Ndege ya Air India yagonga ukuta katika uwanja wa ndege wa Trichy

Chanzo cha picha, Air India
Ndege ya abiria iliyokuwa ikisafiri kutoka mji wa Trichy kusini mwa India kuelekea Dubai ilivunjika sehemu ya bawa lake baada ya kugonga ukuta katika uwanja wa ndege kabla ya kupaa.
Ndege hiyo iliyokua na abiria 130 na wahudumu sita ilielekezwa mjini Mumbai ambako ilitua salama.
Shirika la ndege la India limesema marubani wawili wa ndege hiyo ambao wote wana tajiriba ya kupaa kwa zaidi ya saa 6,500 wamesimamishwa kazi hadi uchunguzi utakapokamilika.
Katika taarifa kutoka shirika hilo zinasema kuwa ndege hiyo ya Boeing 737 ilipaa kutoka uwanja wa ndege wa Trichy kusini mwa India mapema Ijumaa asubuhi wakati maafisa walipogundua huenda imegonga ukuta katika uwanja wa ndege.

Chanzo cha picha, Air India
Tukio hilo limewasilishwa kwa shirika la kudhibiti usafiri wa angani huku shirika la Air India likisema liko tayari kushirikiana kwa uchunguzi
Pia limetokea wiki kadhaa baada ya zaidi ya abiria 30 waliyokuwa wameabiri ndege nyingine ya India walilazimika kupewa matibabu baada ya rubani kusahau kubonyeza kifaa kinachodhibiti kiwango cha presha ndani ya ndege.
Mwaka 2015 ndege nyingine ya shirika la Air India iliyokuwa safarini kutoka Mumbai kwenda London ililazimika kukatiza safari na kurejea uwanja wa ndege baada ya panya kuonekana ndani ya ndege hiyo.
Ndege hiyo nambari AI 131 ilikuwa imefika Iran pale panya alipoonekana na mmoja wa watu waliokuwa ndani ya ndege hiyo, ripoti zinasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Abiria waliendelea na safari yao kwa kutumia ndege nyingine.
Air India ambayo ni moja ya shirika la ndege la muda mrefu halijapata faida tangu mwaka 2007.
Mwezi Juni mwaka 2017, baraza la mawaziri nchini India ilidhinisha mpango wa kubinafsisha shirika hilo lakini halikupata wanunuzi baada ya serikali kutoa ofa ya kuuza sehemu kidogo ya usimamizi wake.
Mnunuzi yeyote atalazimika kuchukua karibu dola bilioni 5 ya deni ambayo ni nusu ya deni lote linalodaiwa shirika hilo.













