Iran yasema mashambulizi ya Marekani ni 'kosa kubwa la kimkakati'

Chanzo cha picha, EPA
Iran imetaja mashambulizi ya angani ya Marekani dhidi ya Iraq na Syria kuwa ni "kosa la kimkakati" baada ya maeneo 85 kushambuliwa katika kanda nzima siku ya Ijumaa.
Marekani imefanya mashambulizi ya kulipiza kisasi kujibu mashambulizi ya wiki iliyopita ya ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya kijeshi ya Marekani na kuwaua wanajeshi watatu wa Marekani.
Ikulu ya White House ililaumu shambulio la ndege zisizo na rubani dhidi ya kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran.
Marekani na Uingereza pia zilianzisha awamu mpya ya mashambulizi ya pamoja dhidi ya wapiganaji wa Houthi nchini Yemen siku ya Jumamosi.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema mashambulizi dhidi ya Iraq na Syria "hayatakuwa na matokeo yoyote zaidi ya kuzidisha hali ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu katika eneo hilo".
Hapo awali, Iraq ilisema mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Marekani yangesababisha "matokeo mabaya" kwa eneo hilo.
Takriban watu 16, wakiwemo raia, waliuawa kutokana na mashambulizi hayo, maafisa wa Iraq walisema.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Msemaji wa Waziri Mkuu wa Iraq alisema mashambulizi hayo ni "ukiukaji" wa mamlaka ya nchi yake na kwamba yataathiri "usalama na utulivu wa Iraq na eneo hilo".
Syria nayo imesema "ukaaji" wa Marekani katika ardhi ya Syria "hauwezi kuendelea".
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Marekani, Marekani ilishambulia Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) Kikosi cha Quds na wanamgambo washirika huko Iraq na Syria.
Ndege kadhaa za Marekani zilihusika, ikiwa ni pamoja na walipuaji wa masafa marefu walioruka kutoka Marekani.
Maeneo saba yalipigwa - manne nchini Syria na matatu nchini Iraq - huku shabaha zaidi ya 85 zikipigwa, jeshi la Marekani lilisema.
Hakujakuwa na mashambulizi katika ardhi ya Iran.
Tangu mashambulizi ya Ijumaa ya Marekani nchini Iraq na Syria, kumekuwa na shambulio moja dhidi ya wanajeshi wa Marekani, afisa wa ulinzi wa Marekani aliambia mshirika wa BBC wa Marekani CBS News.
Mashambulizi hayo yalilenga wanajeshi wa Marekani walioko katika eneo la Euphrates nchini Syria kwa kutumia roketi, lakini hakuna majeruhi walioripotiwa.
Rais Joe Biden alisema mashambulizi ya Marekani "yataendelea wakati na mahali tunapochagua" lakini akaongeza kuwa nchi yake "haitafuti mzozo katika Mashariki ya Kati au popote pengine duniani".
Mashambulizi hayo yametokea baada ya wanajeshi watatu wa Marekani kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye kambi ya Marekani karibu na mpaka wa Jordan na Syria.
Maafisa wa Marekani walisema kundi la Islamic Resistance in Iraq, kundi la wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Ndege hiyo isiyo na rubani ilitengenezwa na Iran, walisema, na ni sawa na ile iliopewa Urusi.
Shirika la wanamgambo - kundi mwavuli la wanamgambo wengi - linaaminika kuwa na silaha, na mafunzo kutoka kwa IRGC.
Iran imekanusha kuhusika na shambulio hilo dhidi ya kambi ya Marekani, ikisema "haikuhusika katika maamuzi ya makundi ya upinzani".
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iraq, Syria na Yemen "yanalenga tu utawala wa Kizayuni", akimaanisha mshirika wa Marekani Israel.
Urusi imetoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa "dharura" katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa "kuhusu tishio la amani na usalama lililosababishwa na mashambulizi ya Marekani dhidi ya Syria na Iraq," mwanadiplomasia wa Moscow katika Umoja wa Mataifa, Dmitry Polyansky, alisema kwenye mtandao wa kijamii.
Urusi - mwanachama wa kudumu wa baraza - imekuwa mshirika wa karibu wa Iran.

Mashambulizi ya Marekani yalitokea saa kadhaa baada ya Bw Biden kuhudhuria sherehe ya kuwarejesha nyumbani William Rivers, 46, Kennedy Sanders, 24, na Breonna Moffett, 23, waliofariki katika shambulizi hilo wikendi iliyopita.
Zaidi ya wahudumu wengine 40 walijeruhiwa katika shambulizi hilo la ndege isiyo na rubani, iliyoikumba kambi ya US Tower 22.
Wanachama wa Republican nchini Marekani walikosoa muda wa mashambulizi ya kulipiza kisasi, wakisema kuwa Marekani ilikuwa imesubiri kwa muda mrefu sana kujibu.
Maafisa wa Marekani walisema kusimamishwa kwa hali yoyote ni kwa sababu ya hali ya hewa ya mawingu kuzuia maeneo yanayolengwa.
Baadhi ya wataalam wa sera za kigeni wanaamini kuwa kuchelewa kuliruhusu Iran kuwaondoa maafisa wake, na hivyo kuepusha mzozo mkubwa kati ya Marekani na Iran.

Chanzo cha picha, Getty Images
Imetafsiriwa na Abdalla Seif Dzungu








