Kambi za kijeshi za Marekani zashambuliwa kwa makombora Iraq

Chanzo cha picha, IRIB
Iran imefanya mashambulio ya makombora dhidi ya ngome za kijeshi za Marekani nchini Iraq kama hatua ya kilipiza kisasi mauaji ya jenerali Qasem Soleimani .
Makombora kadhaa yaliyorushwa kutoka Iran yalilenga eneo la Irbil na Al Asad, magharibi mwa mji wa Baghdad.
Runinga ya kitaifa ya Iran imetangaza kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu Qasem Soleimani aliyeuawa katika shambulio la ndege isiyokuwa na rubani mjini Baghdad, kufuatia agizo la rais wa Marekani Donald Trump.
Rais Trump ameandika katika Twitter yake akisema kwamba mambo ni shwari na kuongeza kuwa nchi yake kwa sasa inatathmini kiwango cha athari ya mashambulio hayo.
Kambi hizo mbili za kijeshi za nchini Iraq ambayo ni makao ya vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Marekani zililengwa- moja ya Al Asad na nyingine mjini Irbil zilishambuliwa saa kadhaa baada ya mazishi ya Soleimani.
Kambi ya Al Asad- ambayo iko mkoa wa Anbar magharibi mwa Iraq - ilishambuliwa na makombora karibu sita.
Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Khamenei amesema shambulio hilo lilikuwa "kofi la usoni" kwa Marekani.
"Tukizungumzia makabiliano ya kijeshi shambulio hili ni mzaha. Cha msingi kwa sasa ni kuhakikisha uwepo wa Marekani katika eneo letu lazima ufike mwisho," alisema.
Je huundio mwisho wa mapambano?
Hili ndilo shambulio la Iran la moja kwa moja ldhidi ya Marekani tangu kutekwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran mwaka 1979.
Jeshi la ulinzi la Iran Revolutionary Guard limesema kuwa shambulio hilo ni la kulipiza kisasi kifo cha Soleimani cha Ijumaa iliyopita, kufuatia agizo la rais wa Marekani Donald Trump.
"Tunawaonya washirika wote wa Marekani,ambao wameruhusu vikosi vya Marekani kuwa katika ardhi yao, kwamba wakijaribu uchokozi wa aina yoyote dhidi ya Iran yatalengwa," ilisema kupitia taarifa yake iliyotolewa shirika la habari la Iran, IRNA.
Mashambulio hiyo yalifanyika saa kadha baada ya mazishi ya Soleimani.

Awali, rais Trump alisema kuwa hatua ya kuondoa vikosi vyake Iraq itakuwa na athari mbaya sana kwa nchi hiyo.
Marekani ina karibu wanajeshi 5,000 nchini Iraq.
Uingereza imechukua hatua ya tahadhari kwa kuweka tayari manuari yake ya kivita na helikopta za kijeshi baada ya kuongezeka kwa hali ya taharuki mashariki ya kati, alisema waziri wa ulinzi Ben Wallace.
Mambo yalifikaje hapa?
Kuuawa kwa Soleimani Januari 3 kulizorotesha uhusiano kati ya Iran na Marekani.
Jenerali Soleimani - alikuwa kiongozi wa oparesheni ya kijeshi ya Iran katika eneo la mashariki ya kati - lakini serikali ya Marekani ilimuona kuwa gaidi, ambaye alihusika na vifo vya mamia ya wanajeshi wake na kwamba alikuwa akipanga shambulio "hatari".
Iran iliapa "kulipiza kisasi" kifo chake.
Bwana Trump, kwa upande wake, alionya kuwa Marekani itajibu jaribio lolote la kulipiza kisasi "pengine kwa njia kali zaidi".
"Alikuwa adui lakini sasa sio adui tena. Amekufa," Bwana Trump alisema, akitetea uamuzi wake.
"Alikuwa anapanga shambulio kubwa, shambulio hatari dhidi yetu. Sidhani mtu yeyote anaweza kulalamika kuhusiana na hilo."
Mamilioni ya raia wa Iran walijitokeza kwa mazishi ya kamanda huyo wa kijeshi, wakibeba mabango na kusema kwa sauti "kifo kwa America" na "kifo kwa Trump".

Chanzo cha picha, EPA
Iraq inaingilia wapi suala hili?
Iran inaunga mkono makundi kadhaa ya wanamgambo wa kishia katika nchi jirani ya Iraq.
Siku ya Ijumaa, Soleimani alikuwa amewasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Baghdad na alikuwa katika msafara akiandamana na maafisa kadhaa wa makundi hayo, magari yao yaliposhambuliwa kwa makombora ya Marekani.
Iraq sasa imejipata katika njia panda kwasababu Iran na Marekani ni washirika wake.
Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wamekuwa nchini humo kusaidia katika mapambano dhidi ya wapiganaji wa kundi la Islamic State (IS) lakini serkali ya Iraq inasema hatua ya Marekani ilienda kinyume na makubaliano yao.















