha yake, je! Hakuona ni ajabu kujificha katika nyumba za watu nchini Libya?
Kujibu swali hili, Islam ilisema, "Sisi ni kama samaki na watu wa Libya ni kama bahari kwetu. Bila wao tutakufa. Kutoka kwao tunapata msaada. Tunajificha hapa na kupigana hapa." . Watu wa Libya ni bahari zetu. " alisema Saif.
















