Fahamu ukweli kuhusu kikosi cha wanawake pekee kilichokuwa kikimlinda Muammar Gaddafi

kikosi

Chanzo cha picha, Reuters

Tangu kifo cha aliyekuwa kiongozi wa Libaya Muammar Gaddafi mikononi mwa kundi la waasi mnamo Oktoba 2011 mengi yameandikwa na kusemwa juu yake.

Lakini hakuna mengi yaliyosemwa kuhusu , kikosi cha walinzi wa kike ambao walikuwa akiandamana naye kote katika safari zake .

Alijulikana kwa kuwapenda wanawake na kiongozi huyo wa zamani wa Libya alioa mara mbili. Alikuwa na wake wawili, binti na mamia ya walinzi wa kike waliokuwa wakijihami vikali kwa bunduki.Kulikuwa pia na muuguzi wa Kiukreni na wafuasi wengi wanawake ambao walisimama karibu naye wakati wa maisha yake.

Mkewe wa kwanza, alikuwa mwalimu wa shule. Walitengana baada ya miezi sita na wana mtoto wa kiume - Muhammad. Mkewe wa pili, Safia al-Gaddafi, muuguzi kwa taaluma, ndiye mama wa wanawe wengine saba.

libya

Chanzo cha picha, Reuters

Walakini, kati ya wanawake wote maishani mwake, wale maarufu zaidi, labda, walioonyeshwa naye walikuwa walinzi wake wa kike waliozungumziwa sana. Jeshi lake la walinzi wanawake na timu za wauguzi wa kike zilimpatia umaarufu ulimwenguni.

Kulingana na ripoti, walinzi wake, pamoja na kuwa wanawake, walichaguliwa kwa kuwa mabikira. Kwa kuongezea, walipaswa kuchukua kiapo cha usafi na kuapa kuyatoa maisha yao kwa ajili yake. Inavyoonekana, walichukua viapo vyao kwa uzito - inasemekana hakuenda mbali naye mchana au usiku.

Walinzi hawa waliofunzwa walikuwa na ujuzi wa kijeshi na walikuwa wataalam katika utumiaji wa silaha, kulingana na ripoti mbali mbali za habari nje na ndani ya Libya. Jarida la Huffington lilisema wanawake hao walipata mafunzo mengi ya kijeshi na silaha katika chuo kikuu maalum kabla ya kuingizwa rasmi.

libya

Chanzo cha picha, Reuters

Gaddafi lazima alifikiri ilikuwa na maana kufundisha wanawake wazuri na kuwageuza kuwa wauaji. Wakiwa wamejipamba kuvutia na kuvalia viatu virefu katika nchi ambayo wanawake walivalia mavazi ya kiislamu hakika ni jambo ambalo liligeuza vichwa vya watu wengi

Walinzi wa Gaddafi walikuwa sawa na utawala wake. Angewatumia kama ishara ya imani yake katika ukombozi wa wanawake. Hata hivyo baadaye ufichuzi wa kutisha ulitolwa na baadhi ya wanawake waliokuwa katika kikosi hicho kwamba Gaddafi alikuwa akiwabaka na kuwafanyia unyanyasaji mwingine .

Ziara ya Gaddafi nchini Italia mnamo 2009 iligonga vichwa vya habari baada ya kutolewa mwaliko wa wasichana 500 wa kuvutia wa Italia kwa dhifa ya chakula cha jioni katika jumba ambamo Gaddafi alikuwa akilala .

Inasemekana alitumia hafla hiyo kuwashawishi wasichana hao wasilimu na akawapatia nakala ya kitabu chake cha Green Book.

Madai ya Ubakaji na unyanyasaji

Ripoti zilizoibuka baadaye zilidai kwamba walinzi hao wa zamani walisema Gaddafi na wanawe waliwabaka na kuwanyanyasa na kisha kuwatupa wanawake mara tu wanaume "walipokuwa wakichoka" nao.

Mwanasaikolojia aliyekuwa na makao yake katika mji wa Benghazi Seham Sergewa alikusanya maelezo ya kutumiwa na Korti ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC), ambayo ilichunguza uhalifu wa kivita wa Gaddafi na washirika wake.

Idadi kamili ya walinzi hao haikujulikana lakini walifika wanawake wapatao 400 na angesafiri na hadi walinzi 30 wa kike katika ziara za nje ya nchi yake .

libya

Chanzo cha picha, Reuters

Baada ya baadhi ya wanawake hao kujitokeza na madai kwamba waliakuwa wakibakwa ,wenzao kadhaa pia waliibuka na madai hayo .mtindo wa unyanyasaji wao ulikuwa ule ule.

Sergewa pia alichunguza madai kwamba wanajeshi wa Gaddafi walibaka wanawake wakati wa mzozo nchini humo uliosababisha kupinduliwa kwa serikali yake na kisha baadaye kuuawa .

Wanawake wengine walijitokeza wakisema walibakwa na wanajeshi 20 kwa wakati mmoja.

"Katika kisa kimoja, msichana, karibu miaka 18 au zaidi, alisema alibakwa mbele ya baba yake. Aliendelea kumwambia asimtazame, "Sergewa alisema.

Waathiriwa wengine wamejiua au walikuwa wakifikiria kujiua .

Mauaji ya Gadhafi

Wakati upepo wa uasi ulipoanza kuvuma katika ulimwengu wa Kiarabu kutoka Tunisia mnamo Desemba 2010, Libya haikuwa juu ya orodha ya watu wengi wa "nani afuataye".

Gaddafi kwa wengi alikuwa akionekana kama mtawala wa kimabavu ambaye alivumiliwa kwa miaka zaidi mingi kuliko idadi kubwa ya raia wake wanavyoweza kukumbuka. Lakini hakutambuliwa sana kama kibaraka wa magharibi kama viongozi wengine wa Kiarabu, walioshutumiwa kwa kuweka masilahi ya nje mbele ya maslahi ya watu wao wenyewe.

Gadhafi

Kadiri maasi yalilivyoenea, na uzito wa tishio kwa utawala wake kuonekana, Gaddafi alionyesha kuwa hakuwa amepoteza unyama wowote ulioelekezwa dhidi ya wapinzani na waliotoroka nchi miaka ya 1970 na 1980.

Wakati huu miji mizima na vijiji vililengwa kwa ukatili wake ambapo watu walikuwa wamethubutu kurarua mabango yake na kutoa wito kumalizika kwa utawala wake . Wanajeshi wa kawaida na mamluki karibu wangewazidi nguvu waasi ambao hawakuwa na mafunzo ya kutosha , wakiwemo wanajeshi waliotoroka vikosi vya Gaddafi chini ya mwavuli wa Baraza la Mpito la Kitaifa (NTC).

Kuingilia kati kwa Nato kwa upande wa waasi mnamo Machi, baada ya kuidhinishwa na azimio la UN lililotaka ulinzi wa raia, ulizuia maangamizi yao ambayo yalionekana kuwa karibu - lakini ilikuwa miezi kabla ya kugeuza hali hiyo kuwa faida kwao.

Kisha Tripoli ikaatekwa na waasi na Gaddafi akakimbilia mafichoni bado akidai watu wake walikuwa nyuma yake na kuahidi mafanikio dhidi ya "wavamizi" na "washirika". Utawala wake wa kidikteta ulikuwa umeporomoka, lakini wengi waliogopa kwamba angebaki huru ili kupanga uasi.

Alikutana na mauti yake kwa njia ya aibu na mbaya, wakati vikosi vya NTC vilipompata akijificha kwenye handaki kufuatia shambulio la ndege za Nato kwenye msafara wake alipojaribu kuondoka kutoka ngome yake ya mwisho, jiji la Sirte, ambapo yote yalikuwa yameanzia

Mazingira haswa ya kifo chake hayajawahi kufahamika iwapo "aliuawa katika ufyatulianaji wa risasi, aliuawa kwa kupigwa risasi , au aliuawa kwa kushambuliwa na umati kisha kuburuzwa mitaani na wapiganaji walioshangilia ushindi wao'

Utawala wake wa miaka 42 ulikomea hapo kwa njia ambayo wengi hawakuitarajia kwani mwanapinduzi huyo alikuwa ameingia madarakani kwa kishindo na kuongoza kimabavu bila kujali kwamba mauti yangempata kwa hali kama hiyo akiomba kusamewhewa na waliomkamata wengi wao wakiwa hata hawakuwa wamezaliwa wakati Gaddafi alipokuwa akipindua serikali kuchukua uongozi wa Libya