Mzozo wa Tigray Ethiopia: Debretsion Gebremichael, mtu anayepigania Tigray kujitenga na Ethiopia

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbabe wa kivita wa zamani ambaye alikuwa akivuruga mtandao wa mawasiliano ya majeshi ya Ethiopia, Debretsion Gebremichael sasa anaongoza mapigano dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kudhibiti eneo la kaskazini la Tigray, linalotajwa kama "uzao" wa nchi.
Bwana Debretsion anaongoza Tigray People's Liberation Front (TPLF), chama ambacho kinaongoza eneo la Tigray, ambacho kimetofautiana vikali na Bw. Abiy.
Ikiwa sasa ni mume na baba wa mtoto mdogo, Bw. Debretsion alikatiza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa miaka ya 1970 kujiunga na TPLF katika mapambano yake ya miaka 17- dhidi ya utawala wa kimabavu wa Mengistu Haile Mariam.
Baadaye alikuwa waziri wa serikali baada ya Derg kushindwa na uongozi wa nchi kuchukuliwa na muungano wa vyama ambavyo vilitawaliwa TPLF hadi Bw. Abiy alipoingia madarakani mwaka 2018.
Mwandani wake wa karibu Alemayehu Gezahegnalisema baada ya kukamilisha pamoja mafunzo ya kijeshi katika milima ya Tigray, akiangazia uwezo wa kiufundi wa mwenzake, alipendekeza kwa makamanda wa TPLF kwamba Bwana Debretsion anapaswa kupelekwa kwa "kitengo cha ufundi".

Chanzo cha picha, TPLF Museum
Kwa Bwana Alemayehu, hapo palikuwa mahali pazuri kwa Bwana Debretsion, kwani alikuwa mwerevu, lakini ''kijana mpole wa mjini'' ambaye alikulia huko Shire, ambayo kwasasa iko chini ya udhibiti wa vikosi vya muungano.
Hatua ambayo ni pigo kubwa kwa kiongozi wa Tigray.
'Alitengezea taa kutokana na mabaki ya vifaa ya umeme'
Kiongozi huyo wa Tigray anayetokea familia ya Kikristo ya Orthodox, alipewa jina la Debretsion, linalomaanisha Mlima Sayuni, huku jina lake la pili likiwa ni la baba yake, Gebremichael, likimaanisha Mtumishi wa Mtakatifu Michael.
"Alipokua katika shule ya msingi, alikuwa akikusanya betri kuu kuu, radio, vifaa vinavyotumia umeme na kuzitengeza. Wakati hakuna mtu yeyote aliyekuwa akitumia nguvu za umeme katika mji wetu, lakini alijitengezea taa kutokana na na mabaki ya vifaa hivyo," Bwana Alemayehu alisema.
Bwana Debretsion alijipati aufanisi katika "kitengo cha ufundi" cha TPLF, ambapo alitekeleza jukumu muhimu la kukuza uwezo wa ujasusi wa TPLF na kuiwezesha kusikiza mazungumzo ya jeshi la Ethiopia na kubana mawasiliano yao ya redio
"Hatua hii ilituwezesha kushinda kwasababu wapiganaji wa uhuru wa TPLF walikuwa na ufahamu kuhusu hatua zinazochukuliwa na maadui mapema na kubana mawasiliano yao wasiweze kujulishana waliposhambuliwa," Bwana Alemayehu alisema.
Ili kuendeleza zaidi ujuzi wake, Bwana Debretsion alisafiri Italia kwa kutumia hati bandia ya usafiri na baadae akarejea kuanzisha kituo cha kwanza cha redio cha TPLF - kilichofahamika kama Dimtsi Weyane, kumaanisha Sauti ya Mapinduzi.
'Aliponea kifo baada ya kuteleza mlimani'
Mpiganaji mwingine wa kuvizia wa TPLF, Measho Gebrekidan, anakumbuka kuwa walikuwa wakienda pamoja milimani nyakati za usiku waka ambapo ni nadra sana kuonekana na majasusi wa wa serikali kwenda kuweka mitambo yao ya mawasiliano.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Usiku mmoja, aliteleza... na ni mimi na mwenzangu tulimuokoa. Wakati wote najiuliza ikiwa ajali hiyo ingetokea, je hii redio ingelikuwepo?" Bwana Measho amesema.
Sasa kituo cha redio cha Dimtsi Weyane ni sehemu kubwa ya mtandao wa mawasiliano uliyo na makao yake katika mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle, likitangaza taarifa za PTLF kuhusu oparesheni dhidi ya vikosi vya serikali kuu.
Kituo hicho kimekuwa kikimkosoa Bwana Abiy, na mzozo ulipoanza matanazo yake yalikatizwa, lakini Dimtsi ilirejea hewani siku moja baadaye.
Mpinzani wa Abiy katika wadhifa wa waziri mkuu
Bwana Debretsion na Bwana Abiy walionekana kuwa marafiki mwanzoni waziri mkuu alipoingia madarakani mwaka 2018. Kiongozi wa Tigray pia alipanga hafla kubwa kumkaribisha waziri mkuu mjini Mekelle.

Chanzo cha picha, EPA
"Tigray ni mahali ambapo historia ya nchi yetu ilipopikwa, na ni eneo ambapo wa wavamizi wa kigeni [miongoni mwao Waitaliano na Wamisri] waliposhindwa na kufedheheshwa.
Katika Ethiopia ya sasa, ni uzao wa Ethiopia," Bwana Abiy alisema mwaka 2018.

Kwa upande wake, Bwana Debretsion alimpongeza waziri mkuu wa juhudi zake za kuweka amani na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki kukomesha "mzozo wa muda mrefu" ambao ulidumu kati ya nchi hizo mbili tangu kumalizika kwa mzozo wao wa mpakani mwaka 1998-2000.
"[Bwana Abiy] alizuru Eritrea na kukutana na Isaias. Hatua hiyo ilikuwa vigumu sana kwa miaka mingi. Ni mkataba ambao utatoa nafasi kubwa kwa nchi," Bwana Debretsion alisema mkataba wa amani ulipofikiwa.
Lakini ishara hiyo ya ushirikiano kati ya viongozi hao wawili iligubikwa na taharuki iliyokuwa ikitokota kati yao.
Bwana Debretsion alikuwa na azma ya kuwa waziri mkuu lakini juhudi hizo zikalemazwa na uteuzi wa Bwana Abiy mwaka 2018 katika kinyang'anyiro kilichoandaliwa ndani ya muungano tawala.

Pia unaweza kutazama:

Mambo matano kuhusu Tigray:
1. Ufalme wa Aksum uko katika eneo hilo.Ilielezewa kama moja ya ustaarabu mkubwa wa ulimwengu wa zamani, wakati mmoja ilikuwa serikali yenye nguvu kati ya milki za Kirumi na Uajemi.

Chanzo cha picha, Getty Images
2. Magofu ya mii wa Aksum yametambuliwa na Umoja wa Mataifa kama eneo la turathi za kale duniani. Eneo hilo ambalo limekuwepo kati ya karne ya kwanza hadi ya tatu AD, linajumuisha , makasri, makaburi ya wafalme na kanisa linaloaminiwa na baadhi ya watu kuwa sanduku la agano (Ark of the Covenant).
3. Watu wengi katika eneo la Tigray ni Wakristo wa dhehebu la Orthodox Ethiopia.Mzizi wa Dini ya Kikristo ulianza kuchipuka miaka 1,600 iliyopita.
4. Lugha kuu katika eneo hilo ni Tigrinya, lahaja ya Kisemeti ina wasemaji wasiopungua milioni saba ulimwenguni.
5. Ufuta ni zao kuu la biashara, unasafirishwa Marekani, China na nchi nyingine.
















