Usafiri wa treni Uswidi: Mwanamke mja mzito aburuzwa ndani ya treni kwa kukosa nauli

Mwanamke mja mzito akiburuzwa ndani ya treni na maafisa wa usalama

Chanzo cha picha, action4humanity

Maelezo ya picha, Mwanamke mja mzito akiburuzwa ndani ya treni na maafisa wa usalama

Video inayomuonesha mwanamke mja mzito akiburuzwa ndani ya treni na maafisa wa usalama mjini Stockholm imevutia hisia kali nchini Uswidi.

Mwanamke huyo aliyekuwa ameandamana na bintiyake mdogo hakuwa na tiketi, maafisa walisema.

Baada ya majibizano mafupi na maafisa wa usalama aliburuzwa kutoka ndani ya treni na kuondolewa kwenye kiti.

Maafisa wawili waliyohusika na kisa hicho wamesimamishwa kazi ili uchunguzi ufanywe.

Hata hivyo mwanamke huyo baadae alikimbizwa hospitali kwa matibabu ya dharura.

picha ya maktaba ya treni mjini Stockholm

Chanzo cha picha, Getty Images

"Kuna video nyingi zilizonaswa kwa simu zinazowaonesha walinzi wa treni wakiwadhalilisha abiria kwa kutumia nguvu kupita kiasi," Mhudumu wa usafiri wa umma Henrik Palmer, aliambia vyombo vya habari vya Uswidi.

Video hiyo iliyosambazwa sana katika mitandao ya kijamii imevutia malalamiko makali kuhusiana na jinsi wanawake weusi wanavyolengwa katika jamii ya waswidi.

Binti ya mama huyo aliyejawa na uoga alikuwa akilia huku akimtizama mama yake akilemewa na maafisa wa usalama.

Mwana blogu Lovette Jallow aliangazia kisa hicho katika mtandao wa kijamii wa Instagram

Chanzo cha picha, Lovette Jallow/Instagram

Maelezo ya picha, Mwana blogu Lovette Jallow aliangazia kisa hicho katika mtandao wa kijamii wa Instagram
Presentational white space

'Dhulma dhidi ya watu weusi'

Mwanablogu mashuhuri nchini UswidiLovette Jallow alisema ni jambo la kuikitisha kuona raia wa Uswidi wenye asili ya Afrika ''wakibaguliwa na kudhalilishwa''.

"Natumai mtoto huyo hajadhuriwa na tukio hilo," aliandika katika mtandao wake wa Instagram.

Anasema aliwasiliana na familia ya mwanamke huyo mwenye mimba ya miezi minane na kwamba imemfahamisha kuwa amepata matibabu hospitalini na kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Katika taarifa yake kampuni ya usafiri wa umma nchini Uswidi imeiambia BBC kuwa kisa hicho kwa sasa kinachunguzwa lakini maafisa wa usalama wana haki ya kumzulia mtu yeyote ''anayezua vurugu".

"Kile kinachofahamu ni kuwa mwanamke mmoja alipatikana bila tiketi halisi akapigwa faini kwa mujibu wa kanuni zetu,alipokataa amri hiyo akaambiwa ashuke hatua ambayo ilisababisha vurumai hilo," alisema msemaji wa kampuni ya usafiri ya SL.

Picha ya maktaba ya treni mjini Stockholm

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Walizi wawili wamesimamishwa kazi kwa kuburuza chini mwanamke mja mzito ndani

Shirika la kutetea haki za wanawake limesema maafisa wa usalama wamekuwa wakitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya watu weusi katika siku za hivu karibuni.

Rais wa shirika hilo amesema "Linapokuja suala la watu weusi na weupe - kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha maafisa wa usalama wakati mwingine wanawabagua watu weusi bila sababu yoyote ya msing," anasema rais wa shirika hilo, Alan Ali.

Aliongeza kuwa kuwasimamisha kazi maafisa hao ni hatua ya kwanza, lakini mamlaka ya usafiri wa umma na mashirika ya kutoa ulinzi wanastahili kupewa mafunzo kuhusiana na ubaguzi wa rangi na masuala ya afya ya uzazi.