Kwanini kesi ya yaya aliyekabiliana na milionea imezua hisia Singapore

Collage of Parti Liyani and Liew Mun Leong

Chanzo cha picha, Parti Liyani/Getty

Maelezo ya picha, Bi. Parti (kushoto) alifanyakazi kwa Bwana Liew Mun Leong (kulia) kwa miaka mingi

Alikuwa mfanyakazi wa ndani kutoka Indonesia ambaye alikuwa akipokea mshahara wa S$600 sawa na (£345) kwa mwezi kwa kufanyia kazi familia moja tajiri nchini Singapore.

Alikuwa ameajiriwa na mfanya biashara milionea wa Singapore na mwenyekiti wa makampuni makubwa nchini humo.

Siku moja, familia yake ikamtuhumu kwa wizi. Waliwasilisha ripoti polisi katika kesi ambayo iligonga vichwa vya habari kwa madai ya wizi wa vibeti vya kifahari, mashine za kucheza DVD na hata nguo.

Mapema mwezi huu, Parti Liyani hatimaye aliondolewa mashitaka.

"Nashukuru hatimaye niko huru," aliwaambia wanahabari kupitia mkalimani. "Nimekuwa nikipigania haki kwa miaka minne."

Lakini kesi yake imeibua suala la usawa na utekelezaji wa haki nchini Singapore, huku wengi wakihoji ni kwa namna gani alipatikana na makosa.

Bi Parti alianza kufanya kazi katika nyumba ya Bw.Liew Mun Leong mwaka 2007, ambako jamaa kadhaa wa familia yake akiwemo kijana wake wa kiume Karl walikuwa wakiishi.

Machi mosi 2016, Bw. Karl Liew na familia yake walihama kutoka nyumba hiyo na kwenda kuishi mahali pengine.

Nyaraka za mahakama zilizo na maelezo kuhusu mambo yalivyojiri zinasema kuwa Bi. Parti aliombwa kusafisha nyumba mpya ya muajiri wake pamoja na ofisi "mara kadhaa" - hatua ambayo inakiuka kanuni za ajira na kwamba aliwahi kulalamikia.

Miezi kadhaa baadae, familia ya Liew ilimfahamisha Bi.Parti kuwa amefutwa kazi, kwa madai kwamba anawaibia.

Lakini wakati Bw.Karl Liew alipomwambia Parti kwamba amesimamishwa kazi, inaripotiwa kuwa alimwambia: "Najua kwa nini. Umekasirika kwa sababu nimekataa kusafisha choo chako."

Alipewa masaa mawili kufungasha virago vyake na kuweka kwenye masanduku kadhaa ili itumwe kama mzigo hadi Indonesia na familia. Yeye pia alisafiri kwenda kwao siku hiyo hiyo.

Alipokuwa anafunganya virago vyake alitisha kuwasilisha malalamiko yake kwa mamlaka za Singapore kwamba alikuwa anaombwa kusafisha nyumba ya Karl Liew.

Familia ya Liew iliamua kuangalia mizigo yake baada ya Bi Parti kuondoka, na kudai kuwa walipata vitu vyao ndani ya mizigo hiyo. Bw. Liew Mun Leong na mwanawe wa kiume waliandikisha taarifa polisi Oktoba 30.

Bi. Parti anasema hakuwa na habari kuhusu hilo - hadi wiki tano baadae aliporejea Singapore kutafuta kazi mpya, ambapo alikamtwa alipowasili nchini humo.

Kwasababu hakuweza kupata kazi kutokana na rekodi ya uhalifu dhidi yake, alilazimika kuishi katika makazi ya wafanyakazi wahamiaji na kutegemea msaada wa kifedha akisubiri kesi yake kusikizwa na kuamuliwa.

Alidaiwa kuiba nini?

Bi Parti alituhumiwa kwa kuiba vitu kadhaa kutoka kwa nyumba ya Liews ikiwemo nguo 115, vibeti vya kifahari, DVD na saa ya thamani.

Kwa jumla thamani ya vitu hivyo vyote ilikuwa dola 34,000 za Singapore.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake alijitetea akisema kwamba vitu anavyodaiwa kuiba, vingine vilikuwa vyake ama vya kuokota baada ya kutupwa. Pia alisema vitu vingine ni vya kusingiziwa hakuweka mwenyewe kwenye sanduku.

Mwaka 2019, jaji wa mahakama wa ngazi ya wilaya alimpata na makosa na kumhukumu kifungo cha miaka miwili na miezi miwili jela. Bi. Parti aliamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Kesi hiyo iliendelea hadi mapema mwezi huu ambapo mahakama ya Juu ya Singapore ilipomuondolea makosa.

Jaji Chan Seng Onn alijiridhisha kuwa familia hiyo ilikuwa na "njama fiche" katika mashitaka yao dhidi yake ikizingatia mambo kadhaa kama kwa mfano jinsi polisi, waendesha mashtaka na pia jaji walivyoshughulikia kesi hiyo.

Alisema kuna sababu ya kuamini kuwa familia ya Liew iliandikisha taarifa kwa polisi ili kumzuia asiripoti malalamiko yake kwamba alikuwa akiambiwa asafishe nyumba ya Bw. Karl Liew kinyume na sheria.

Jaji alisema baadhi ya vitu ambavyo Bi Parti alidaiwa kuiba vilikuwa vimeharibika kama vile saa ambayo ilikuwa haina kifuniko upande wa chini, na simu mbili aina ya iPhone ambazo zilikuwa hazifanyi kazi - na kusema kuwa ni "nadra" kuiba vitu vilivyoharibika.

Pioneer DVD player

Chanzo cha picha, HOME

Maelezo ya picha, Inadaiwa kwamba Parti aliiba mashini ya kucheza DVD anayosema ilikuwa imeharibika

Jaji Chan pia alihoji hatua ya Bw. Karl Liew kuwa shahidi katika kesi hiyo.

Jaji Chan pia alihoji hatua iliyochukuliwa na polisi - ambao hawakufika katika eneo la tukio hadi baada ya karibu wiki tano baada ya ripoti ya kuandikishwa.

Polisi pia walikosa kumpatia mkalimani anayeongea lugha ya Kiindonesia na badala yake wakampatia yule anaongea lugha ya Malay, ambayo ni tofauti na lugha anayojua Bi Parti.

"Mwenendo wa polisi ni wa kutiliwa shaka hasa ikizingatiwa jinsi walivyofanya uchunguzi," Eugene Tan, Mhadhiri wa somo la sheria katika chuo Singapore aliambia BBC.

"Jaji wa mahakama ya wilaya inaonekana aliamua kesi bila kufuatilia kwa makini hatua ambazo huenda zilikuwa na dosari katika uchunguzi wa polisi na waendesha mashtaka."

Vita vya Daudi na Goliathi

Kesi hiyo ilizua gumzo kali nchini Singapore huku hasira zikielekezewa Bw. Liew na familia yake.

Baadhi ya watu wanaamini kesi hiyo ni mfano wa jinsi matajiri wanavyo wanyanyasa watu masikini.

Japo haki hatimaye ilitendeka, kwa baadhi ya raia wa Singapore iliwabainishia hofu yao kwamba mfumo wa sheria umetekwa na wenye fedha na kwamba mnyonge hana haki ikizingatiwa jinsi ilivyoendeshwa kwa njia ya upendeleo.

"Kesi kama hii ishawahi kushuhudiwa tena hivi karibuni," alisema Profesa Tan.

"Kosa la kimfumo na uzembe wa polisi na waendesha mashtaka katika kesi hii umefanya watu kuwa na ghadhabu.

Swali ambalo baadhi ya watu wanajiuliza ni: laiti ningelikuwa katika hali yake? Je kesi ingelichunguzwa bila upendeleo… na kesi kuamuliwa bila kuegemea upande wowote?

Hatua ya familia ya Liew kuweza kushawishi polisi na mahakama ya chini kwa kutumia madai ya uwongo imeibua swali ikiwa uchunguzi ulikuwa huru."

Kutokana na shinikizo na ukosoaji wa ummao, Bw. Liew Mun Leong alitangaza kustaafu kutoka wadhifa wake ama mwenyekiti wa kampuni kadhaa za kifahari.

Katika taarifa alisema, "anaheshimu" uamuzi wa Mahakama Kuu na kwama ana imani na mfumo wa sheria wa Singapore. Lakini pia akatetea uamuzi wake wa kuandikisha taarifa polisi, akisema: "Naamini kwamba ikiwa kuna hofu huenda kuna kosa limefanyika, ni jukumu letu la kupiga ripoti na kuwasilisha siala hilo".

Bwana Karl Liew amesalia kimya na hajawahi kutoa tamko lolote kuhusiana na suals hilo.

Kesi hiyo imefanya mchakato wa polisi kumfikisha mtu mahakamani kuchunguzwa umpya. Waziri wa Sheria maswala ya kijamii K Shanmugam amekira "disari ilitokea katika msururucwa matukio".

Kile serikali itafanya baada ya hapo ni kufuatilia kwa karibu suala hilo. Ikiwa itashindwa kushughulikia matakwa ya Wasingapore "Uwajibikaji na usawa", basi hali hiyo huenda "ikajenga taswira ya kwamba wanaojiweza wanaweka maslahi yao mbele kuliko ya jamii," aliandika mchambuzi wa wa maswala ya kijamii Donald Low hivi karibuni.

"Gumzo lililoibuka ni la iwapo watu wenye mali ama wenye ushawishi wameingilia mifumo ya serikali na kufichua uozo katika maadi ya kijamii,"mwandishi wa habari wa zamani wa PN Balji alisema katika uchambuzi mwingine.

"Ikiwa suala hilo halitashughulikiwa kikamilifu, basi juhudi za msaidizi, wakili, mwanaharakati na jaji zitakuwa zimepotea bure."

Kesi hiyo pia imeibua hali inayowakabili wafanyakazi wahamiaji kupata haki.

Bi Parti akiweza kuishi Singapore na kupigania kesi yake kutokana usaidizi aliyopata kutoka kwa shirika lisilokuwa la kiserikali la Home, pamoja na wikili Anil Balchandani, ambaye aliamua kumwakilisha bila malipo ya huduma zake za kisheria ambayo ingelikuwa dola 150,000 za Singapore.

PICHA.......

Anil and Parti

Chanzo cha picha, Home/Grace Baey

Maelezo ya picha, Bwana Balchandani na Bi. Parti wamekuwa wakipambana kwenye kesi hiyo kwa miaka kadhaa

Singapore hutoa msaada wa kisheria kwa wafanyakszi wahamiaji, lakini kwasababu wao ndio wanakimu familia zao, baadhi ya wale wanaokabiliwa na mashitaka huamua kutofuatialia mchakato huo wa kisheria, kwani hawana uwezo wa kurudi makwao na kukas miazi kadhaa au mwaka bila kipato, kwamujibu wa Wizara husika.

"Parti aliwakilishwa na wakili wake ambaye… alikabiliana na vigogo serikalini. Haikuwa rahisi," alisema Prof Tan.

"Ilikuwa mapambano ya Daudi na Goliath - ambapo Daudi aliibuka na ushindi."

Bi Parti, amesema sasa atarudi nyumbani.

"Kwa sababu sasa, matatizo yamekwisha, nataka kurudu Indonesia," alisema katika mahojiano na vyombo vya habari.

"Namsamehe mwajiri wangu. Namuomba tu asiwafanyie wafanyakazi wengine kitendo alichonifanyia."