Viongozi wa kieneo wakutana katika mkutano wa EAC Arusha

Rais wa Rwanda, Paul Kagame amepokea uwenyekiti wa jumuiya ya Afrika mashariki katika mkutano uliofanyika hii leo mjini Arusha Tanzania.
Baada ya kukabidhiwa madaraka, rais Kagame alishukuru na kumrudishia mwenyekiti anayeondoka rais Uganda Yoweri Museveni aendeleze ajenda ya siku.
Viongozi hao wamekuwa katika mkutano wa faragha tangu mchana, huku kukiwa na hali ya wasiwasi na uhasama miongoni mwa nchi wanachama.
Waliowasili Arusha ni mwenyeji Rais John Magufuli wa Tanzania, Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Mwandishi wa BBC Munira Hussein ambaye anafuatilia mkutano huo jijini Arusha anaripoti kuwa Marais wa Burundi na Sudani Kusini wametuma wawakilishi wao kwenye mkutano huo.
Katika siku za hivi karibuni Burundi iliitangaza Rwanda kama adui yake. Na kwa upande mwingine Rwanda imekuwa ikilalamikia juu ya kile inachosema vitendo vya utesaji, utekwaji na kurudishwa nyumbani kiholela kwa raia wake wanaosafiri nchini Uganda.
Wanachama wengine wa jumuia hiyo ya EAC ni pamoja na wenyeji wa mkutano Tanzania, Kenya na Sudan ya Kusini.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Sio viongozi wote wa mataifa sita wanachama watahudhuria mkutano huo wa leo. Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza amewakilishwa na naibu wake wa kwanza, Gaston Sindimwo.
Rais wa Sudan kusini, Salva Kiir naye amewakilishwa na ujumbe maalum.
Mkutano huu ulipangwa kufanyika Novemba mwaka jana lakini ukaahirishwa mara mbiili baada ya Burundi kuugomea. Burundi inalalamika kwamba jumuia inafumbia macho uhusiano wake mbaya na Rwanda, ambayo kwa sasa ndio nchi adui yake mkubwa katika eneo hili.

Chanzo cha picha, AFP
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi anamlaumu mwenziye wa Rwanda Paul Kagame kwa kufadhili jaribio la kutaka kumpindua madarakani miaka mitatu iliyopita pamoja na kutoa mafunzo kwa vikundi vya waasi vinavyovuruga usalama wa nchi hiyo.
Rwanda nayo haiko sawa na jirani zake Uganda. Mamlaka mjini Kigali zimekuwa zikilalamikia matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu dhidi ya raia wake wanaoenda Uganda. Rwanda imekuwa ikikanusha madai ya Burundi, wakati Uganda haisemi lolote.
Ratiba ya mkutano wa leo inaonesha kuwa kutazungumziwa masuala kuhusu kuanzishwa kwa sarafu ya pamoja na masuala mengine ya kisiasa ndani ya jumuiya.
Suala lengine linalotarajiwa kujadiliwa ni juu ya vikwazo vya kibiashara miongoni mwa mataifa hayo. Tanzania na Kenya zimekuwa zikilaumiana juu ya kuwekeana vikwazo vya kibiashara.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Rais Kenyatta akiwa njiani kuelekea Arusha ameandika kupitia mtandao wake wa Twitter kuwa ajenda yake kuu kwenye mkutano huo ni kuboresha mahusiano ya kibiashara kwenye jumuiya hiyo.












