Mwanamume amrejeshea fahamu mwanatembo aliyegongwa na piki piki
Mwanatembo aliyegongwa na piki piki alipokuwa anavuka barabara nchini Thailand aliponea kifo baada ya kuokolewa na mfanyakazi wa uokozi ambaye hakuwa kazini.
Mana Srivate aliambia shirika la habari la Reuters kwamba amewahi kuwaokoa wanyama mara kadhaa katika kazi yake - lakini hajawahi kumuokoa tembo.
Katika kanda ya video iliyopata umaarufu mtandaoni anaonekana akimsaidia mwanatembo aliyelala chini kwa ubavu wake akiwa amezirai katikati ya barabara iliyokuwa na giza.
Mwanatembo huyo alisimama baada ya dakika 10.
Alikuwa akijaribu kuvuka barabara na kundi la tembo wenzake katika mkoa wa Chanthaburi mashariki mwa Thailand.
Katika video, Wafanyakazi wenza wa Bw. Mana pia wanaonekana wakimhudumia mwendesha piki piki aliyejeruhiwa kidogo kufuatia ajali hiyo.
Bw. Mana, ambaye amekuwa akifanya kazi ya uokozi kwa miaka 26, aliambia Reuters alifika katika eneo la ajali usiku wa Jumapili akiwa safarini japo hakuwa kazini.
"Niliamua kuokoa maisha ya tembo huyo mdogo, lakini nilikuwa na hofu muda wote huo kwa sababu nilikuwa nikiskia mlio wa mama yake na tembo wengine wakimtafuta mtoto," Bw. Mana aliambia shirika hilo la habari kwa njia ya simu.
"Nilikisi moyo wa tembo uko wapi kwa kutumia nadharia ya ilipo moyo wa binadamu kama ulivyoona katika kanda ya video iliyosambazwa mtandaoni.
"Wakati mwanatembo alipopata fahamu na kuanza kutikisika, Nilikuwa karibu kulia," alisema.

Chanzo cha picha, Reuters
Mwanatembo huyo alisimama baada ya karibu dakika 10 na kupelekwa katka eneo lingine kwa matibabu, kabla ya kurejeshwa katika eneo la ajali kwa matumaini y akumpata mama yake,Reuters iliripoti.
Tembo wengine walirejea wakati walipomsikia mama yake akitoa mlio wa kumtafuta, Bw. Mana aliambia shirika hilo la habari.
Aliongeza kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kumuokoa tembo kupitia ufufuo wa moyo.















