Felix Tshisekedi: Mgombea wa upinzani ashinda uchaguzi wa urais DRC

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Felix Tshisekedi ameshinda uchaguzi wa urais nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, tume ya uchaguzi imesema.
Matokeo ya awali yanaonyesha mgombea huyo wa upinzani amemshinda mgombea mwingine wa upinzani Martin Fayulu, pamoja na mgombea aliyekuwa anaungwa mkono na serikali Emmanuel Shadary.
Mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Ceni) Corneille Nangaa, alisema mapema Alhamisi kwamba Bw Tshisekedi alipata asilimia 38.57 ya kura zilizopigwa na "anatangazwa mshindi wa urais mteule."
Tshisekedi alipata zaidi ya kura 7 milioni naye Bw Fayulu akapata kura takriban 6.4 milioni, huku mgombea wa serikali Emmanuel Ramazani Shadary akipata takriban kura 4.4 milioni.
Matokeo yaliyotangazwa na CENI:
- Felix Tshisekedi 7,051,013 (38.57%)
- Martin Fayulu Madidi 6,366,732 (34.83%)
- Emmanuel Shadary 4,357,359 (23.84%)
*Waliojitokeza kupiga kura kwa mujibu wa CENI ni 47.56%.
Bw Fayulu ameyapinga matokeo hayo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi.
Ameambia Idhaa ya Kifaransa ya BBC kuwa: "Hii ni kashfa mbaya sana. Matokeo haya hayana uhusiano hata kidogo na ukweli halisi. Raia wa Congo hawataukubali utapeli kama huu daima. Felix Tshisekedi hakupata kura 7 milioni, haiwezekani. Alizitoa wapi?"

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Bw Tshisekedi, kwa upande wake ameyafurahia matokeo hayo na kumsifu pia rais anayeondoka Joseph Kabila.
Akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mji mkuu Kinshasa, Tshisekedi amesema atakuwa "rais wa raia wote wa Congo".
"Namshukuru Rais Joseph Kabila ambaye leo hatufai tena kumchukulia kama adui, lakini kama mshirika katika mabadiliko ya kidemokrasia nchini mwetu," amesema.
Tamko la Ufaransa na Ubelgiji
Barnabe Kikaya Bin Karubi, ambaye ni mmoja wa washauri wakuu wa Rais Joseph Kabila amekubali matokeo hayo, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Amesema: "Bila shaka hatujafurahia kwamba mgombea wetu alishindwa, lakini raia wa Congo wameamua na demokrasia imeshinda."
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters ameomba kuwepo na ufafanuzi kuhusu matokeo hayo akisema ushindi wa Bw Tshisekedi unaenda kinyume na uhalisia mashinani.
"Kanisa Katoliki la Congo lilifanya hesabu yake na kutoa matokeo tofauti kabisa," amenukuliwa na shirika hilo.
Nchi ya Ubelgiji ambayo iliitawala DRC wakati wa ukoloni imeungana na Ufaransa katika kutilia mashaka matokeo hayo.
Waziri wa Mambo ya Nje Didier Reynders amenukuliwa la shirika la habari la Reuters akiiambia redio ya taifa RTBF kuwa Ubelgiji itatumia nafasi yake ya muda katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutaka taarifa rasmi ya kilichotokea.
"Tuna mashaka na inabidi tuhakikishe na kujadiliana suala hili katika vikao vya Baraza la Usalama," Bw Reynders ameongeza.
Tamko la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa wadau wote kujiepusha na vurugu.
"...waelekeze mizozo yoyote kuhusu matokeo ya uchaguzi kwa mifumo na taasisi zilizopo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, msemaji wake Stephane Dujarric, amesema akiwa mjini New York.
Umoja wa Afrika (AU) wametaka mzozo wowote kuhusu matokeo ya uchaguzi huo yatatulie kwa njia ya amani.
Mkuu wa Kamisheni ya AU Moussa Faki Mahamat amesema: "Ni muhimu kwa mtanziko wowote wa matokeo, hususani kuwa hayajaakisi matakwa ya wananchi, inabidi utatuliwe kwa njia ya amani kwa kutumia sheria na makubaliano ya kisiasa kwa pande zinazohusika."
Iwapo matokeo hayo yatathibitishwa, Bw Tshisekedi atakuwa mgombea wa kwanza kabisa wa upinzani kushinda uchaguzi wa urais tangu DRC ilipojipatia uhuru.
Bw Tshisekedi yuko kwenye muungano wa kisiasa aliyekuwa mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe UNC ambapo walikuwa wamekubaliana kwamba Tshiskedi atagombea wadhifa wa rais naye Kamerhe awe waziri mkuu iwapo muungano wao utashinda urais.

Chanzo cha picha, EPA
Rais Joseph Kabila anatarajiwa kuondoka madarakani baada ya kuongoza kwa miaka 18.
Mgombea wake aliyemteua kuwakilisha muungano tawala Emmanuel Ramazani Shadary amemaliza wa tatu.
Martin Fayulu ambaye awali alikuwa mgombea wa pamoja wa muungano wa upinzani kabla ya Tshisekedi na mgombea wa chama cha UNC (Union for the Congolese Nation) Vital Kamerhe kujiondoa kutoka kwenye muungano huo na kuunda muungano wao wawili, alimaliza akiwa nafasi ya pili.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, CENI, matokeo kamili yanatarajiwa kutangazwa mnamo 15 Januari na rais mpya ataapishwa siku tatu baadaye. Matokeo hayo hata hivyo yanaweza kupingwa katika Mahakama ya Kikatiba.

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images
Bw Kabila alikuwa ameahidi kukabidhi madaraka kwa mshindi wa uchaguzi huo, jambo ambalo likitokea itakuwa mara ya kwanza tangu DRC kupata uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Matokeo hayo yalikuwa awali yametarajiwa kutangazwa Jumapili lakini yakaahirishwa.

Ushindi wa kihistoria
Mwandishi wa BBC Louise Dewast anasema ushindi huo uliotangazwa na CENI ni wa kihistoria kwa chama cha UDPS na Tshisekedi mwenyewe.
Chama hicho cha upinzani kimejaribu kwa miaka mingi kushinda uchaguzi DRC bila mafanikio. Lakini katika siku za karibuni kumekuwa na tetesi kuhusu uwezekano wa kufanyika kwa mwafaka kati ya Tshisekedi na rais Joseph Kabila hatua ambayo ilizua wasiwasi miongoni mwa wanasiasa wa upinzani.
Bw Tshisekedi mwenyewe amekiri kwamba alifanya mazungumzo na chama tawala lakini kuhusu maandalizi ya kipindi cha mpito.
Swali kuu kwa sasa ni jinsi wananchi na wadau wa kisiasa watayapokea matangazo hayo. Kanisa Katoliki ambalo lina waumini wengi na lilikuwa na waangalizi wa uchaguzi maeneo mengi lilikuwa limetahadharisha kwamba litayakataa matokeo iwapo hayatakuwa ya kweli. Kanisa hilo lilikuwa limesema linamfahamu mshindi wa urais na kwamba alikuwa ni mshindi wa wazi.

Felix Tshisekedi ni nani?
Felix Tshisekedi, ni mwanawe mwanzilishi wa chama cha Union for Democracy and Social Progress (UDPS), mwanasiasa wa upinzani wa muda mrefu Etienne Tshisekedi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Babake alifariki Februari mwaka jana na sasa mwanawe anatarajia kutumia msingi wa umaarufu wa babake kuchaguliwa kuwa rais.
Marafiki zake humuita kwa jina la utani "Fatshi" kutokana na hali kwamba yeye ni mnene kiasi.
Kwa muda ilionekana kana kwamba Tshishekedi, 55, jina lake halingekuwa kwenye karatasi za kura.
Novemba 11, yeye na Vital Kamerhe pamoja na wagombea wengine watano wa vyama vya upinzani walikutana na kumchagua Martin Fayulu apambane na Emmanuel Ramazani Shadary.
Lakini makubaliano yao yalidumu saa 24 pekee.
Tshisekedi na Kamerhe walidai kushinikizwa na vyama vyao kujiondoa na wakajitenga na Fayulu hatua iliyougawanya upinzani.
Wakishinda, Tshisekedi atakuwa rais naye Kamerhe, ambaye ni rais wa zamani wa Bunge na ambaye aliwania dhidi ya Kabila mwaka 2011 awe waziri mkuu.
Tangu babake Tshisekedi alipoanzisha chama cha UDPS mwaka 1982, kilihudumu kama chama kikuu cha upinzani, mwanzoni wakati wa utawala wa Mobutu Sese Seko kisha wakati wa utawala wa babake Kabila, Laurent-Desire Kabila, aliyeongoza 1997 hadi kifo chake 2001.
Kujiondoa kwa Tshisekedi kutoka kumuunga mkono Fayulu kulizua lalama, kwani kuliugawanya upinzani uliokuwa umeonesha dalili za kuungana.
Tshisekedi ni baba wa watoto watatu na yeye na Fayulu ni waumini katika kanisa moja la kipentekoste jijini Kinshasa.
Waliwania wanawania dhidi ya Shadary ambaye ni Mkatoliki.

Chanzo cha picha, AFP
Tshisekedi ana stashahada katika mauzo na mawasiliano kutoka Ubelgiji, lakini wakosoaji wake hutilia shaka hilo.
Wakosoaji wake pia wamekuwa wakisema hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa juu au kuwa na uzoefu wa usimamizi.
Lakini amepanda cheo chamani, kuanzia mwaka 2008 ambapo alikuwa katibu wa taifa aliyeangazia masuala ya uhusiano wa nje.
Machi mwaka jana aliteuliwa kiongozi wa chama baada ya kifo cha babake.
Alichaguliwa kuwa mbunge 2011, akiwakilisha eneo la Mbuji-Mayi katika mkoa wa Kasai-Oriental lakini alikataa kuhudumu kwa kuwa hakutambua kushindwa kwa babake na Rais Kabila katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2011.
Tshisekedi, ingawa hana uungwaji mkono mkubwa kama wa babake, aliambia AFP mwaka jana kwamba akishinda urais ataunda tume ya ukweli, haki na maridhiano na kumuwajibisha Bw Kabila. Lakini alisema atamruhusu kusalia nchini DR Congo.

Walioruhusiwa kuwania urais DR Congo
- Emmanuel Ramazani Shadary
- Kikuni Masudi Seth
- Mukona Kumbe Kumbe Pierre
- Ngoy Ilunga Isidore
- Makuta Joseph
- Kabamba Noel
- Mabaya
- Kinkiey Mulumba
- Freddy Matungulu
- Felix Tshisekedi
- Allain Shekomba
- Radjabu Sombolabo
- Kamerhe Vital
- Fayulu Martin
- Bomba
- Gabriel Mokia
- Basheke Sylvain
- Charles Gamena
- Mbemba Francis

Wagombea urais wakuu

Chanzo cha picha, AFP/Reuters
Kulikuwa na wagombea 21 lakini watatu ndio wakuu:
- Emmanuel Ramazani Shadary, Waziri wa zamani wa mambo ya ndani na mtiifu kwa Kabila, ambaye aliwekewa vikwazo na Muungano wa Ulaya kwa hatua zilizochuliwa upinzani wakati wa maandamano ya mwaka 2017.
- Martin Fayulu, Mkurugenzi mkuu wa zamani wa mafuta ambaye ameahidi nchi yenye mafanikio lakini ambaye watu maskini wanahisi hawezi kuwatetea.
- Felix Tshisekedi Tshilombo, Mtoto wa mwanasiasa mkongwe ambaye ameahidi kupambana na umaskini.
Waangalizi wa kanda walifuatilia uchaguzi huo lakini waangalizi wa kimataifa hawakualikwa.

Zaidi kuhusu DR Congo
Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya kati ina utajiri wa madini na ndiyo mzalishaji mkubwa wa madini ya cobalt, yanayotumiwa kwa simu na betri za magari.
Lakini ina viwango vya juu vya umaskini, miundo msingi duni na wanasiasa na wafanyabiashara wanalaumiwa kwa kujitajirisha huku wengine wengi wakibaki kuwa maskini.
Imekuwa kwenye hali ambayo waangalizi wengine wanataja kuwa vita vya dunia vya Afrika kati ya mwaka 1997 na 2003.

















