Maporomoko ya udongo Pokot Magharibi: Maafisa wa usalama wawasili kutoa msaada

Juhudi za kuipata na kuivuta miili kutoka kwenye matope zimekwmaishwa na usafiri baada ya barabara zinazokwenda katika maeneo hayo kuharibika.
Maelezo ya picha, Juhudi za kuipata na kuivuta miili kutoka kwenye matope zimekwmaishwa na usafiri baada ya barabara zinazokwenda katika maeneo hayo kuharibika.

Maafisa wa usalama wamewasili katika jimbo la Pokot Magharibi nchini Kenya kwa ajili ya kutoa msaada kwa waathiriwa wa maporomoko ya udongo. Mmoja wa waathiriwa ameiambia BBC leo asubuhi.

Idadi ya watu waliofariki katika mkasa wa maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa inayonyesha katika eneo la Pokot Magharibi nchini Kenya imefikia watu 56, kulingana na afisa wa serikali katika eneo hilo.

'' Polisi na wanajeshi wamefika hapa kwa helikopta kubwa mbili'', alisema muathiriwa Thomas Ngura ambaye jirani yake alipoteza watu watano kwenye mkasa huo uliotokea mwishoni mwa Juma.

Anasema msaada ulipatikana hata hivyo haujatosha, akiwa na matumaini kuwa serikali itaendelea kuwasaidia kukabiliana na athari za maporomoko ya ardhi.

Unaweza pia kusoma:

Bwana Ngura amesema kuwa waathiriwa wote na watu ambao hawana makazi kutokana na mkasa wa maporomoko ya ardhi wameshauriwa kuhamia maeneo salama kama vile shule ili kuyanusuru maisha yao, kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.

'' Tumeshauriwa tuende eneo salama la Paroa...watu wanapofika katika maeneo salama kama haya wanapewa chakula, nguo na blanketi' , Bwana Ngura ameiambia BBC

Hata hivyo anasema hali ya wasi wasi bado imetanda miongoni kwa wakazi wa West Pokot kutokana na dalili za kunyesha kwa mvua zaidi inayoweza kusababisha maafa zaidi.

Viji vilivyosombwa na maji ya mafuriko

Chanzo cha picha, Mark Meut

Maelezo ya picha, Nyumba 22,000 zimeharibiwa na maporomoko ya ardhi na kati ya watu 80,000 na 120,000 wamesambaratika au kuathiriwa na mafuriko hayo

''Katika eneo la kijiji chetu hatujawapata watu 6 waliozikwa ndani ya udongo ..hatujui wako wapi, labda serikali itatusaidia kuwapata. Polisi wamekuja wamewasaidia watu kutafuta miili Sigor '' , aliongeza.

Idadi ya miili ambayo haijapatikana ni 22, baada ya mkasa huo kuyakumba maeneo ya Parua, Nyarkulian and Muino, kwa mujibu wa Gavana wa jimbo hilo, Profesa John Lonyangapuo.

Profesa Lonyangapuo aliiambia BBC Jumatatu kuwa shughuli ya kusaka na kuokoa miili bado inaendelea.

Juhudi za kuipata na kuivuta miili kutoka kwenye matope zimekwamishwa na miundombinu mibaya baada ya barabara zinazokwenda katika maeneo hayo kuharibika.

Amesema kuwa nyumba 22,000 zimeharibiwa na maporomoko ya ardhi na kati ya watu 80,000 na 120,000 wamesambaratika au kuathiriwa na mafuriko hayo.

Awali maafisa walisema kuwa barabara zinazounganisha vijiji zimeharibika kutokana na mafuriko katika barabara na daraja moja lilisombwa na maji.

Bwana Lonyangapuo alitoa wito kwa waziri wa mambo ya ndani nchini humo Fred Matiang'i akimuomba usaidizi wa helikopta kwa ajili ya uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa na maporomoko ya ardhi.