Je, ni kweli Urusi imepokea mamia ya makombora kutoka Iran?

Chanzo cha picha, Getty Images
Februari 21, 2024 shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo sita, liliripoti kwamba Iran imepeleka makombora 400 nchini Urusi.
Vyanzo vitatu kutoka Iran vililiambia shirika hilo kuwa makombora ya Zolfaghar, yanayoweza kushambulia kwa umbali wa hadi kilomita 700, ni miongoni mwa makombora yaliyopelekwa Urusi.
Bado hakuna uthibitisho

Chanzo cha picha, Getty Images
Makabidhiano hayo, kulingana na shirika hilo, yalianza mwishoni mwa Januari na afisa mmoja wa Iran ambaye hakutaka kutajwa jina lake aliahidi kwamba yataendelea.
Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, John Kirby alisema Marekani bado haina ushahidi wa usafirishwaji wa makombora kutoka Iran kwenda Urusi. Aliahidi jibu la "haraka na kali" kutoka jumuiya ya kimataifa ikiwa Tehran imeipatia Moscow makombora.
Yuriy Ignat, msemaji wa Jeshi la Anga la Ukraine, aliuambia mtandao wa Ukrinform, ''kwa sasa hakuna taarifa kuhusu upelekwaji wa idadi hiyo ya makombora.''
Mwaka 2024, mkuu wa Kurugenzi ya Ujasusi ya Wizara ya Ulinzi, Ukraine, Kyrylo Budanov, alisema habari kuhusu ununuzi wa Urusi wa makombora ya Iran "hailingani na ukweli."
Wizara ya Ulinzi ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu walikataa kutoa maoni yao kwa Reuters kuhusu shehena hizo.
Ikiwa makombora ya Iran yatafika Urusi, yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa Ukraine. Lakini kuanzia 2022, Urusi ilianza kutumia ndege zisizo na rubani za Shahed za Iran dhidi ya Ukraine.
Mara kwa mara Ukraine imeitaka Iran kusitisha utoaji wa silaha kwa Urusi, na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine iliwasilisha pendekezo kwa Rais Zelensky la kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ushirikiano wa kijeshi kati ya Urusi na Iran umekua kwa kiasi kikubwa.
Mwaka jana, Iran ilithibitisha kununua ndege za kijeshi za Urusi aina ya Su-35 na Yak-130 na helikopta za Mi-28.
Hatari kwa Ukraine

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ikiwa Urusi itapokea makombora ya Iran, itaongeza changamoto kwa ulinzi wa anga wa Ukraine.
Fabian Hintz, mtafiti katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS), anachunguza silaha za makombora Mashariki ya Kati, anabainisha kuwa makombora ya Zolfagh kutoka familia ya Fateh ni rahisi sana kufanya kazi na kurusha.
"Makombora haya yanalenga kwa usahihi na yanaharibu, yakiwa na vichwa vyenye uzito wa zaidi ya kilo 500," Hintz anaelezea. Kombora la Fateh-110 linafika hadi kilomita 300, Fateh-313 - hadi kilomita 500 na Zolfaghar - 700.
Kombora la Fateh-110 linatumia muda mfupi kuliandaa kabla ya kulifyatua, na pia linaweza kutumika katika hali mbaya ya hewa.
Waziri wa zamani wa Ulinzi wa Iran, Ahmad Wahidi alisema lina uwezo wa kupiga shabaha za nchi kavu na baharini, kambi, maghala ya silaha na shabaha zingine kwa usahihi wa 100%.
Ripoti pia zinadai kombora hilo linaweza kubebwa vichwa vya kemikali, pia linaweza kubeba kichwa cha nyuklia.
Marekani inaamini wakati wa utengenezaji wa kombora hili, makampuni ya Iran yalipata msaada mkubwa wa kiteknolojia kutoka makampuni ya Kichina.
Kombora la Fateh-313 ni kombora la masafa mafupi linatumia mafuta. Lilizinduliwa hadharani kwa mara ya kwanza 2015. Kichwa chake kina uzito wa kilo 380.
Kombora la Zolfaghar (ni jina la upanga wa Mtume Muhammad). Inajulikana kuwa wanajeshi wa Iran wameshambulia mara kwa mara maeneo ya maadui kwa makombora haya, haswa wapiganaji wa ISIS huko Syria na Iraq.
"Makombora haya yanaweza kusababisha uharibifu mkubwa lakini yanaweza kunaswa na baadhi ya mifumo ya ulinzi wa anga, kama vile Patriot. Ukraine ina mifumo hiyo, lakini haina uwezo wa kutosha kufunika eneo lote la Ukraine,'' anasema Hinz.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mchambuzi wa masuala ya kijeshi wa Ukraine, Oleksandr Kovalenko kupitia akaunti yake ya Telegram alitaja kombora la Zolfaghar kuwa tatizo kwa ulinzi wa anga wa Ukraine.
"Tatizo la Zolfaghar kwa mifumo yetu ya ulinzi wa anga ni kwamba kombora hili lina kichwa chenye uzito wa kilo 579 na kinaachana na kombora kinaposhambulia. Hii inafanya kuwa ngumu kukigundua, kukifuatilia na kukiharibu.''
Kwa mujibu wa Kovalenko, ulinzi wa anga wa Ukraine utahitaji muda wa kutengeneza mifumo ya kukabiliana na makombora ya Iran.
"Itakuwa bora zaidi kama washirika wetu wataharakisha kuipatia Ukraine mifumo ya ulinzi wa anga yenye uwezo wa kupambana kwa usahihi zaidi,'' anabainisha.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












