Kurejea kwa wanasiasa wa upinzani ni mwanzo mpya wa siasa Tanzania?

Chanzo cha picha, IKULU/TANZANIA
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Katika safu yake ya kila wiki kwenye gazeti la lugha ya Kiingereza la The East African wiki hii, mwandishi wa habari mkongwe nchini Tanzania, Jenerali Ulimwengu, ameandika kuhusu hatari ya kuwasifia wanasiasa kwa sababu wanaweza kubadilika wakati wowote na uliyesifia ukajutia kauli yako.
Maneno hayo aliyaandika katika makala hiyo ambayo kimsingi alikuwa akisifu hatua za makusudi zilizochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha demokrasia na utawala bora tangu aingie madarakani Machi mwaka 2021.
Mojawapo ya hatua hizo ni kuruhusiwa kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara ambayo ilipigwa marufuku mwaka 2016 wakati wa utawala wa mtangulizi wa Samia, hayati Rais John Pombe Magufuli. Tayari Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amerejea tangu Januari 24 mwaka huu na tayari amefanya mkutano mmoja wa hadhara katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.
Mwanasiasa mwingine mashuhuri wa upinzani aliyekimbilia ughaibuni wakati wa utawala wa Magufuli alikuwa ni Godbless Lema – aliyepata kuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chadema ambaye naye tayari ametangaza nia yake ya kurejea nyumbani mwezi ujao.
Swali pekee ambalo wadadisi na wachunguzi wa siasa za Tanzania wanajiuliza kwa sasa ni kama mabadiliko haya ni ya kudumu au ni hatua ya serikali ya Samia kutaka kusafisha taswira ya Tanzania iliyobadilishwa sana wakati wa utawala wa Magufuli.

Siasa za Tanzania na maisha ya ughaibuni
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tundu Lissu na Lema si wanasiasa wa kwanza wa Tanzania kukimbilia ughaibuni kukwepa hali isiyoridhisha ya kisiasa na kiusalama kwao. Wakati wa utawala wa Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wanasiasa kadhaa walikimbia nchi kupinga siasa walizoziita za kidikteta na kuokoa maisha yao.
Wanasiasa mashuhuri zaidi walioondoka Tanzania walikuwa ni Oscar Kambona aliyekimbia kwenye miaka ya 1960 na Abdulrahman Babu aliyeondoka nchini mara baada ya kuachiwa kutoka kizuizini na utawala wa Nyerere. Katika mazungumzo niliyofanya na aliyekuwa mjane wa Babu, Bi Ashura takribani muongo mmoja uliopita, kuwekwa huko kizuizini kwa mumewe kulikuwa pia namna ya Nyerere asiuawe na utawala wa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), hayati Abeid Amani Karume.
Wawili hao, Kambona na Babu, walirejea nchini mara baada ya kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi na walitarajiwa kuongoza vyama vya upinzani kwenye Uchaguzi Mkuu wa kwanza kwa mfumo huo uliopangwa kufanyika mwaka 1995. Hata hivyo, hali haikuwa nzuri kwao kwa sababu walirejea wakati ambapo siasa za Tanzania na kizazi cha kisiasa kikiwa kimebadilika tayari.
Lissu hajakaa kwa muda mrefu ughaibuni – akienda mara ya kwanza Kenya na Ubelgiji baada ya shambulizi dhidi ya maisha yake lililofanyika Septemba mwaka 2017 jijini Dodoma na kurejea mwaka 2020 kushiriki uchaguzi mkuu akiwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema. Aliondoka mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo akieleza kuhofia maisha yake.
Lema aliondoka nchini baada ya uchaguzi huohuo wa mwaka 2020 kwa sababu kama hizo za Makamu Mwenyekiti wa chama chake.
Mambo machache ni muhimu kuyaweka katika muktadha wa makala haya. Kwamba hii si mara ya kwanza kwa wanasiasa wenye misimamo tofauti na serikali kukimbia na kurejea nchini, kwamba chama tawala cha Tanzania; Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kiko madarakani tangu enzi za akina Babu hadi wakati huu wa Lissu na ukweli kuwa mazingira ya siasa na aina ya watu waliopo sasa ni tofauti na ilivyokuwa takribani miaka 30 iliyopita wakati akina Kambona wakirejea.
Ni mabadiliko ya kweli au geresha?

Chanzo cha picha, IKULU/TANZANIA
Katika mazungumzo yake aliyofanya na waandishi wa habari na katika mkutano wa hadhara wa kwanza wa chama chake uliofanyika jijini Mwanza mwishoni mwa mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema katika vikao alivyofanya na Rais Samia, amejiridhisha kwamba ni kiongozi aliye na dhamira ya dhati ya kuleta maridhiano ya kisiasa.
“Mimi nimezungumza na Rais kupitia vikao vyetu. Nimeona dhamira yake kwamba ni njema. Nafahamu kwamba tunahitaji kuwa makini kwa sababu tunajua yeye ni CCM na chama hicho tunakijua kwamba hakiaminiki. Lakini hadi sasa ninamuamini na naona ana dhamira ya dhati,” alisema Mbowe.
Katika makala yake niliyoizungumzia awali kwenye gazeti la The East African, Jenerali aliandika; “Sifa pekee kubwa ambayo naweza kumpa Rais Samia ni kwamba anafanya mabadiliko makubwa kwenye siasa za Tanzania pasipo kupiga kelele nyingi na badala kuacha vitendo vizungumze”.
Rais Samia alianza kupata umaarufu kisiasa nchini Tanzania wakati akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014. Bunge hilo lilikuwa na mijadala mikali na ilikuwa ikifahamika kwamba kikao kikiwa chini yake alikuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza na kuvumilia hoja kutoka kwa walioonekana kuwa wapinzani wa chama chake cha CCM.
Katika maadhimisho ya miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, Samia alifanya kitu kisichozoeleka kwa kuandika makala katika magazeti mbalimbali ya Kiswahili nchini kwake kueleza dhamira yake ya kuona anajenga taifa lenye maridhiano, uvumilivu, ustahamilivu na ukuaji. Kwa sababu kuna msemo kuwa wino haufutiki, ni wazi Rais asingependa kuandika kitu ambacho anajua hatakifanya na kitamsuta baadaye.
Wakati wa maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa mwaka huu, watu mbalimbali wakiwamo wapinzani wa CCM kisiasa akiwamo aliyewahi kuwa mbunge wa Mbeya Mjini na msanii maarufu wa muziki, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Mr. Sugu, walimtumia salamu za pongezi – jambo ambalo usingelitegemea miaka michache iliyopita wakati wa utawala wa Mtangulizi wake.

Changamoto za mfumo wa demokrasia ya kiliberali
Mabadiliko yanayofanywa na serikali ya Rais Samia yanailekeza Tanzania katika njia ya mfumo wa demokrasia ya kiliberali ulioanza kupata nguvu sana tangu kuvunjika kwa Urusi ya kisovieti mnamo mwaka 1990. Hata hivyo, kulinganisha na katikati ya miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, mfumo huu unapitia changamoto lukuki.
Rais Samia anafanya mabadiliko kupitia chama cha CCM ambacho kilikuwa madarakani hata wakati wa Magufuli. Kwa maana hiyo, mabadiliko haya yanayoendelea sasa yanaweza kubadilika katika wakati huu akiendelea kuwa madarakani au akija mwanasiasa mwingine anayefikiri tofauti na mwanamke huyu wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania.
Katika andishi lake lililotoka mwaka jana la Parties, Democracies and the Ideal of Anti -Factionalism, David Ragazzoni aliandika kuhusu asili ya vyama vya siasa vya sasa ambapo changamoto kubwa ni kuwa na vyama “vinavyomsikiliza zaidi kiongozi wa chama, vinavyojali viongozi na vinavyotaka wananchi wawe wasikilizaji tu badala ya washiriki”. Hii ndiyo changamoto kubwa zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya siasa za Rais Samia.
Hatari ya Tanzania – au nchi nyingine yoyote ya Afrika, kutawaliwa na kiongozi asiyeamini katika mfumo wa demokrasia ya uliberali na badala yake udikteta unaoamini kwamba namna ya kuondoa umasikini ni kubinya haki za wananchi na washindani wako kisiasa, bado ni kubwa.
Lakini, kama alivyosema Jenerali Ulimwengu mwanzoni mwa makala haya, Tanzania inaweza kusema kwamba inapiga hatua sahihi kuelekea kwenye kufanya siasa za kistaarabu.












