Samuel Doe: Rais wa Liberia alivyokamatwa na kuuawa na waasi mchana peupe

Liberia

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni mauaji ambayo yaliushangaza ulimwengu tarehe 9 septemba mwaka wa 1990. Hakuna aliyewahi kufikiria kwamba rais wa nchi angeweza kukamatwa na waasi ,wampige risasi ,wamnyanyase kwa saa kadhaa ,wamkate masikio na kisha wamuue katika hali ya kutatanisha .

Hiyo ndio iliyokuwa hatima ya rais wa Liberia, Samuel Doe mwaka wa 1990 ,baada ya kuwa uongozini kwa miaka kumi iliyojaa umwagikaji wa damu na ukatili ambao haukuwa umewahi kushuhudiwa Afrika magharibi .

Kuingia madarakani

Doe aliingia madarakani katika mapinduzi ya kijeshi Aprili mwaka wa 1980 akiwa na umri mdogo wa miaka 29 . Hakuwa na elimu na utawala wake ulitajwa kama uliozongwa na ufisadi na ulijaa ukatili uliosababisha watu wengi kuuawa katika mazingira yasiyoeleweka . Alishtumiwa kwa kuwapendelea watu wa kabila lake la Krahn na washirika wao wa kabila la Mandingos huku akiwakandamiza watu wa makabila ya Gio na Mano

Katika siku aliyokumbana na kifo chake Doe alikuwa ametoka katika jumba lake karibu na bandari ya mji mkuu Monrovia kwenda kumuona kamanda wa vikosi vya kulinda amani nchini humo .

Mkuu wa mojawapo ya makundi ya waasi Prince Johnson aligundua kuja kwake na pamoja na wapiganaji wake walielekea katika eneo hilo .

Matokeo yake muda mfupi baadaye ni walinzi takriban 60 wa Doe kuuawa -naye akapigwa risasi katika miguu yake yote.

Aliburutwa na kuingizwa katika gari la waasi ambao baadaye walimkata masikio ,kumtesa na wakamuua .

Charles Taylor

Chanzo cha picha, AFP

Waasi wakiongozwa na Charles Taylor na Prince Johnson walikuwa wameanzisha harakati za kumuondoa Doe madarakani na kwa miezi mitatu alikuwa amejifungia katika jumba lake la Monrovia akiwa amezingirwa na walinzi waliojihami vikali. Kuna uvumi kuhusu jinsi Doe alivyosalitiwa na mmoja wa washirika wake wa karibu kutoka nje kabla ya waasi kumpata na kumkamata .

Mwandishi wa BBC aliyekuwa katika makao makuu ya kikosi cha walinda amani cha Afrika Magharibi alishuhudia tukio hilo zima hadi rais Doe alipochukuliwa na waasi huku miili ya walinzi wake ikiachwa imetapakaa kote katika ofisi za makao hayo .

Prince Johnson alisema rais Doe angeshtakiwa na kuhukumiwa lakini ulimwengu haukujua kwamba hukumu yake ingekuwa kifo na ingejiri siku hiyo hiyo . Picha za video zilimuonyesha rais akipiga magoti akimlilia Prince Johnson kumsamehe na yamkini ombi lake hilo la huruma halikumshtua Johnson .

WAASI

Chanzo cha picha, AFP

Matukio kabla ya mauaji ya Doe

1989: Charles Taylor anaanza uasi dhidi ya rais Samuel Doe

1990: Doe auawa kikatili na waasi

1997: Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinafika kikomo -watu 250,000 wanaripotiwa kufariki.Taylor achaguliwa kuwa rais

2012: Taylor apatikana na makosa ya uhalifu wa kivita uliotekelezwa nchi jirani ya Sierra Leone

Ilikuwa kama filamu

Milio ya risasi iliripotiwa kuzuka muda mfupi baada ya Doe kuondoka katika jumba lake la kifalme kwa ziara isiyopangwa kwa makao makuu ya Mghana Jenerali Arnold Quainoo, kamanda wa jeshi la Afrika Magharibi, kulingana na BBC.

Johnson na baadhi ya vikosi vyake walimfuata Doe, na ugomvi ukaibuka ambao ukawa ufyatulianaji wa risasi wa muda mrefu , uliohusisha kurushwa kwa magruneti , ripoti ya BBC ilisema. Wanajeshi wa Johnson walimjeruhi Doe na kumpeleka kwenye kambi yao, iliongeza.

Tukio la siku hiyo lilikuja siku chache tu baada ya Doe na Johnson kuripotiwa kukubaliana rasmi kusitisha mapigano, ambayo yalisababisha vifo vya watu 5,000 na kuwaacha zaidi ya watu 500,000 wakiwa hawana makazi. Doe na Johnson wote wawili walikuwa wamekaribisha juhudi za kulinda amani za Afrika Magharibi.

Liberia

Chanzo cha picha, Getty Images

Johnson na mamia ya wanajeshi waasi walijitenga kutoka kwa jeshi kuu la waasi la Liberia lililoongozwa na Charles Taylor miezi kadhaa iliyopita.

Taylor, aliyedai wakati mmoja kuwa ndiye rais wa Liberia alikuwa ameapa kupigana dhidi ya kikosi cha walinda amani cha Afrika magharibi cha wanajeshi 4000, wanajeshi wa Doe na kundi la waasi la Johnson . Taylor alikuwa kila mara akisema katika mahojiano na wanahabari kwamba lengo lake lilikuwa kumkamata rais Doe na kuupindua utawala wake .

Kulikuwa na madai ya kila mara ya uongo kutoka kila upande kuhusu kukamatwa kwa Doe au mmoja wa kiongozi wa waasi .Mnamo agosti 14 wapiganaji wa Taylor walidai kwamba walikuwa wamemkamata Johnson lakin baadaye alijitokeza katika kikao na waandishi wa habari

Prince Johnson

Kiongozi huyo wa zamani wa waasi ndiye anayelaumiwa kwa mauaji ya Samuel Doe na ulimwengu hautasahau picha yake ya video akinywa pombe wakati Doe alipokuwa akimuomba asimuue . Kwa sasa Johnson ni seneta nchini Liberia

Wakati mmoja alitaka kugombea urais hatua iliyozua hisia mbali mbali kutokana na historia yake na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo .

Baadaye alijiingiza katika uraibu wa pombe na dawa za kulevya lakini akaibuka miaka kadhaa akiwa ameokoka . Alikimbilia mafichoni nchini Nigeria kwa miaka 11 wakati aliposhindwa na Charles Taylor walipokuwa wakipigania madaraka .