Saratani: Joan Wangari apona saratani ya kongosho baada ya miaka minane

Kulingana na Shirika la afya duniani (WHO) ugonjwa wa Saratani umenawaua watu milioni 9.6 kote duniani kila mwaka.
Joan Wangari mwenye umri wa miaka 36 aligunduliwa na saratani ya Kongosho mwaka 2011 na ameweza kukabiliana na yote na hivi sasa ameambiwa amepona lakini sasa anafanyiwa uchunguzi iwapo anaweza kupatwa na magonjwa mengine.
Saratani ya Kongosho ni nadra na hungunduliwa baada ya muda mrefu lakini kwa Joan alianza kupata dalili tofauti katika mwili wake ambazo hakufahamu zilikuwa dalili za satarani lakini alidhani ni dalili za uzio akiwa na umri wa miaka 27.
''Nilikuwa nikiwashwa mwili, nikapoteza uzito, macho yangu yakabadilika yakawa rangi ya manjano na pia rangi ya kinyesi changu kilibadilika'' Joan amesema.

Joan amesema alianza kujitibu mwenyewe kwa kununua dawa katika duka la dawa kwani amekuwa akipatwa na uzio wa muashwo iwapo alitumia sabuni au mafuta ambayo ngozi yake haijazoea.
'Nilikuwa siwezi kulala usiku, nilikuwa nasikia kila mahali katika mwili wangu una muasho hasa kwa mikono na miguu nilikuwa nachukua hata jiwe najikuna napita kwa ukuta ilimradi tu nijikune.''
Baada ya muda alirudi hospitalini na kufanyiwa uchunguzi wa damu lakini hakuna ugonjwa wowote uliopatikana wakati ule. Madaktari wakaanza kusema mambo tofauti na nikaanza kutibiwa ugonjwa wa ini (hepatitis C)licha ya matibabu hayo muasho uliendelea.
''Nilitamani ingekuwa uchungu kwani ningemeza dawa za kupunguza maumivu.''amesema Joan
Muasho huwa ulimfanya atafute matibabu zaidi kwani hakumbuki kuwa mgonjwa au kulazwa hospitali isipokuwa wakati alipokuwa akijifungua kifungua mimba wake kando na homa ya muda mfupi.
Kulingana na Joan hakufahamu chochote kuhusu ugonjwa wa satarani kwani hakuwa na jamaa ambaye alikuwa ameugua ugonjwa huo.
''Mimi sikuambiwa nina saratani. Nilikuja kugunduaa mwenyewe kupitia utafiti. Rafiki yangu mmoja ambaye ni daktari aliniambia upasuaji wa tumbo niliokuwa nimefanyiwa wa kutolewa uvimbe ili muasho uishe ulikuwa wa kuchunguza ugonjwa wa saratani.'' Joan ameongeza.

Baada ya kufanyiwa uchunguzi madaktari waliandika katika kitabu chake kwamba ana saratani ya kongosho lakini hawakumwambia. kitu walichomwambia ni kuwa ana seli katika tumbo lake.
''Nilijua sasa niko na saratani wakati nilipoanza matibabu ya saratani ya chemotherapy.Nilihisi vibaya kwani madaktari hawakuniambia waziwazi.Nilipatwa na mshtuko.''
''Matibabu ya chemotherapy yalikuwa makali kwangu kwani nilipoteza nywele, mwili ulibadilika kucha zikabadilika rangi na kuwa nyeusi na hapo ndipo nilijua kwa kweli nina saratani.Nikadhani mambo yangu yameisha'' amesema Joan.

Baada ya kupokea matibabu ya saratani ya kongosho kwa miaka minne aliweza kubeba uja uzito mwaka 2015 jambo ambalo amelitaja kama la muijiza na uja uzito huo haukumsumbua hata kidogo licha ya kuwa na hofu kutokana na matibabu aliyokuwa akiyapitia hapo awali.
Safari hii ya saratani ilikuwa ngumu kwani watu walibaguliwa na hata kumwambia mume wake aache kumuuguza kwani ataaga dunia na hata ilituwabidi kuhama nyumba waliokuwa wakiishi na kuhaimia katika nyumba ya mabanda kutokana na gharama kubwa ya matibabu.
Lakini kwa hivi sasa Joan hapokei matibabu yoyote ya saratani.
Kulingana na Daktari bingwa wa ugonjwa wa saratani Primus Ochieng, amesema Saratani ya Kongosha huwa ni ngumu kuigundua na watu wengi hutafuta matibabu ikiwa tayari saratani hiyo imesambaa sana kwa mwili.
Watu wengi hutibiwa kwanza kama wana matatizo ya asidi katika tumbo lao na sio saratani ndio maana watu wengi hupatwa na saratani hii ikiwa katika hatua ya nne.

Kulingana na Daktari Ochieng watu wengi katika miaka ya hivi karibuni wanaugua magonjwa ya saratani kuliko miaka 10 iliyopita.
Mtaalamu huyo anasema ni kutokana na mfumo wa maisha kubadilika mfano ; Unywaji wa pombe kupita kiasi , uvutaji wa sigara, kutofanya mazoezi ya mwili na vyakula vilivyo na kemikali
Dkt. Ochieng amesema saratani inaweza kujirudia kutokana na seli kwa jina clonogenic ambazo wakati mwengine hufa wakati mtu anapokea matibabu na ikawa kama mawe na miaka mingi baadaye seli hizo huamka tena na kusababisha saratani kuwa na nguviu zaidi kushinda hapo awali.
Dkt. Ochieng amesihi kwamba ni bora mtu kuchunguzwa kwa kina iwapo ana maumivu yoyote na sio kununu a dawa katika maduka ya dawa na kujitibu.
Kongosho ni sehemu gani ya mwili?
Ni sehemu ya mwili iliyoko katika utumbo na kazi yake kuu ni kuzalisha homoni ya Insulin, Glucagon na Gastric.Gongosho hudhibiti kiwango cha sukari mwilini kama vile glucose.Kogosho huwa katika sehemu tatu; kichwa , mwili na mkia.
Dalili za saratani ya kongosho
- Kubadilika kwa ngozi na macho kuwa na rangi ya manjano.
- Maumivu ya mgongo
- Kuwashwa kwenye mikono na miguu
- Kupunguza uzani
- Kinyeshi kisichokolea rangi , chenye mafuta na harufu sana












