Spika Ndugai: Wabunge wa Chadema tunawatambua kuwa wabunge kamili

Chanzo cha picha, Bunge
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewaapisha wabunge wateule Bw. Humphrey Polepole na Bi. Riziki Said Lulida kuwa wabunge kamili , na kutoa onyo kwa wale wanaodharau na kukebehi shughuli za Bunge.
Bw. Humphrey polepole alikuwa Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza baada ya kuwaapisha wabunge wateule, Spika Ndugai amekemea vikali watu wanaodharau shughuli zinazofanywa na Bunge la Tanzania
"Wako rafiki zetu ambao hivi karibuni wamejipambanua kwa kukejeli shughuli za bunge, niwatahadharishe na kuwakumbusha labda wamesahau kuwa ni jambo lisilokubalika kwa mtu yoyote, kudharau shughuli za bunge, kudhalilisha bunge, kudhalilisha uongozi wa bunge na hata kudhalilisha wabunge waliokwisha kuapishwa.
Amesema maboresho ya kanuni inayosimamia kiapo yanamuwezesha mbunge mpya kutekeleza kazi za kibunge na kuwajibika kwa wananchi mara tu baada ya kuchaguliwa kwake au kuteuliwa kwake.
Kwa utaratibu wa zamani, Ndugai amesema ilibidi wateuliwa hao wakae bila kufanya kazi za kibunge, hadi Februari 2 mwaka 2021, lakini kwa mabadiliko haya yaliyofanyika kwenye bunge lililopita yanawawezesha sasa baada ya kula kiapo kuanza kufanya kazi moja kwa moja kama ilivyo kwa wabunge wengine wote walioapishwa tangu kuanza kwa bunge la 12.
''Shughuli za bunge huwa hazisimami ndio maana wabunge huchaguliwa kwa miaka mitano. Hakuna muda ambao mbunge yuko likizo au bunge kuwa likizo, hakuna''. Alisema Spika Ndugai.
Kwa hiyo wabunge wote wa bunge la 12 tuliowaapisha tunaendelea kuwatambua kuwa wabunge kamili wakiwemo 20 wa chama cha Chadema.
19 wa kuteuliwa na mmoja wa kuchaguliwa, Aida Kenani
''Nashangaa wanawasonga tu hawa 19 yule mmoja wamemgwaya? wakiweza wamfukuze basi, lakini sisi tumeshamwapisha na tunamtambua kwamba ni mbunge, hayo yanayoendelea huko ni ya kwao'',alisema Spika Ndugai.
Ndugai amewatoa wasiwasi waliokuwa wakifikiri kuwa wabunge 19 wateule si halali, akisema kuwa wale ni wabunge kamili.
''Na niwakumbushe wanahabari kuwa kila mnapotamka majina yao muanze kwa jina 'Mheshimiwa' kwa kuwa ni kanuni ya Bunge.''
'Ukandamizaji dhidi ya wanawake'
Spika Ndugai amewasihi Watanzania kukataa na kupiga vita ukandamizaji dhidi ya wanawake kwa kisingizio chochote kile.
Kiongozi huyo amekemea kitendo cha Mwenyekiti wa chama cha Chadema Freeman Mbowe kusimama hadharani na kuwatukana wabunge wanawake.
''Kwa mtu mzima na mwanaume wa Kitanzania uliyefundwa ni aibu kubwa kutukana wanawake hadharani, ningependa kuchukua nafasi hii kumuonya na kumkanya mwenzangu asione sifa jambo hili, wanawake ni mama zetu, dada zetu, shangazi zetu na hata kama wamekosea namna gani tuwatafute na kukaa nao ili kupata maelezo yao, na si kuwafukuza kama vibaka na kuona fahari katika kufanya hivyo''.
Pia amemuonya mbunge wa zamani wa chama hicho kwa kitendo chake cha kuwatukana wanawake wenzake akiwaita 'Covid-19'.
''Yeye mwenyewe ni mwanamke anatukana wenzake namna hii, inasononesha unaona kweli safari ya wanawake bado ni ndefu kufikia mnakotaka kufika, hamjui nyinyi wale 19 wamepitia mapito gani, hamjui kwa nini imekuwa ilivyokuwa, ni ngumu, yako mambo hatuwezi kusema humu.
''Viko vyama ni kampuni ya mtu, mtu ni mungu mtu bila yeye hakiwezekani chochote na kwa masharti yoyote atakayoweka''.
Spika Ndugai amesema wabunge 19 ni wabunge kamili labda wao wenyewe waamue kwa kutumia utaratibu wa kikatiba kujiuzulu
''Lakini kwa yeye na Mnyika wake, wale ni wabunge...hawawezi wao na genge lao la wanaume wakaweza kufanya hivyo kwa dada zetu hata tuwe vyama tofauti hata kabila , rangi tofauti lakini ubaguzi wa aina hii wa kijinsia unatakiwa upigwe vita na Watanzania wote.''
Hivi kweli rafiki yangu Freeman Mbowe, umesahau, Mh Halima alivyovunjika mkono kwa sababu ya kukufuata Magereza umesahau? Esther Bulaya alipopigwa akazimia na kupelekwa Aga Khan hajitambui kwa ajili yako? Esther Matiko amelazwa Segerea mara ngapi kwa ajili yako? Ningeweza kumtaja kila mmoja jinsi walivyosota kwa ajili ya wewe Mbowe, mshahara wao ni kufukuzwa hadharani kwa utaratibu ule usiokuwa wa ki utu? Haiwezekani!.Alisema Spika Ndugai.
Freeman Mbowe alisema nini alipowafukuza uanachama wa Chadema
Mbowe alisema kamati kuu iliyoketi, imeona na imeridhishwa na ukweli kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa katiba ya nchi , sheria za nchi na kanuni zinazosimamia masuala ya uchaguzi zilizokiukwa katika mchakato mzima wa uchaguzi huo hususani katika jambo zima linalohusu viti maalum.
''Tumejiridhisha katika uvunjaji huu wa katiba, sheria na kanuni kama kamati kuu ya chama cha upinzani Chadema, lazima tulifahamishe taifa baada ya kujiridhisha sisi wenyewe baada ya vikao vya ndani va chama kuhusu mapungufu kadhaa yaliyofanyika katika mchakato huu.''
Mbowe ameainisha Mapungufu ya kisheria aliyosema yako dhahiri katika mchakato wa uteuzi wa wabunge wa viti maalumu
Ibara ya 78 (3) inasema majina ya watu waliopendekezwa na tume ya uchaguzi yatatangazwa kama matokeo ya uchaguzi, baada ya tume ya uchaguzi kuridhika kwamba masharti na sheria vimezingatiwa.
Ibara ya 67 (1b) imeweka masharti na sifa ya mtu kuteuliwa kuwa mbunge kuwa lazima awe amependekezwa na chama cha siasa.
Mbowe amesema kuwa huwezi kupendekezwa na chochote kingine kwa mujibu wa sheria za nchi , isipokuwa na chama cha siasa.
Hivyo Mbowe amesema kuwa chama chao hakijateua wabunge, na kuwa hawajui mchakato huo ulivyokwenda.
''Tunaona watu wetu wanaapishwa, hatuwajui, fomu zinazopaswa kujazwa na kuletwa kwenye chama, ili katibu mkuu wa chama chetu aweze kuziidhinisha, hatujawahi kuzijaza, fomu ziko ofisini, tunaona wabunge wetu wanaapishwa''.
Mbowe alitangaza kuwafuta uanachama wabunge hao wateule na kuwavua nyadhifa zao zote ndani ya chama.
Kwa upande wa viongozi ndani ya kundi hilo la watu 19 ''Kamati imeona hawana sifa hata moja kuendelea kushika nafasi yoyote ya uongozi wa chama hiki kwa mazingira haya, kwa hiyo tumewavua mamlaka yote katika chama''. alisema Mbowe












