Miaka 2 baada ya kufariki Etienne Tshisekedi, Je sasa atazikwa DR Congo?

Ni miaka miwili sasa tangu kiongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Etienne Tshisekedi afariki dunia mjini Ubelgiji, lakini mpaka sasa mwili wa marehemu babake rais mpya wa DRC, Felix Tshisekedi hauja rejeshwa nchini.
Familia yake na chama chake, zilituhumu kwamba rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila amezuia juhudi za kurejeshwa kwa kiongozi huyo wa kisiasa nchini.
Leo imetimia miaka miwili, mwili wa marehemu Etienne Tshisekedi wa Mulumba umesalia ndani ya chumba cha kuhifadhi maiti huko Ubelgiji.
Licha ya juhudi za familia yake na chama chake kutaka mwili wake urudishwe nchini Congo, serikali, chama na familia yake zilikosa kueleweana kuhusu pahala pa kumzika marehemu.
Chama chake UPDS kilitaka azikwe katika makao ya chama, lakini serikali ilikataa na badala yake awali iliagiza azikwe katika makaburi yaliopo kwenye mtaa wa Gombe, na baadae walikubaliana azikwe katika kiwanja cha familia yake kilichokuwa mbali na mji wa Kinshasa, lakini mipango yote yalisitishwa.

Gerard Mulumba ni ndugu yake marehemu ambae alipewa jukumu ya kuandaa mazishi ya kiongozi huyo
'Waliogopa kwamba kufika kwa mwili wake katika mji huu wa Kinshasa ambapo alikuwa anapendwa sana, kungevuruga utaratibu, walikataa azikwe pahali tulikuwa tunataka'.
'Hata tulipoamua kumzika nje kidogo ya Kinshasa waliendelea tu kuchelewesha mambo, bila sababu yoyote'.
Familia yake sasa inatumai ya kwamb, kupitiaa mtoto wake marehemu, Felix Tshisekedi ambae sasa ni rais wa DRC , mazishi ya kiongozi huyo mkongwe wa siasa DR Congo yataandaliwa kwa heshima mwezi huu.
'Kuchaguliwa kwa rais wa sasa, tunatumai kuandaa mazishi yanayofaa , familia imeshakutana na hivi kazi inaendelea, nadhani kabla ya mwisho wa Februari mwili wake utazikwa' ameeleza Mulumba.

Kwa mujibu wa familia ya marehemu , hadi sasa mjane, mkewe marehemu Tshisekedi hajatoka nje kwa muda wa miaka miwili sasa, hata siku alipoapishwa mwanawe Felix Tshisekedi, hakuweza kufika kulingana na mila ya familia hiyo ambayoo hairuhusu mjane kusafiri au kufanya shuguli zozote wakati mwili wa mpenzi wake hauja zikwa.

Etienne Tshisekedi ni nani?
Akiwa mzaliwa wa jimbo la kati la Kasai mnamo mwezi Disemba mwaka 1932, bw Tshisekedi alikuwa kiongozi wa upinzani mwenye umri mkubwa.
- Alisomea sheria chini ya ukoloni nchini Ubelgiji.
- Harakati zake za kisiasa zilianza wakati wa uhuru wa taifa hilo mwaka 1960 ambapo alikabidhiwa nyadhfa za juu katika serikali ya kati mbali na utawala wa Kasaian uliokuwa mfupi.
- Mnamo terehe 14 mwezi Novemba 2011, akiwa waziri wakati wa serikali ya dikteta Mobutu Sese Seko, bw Tshisekedi alijimwaga katika siasa za upinzani 1980 wakati Mobutu alipoamua kufutilia mbali uchaguzi wote.
- Akiwa kiongozi wa chama cha muungano wa Demokrasia pamoja na chama cha Social Progrees, amekuwa mpinzani wa serikali zote tangu wakati huo.
- Wakati Mobutu alipolazimishwa kutengeza serikali ya muungano na upinzani, bw Tshisekedi alikuwa waziri mkuu mara mbili katika kipindi cha miaka miwili.
- Alijiuzulu nyakati zote hizo alipokosana na Mobutu.
Etienne Tshisekedi ana umaarufu mkubwa katika jimbo la Kasai mjini Kinshasa.
Kadhalika, chama chake UDPS kina umaarufu mkubwa kusini mwa taifa hilo lakini sio maeneo yote ya nchi.












