Jinsi mwanadiplomasia wa Tanzania alivyotaka kutatua mzozo wa mateka wa Marekani nchini Iran

Na Ahmed Salim

f

Chanzo cha picha, SAS ARCHIVES

Mzozo wa utekwaji nyara wa rai awa Marekani nchini Iran, ulioanza tarehe 4 Novemba 1979, ulikuwa nimoja ya matukio makubwa namuhimu sana yaliyotokea wakati wa uongozi wa rais Jimmy Carter, nchini Marekani.

Mgogoro huo uliodumu siku 444 ulihusisha mateka 52 raia wa Marekani na mamia ya wanafunzi wa chuo kikuu cha Iran, ambao waliuteka ubalozi wa nchi hiyo mjini Tehran.

Tukio hilo lilibadilisha kabisa mwelekeo na uhusiano kati ya Marekani na Iran wakati tayari kukiwa na mazingira ya wasiwasi ya wakati wa Vita Baridi.

Kwa sababu kadhaa, mzozo huo pia ulichangia kwa hakika kwa rais Carter kusalia madarakani kwa muhula mmoja, na kushindwa uchaguzi dhidi ya Ronald Reagan.

Suala hilo la uchaguzi pamoja na mipango ya Marekani ya majaribio ya kuwaokoa mateka, yanajulikana na umma.

Kile ambacho hakijulikani ni kuwa mwanzoni mwa mgogoro huu, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa – ambaye alikuwa mwanadiplomasia wa Tanzania aliyekuwa na umri wa miaka 37, alifikiriwa kuwa msuluhishi ambaye angeweza kusaidia kuachiliwa mateka hao na kufanya mapatano na Ayatollah Khomeini mjini Tehran.

Mwanadiplomasia huyo alikuwa Salim Ahmed Salim, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.

Ingawa safari ya Tehran haikuwahi kutokea, hasa kutokana na siasa na kuzuiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo Kurt Waldheim - ambaye alikuwa anataka kuchaguliwa tena mwaka 1981.

g

Chanzo cha picha, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje Tanzania

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Imani aliyopewa na kujiamini kwake Salim kuwa ana uwezo wa kushiriki na kuipatanisha Iran na Marekani, vilitoa nafasi ambayo haijawahi kushuhudiwa, kuhusu jinsi wanadiplomasia wa Kiafrika wanavyoweza kuwa na ushawishi katika korido za Umoja wa Mataifa.

Pia inaonyesha jinsi Tanzania, na wanadiplomasia wake walivyoheshimika katika kipindi ambacho mataifa yenye nguvu duniani yalivyokuwa yanaifinyanga dunia na mataifa mengine, hasa ya Afrika, yalivyokuwa watazamaji tu.

Matokeo ya mustakabali wa Balozi Salim kugombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwaka 1981 na juhudi za kuchaguliwa tena za Rais Carter – yalikuwa matukio mawili yaliyoathiriwa kwa kushindwa kupatikana kwa utatuzi wa haraka wa mzozo wa mateka jijini Tehran.

Kwa mujibu wa maelezo binafsi ya Dkt. Salim na Balozi wa Marekani wa wakati huo, iwapo Carter angeshinda tena uchaguzi, yeye (Dkt. Salim) angekuwa na nafasi kubwa kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa UN. Ikiwa Reagan angeshinda, "mambo yangebadilika kabisa."

Balozi wa Marekani alikuwa sahihi.

Rais Carter alishindwa katika uchaguzi mkuu 1980 na Ronald Reagan. Dkt. Salim naye alishindwa kupata kura za kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati wa uchaguzi wa 1981.

g

Chanzo cha picha, SAS ARCHIVES

Maelezo ya picha, DKt Salim Ahmed Salim katika moja ya matukio mwaka 1993 akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Afrika

Marekani ilipiga kura ya turufu dhidi ya Dk. Salim kila mara katika duru 16 za upigaji kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mjadala hasa, sio kile ambacho kingeweza kutokea. Habari kuu hasa; ni kuwa bila maelezo ya kina na uwekaji kumbukumbu wa Dkt. Salim, tusingeweza kamwe kujua kuhusu uwezekano wa kwenda Tehran na jukumu la diplomasia ya Tanzania katika kupunguza mvutano na kutafuta suluhu ya moja ya migogoro mikubwa iliotokea 1979.

Kutokuwepo kwa kumbukumbu hizi ingekuwa ni hasara kwa wale wanaothamini historia na wana shauku ya kuelewa jinsi wanadiplomasia wa Tanzania walivyokuwa na ushawishi katika nyanja za kimataifa.

Kwa kila kipande kisichoelezwa cha historia, tunapoteza sehemu yetu wenyewe.

Na hiyo ni moja ya sababu kuu ya kuanzishwa Tovuti ya Kumbukumbu ya Salim Ahmed Salim. Tulitaka kuhakikisha matukio yaliyorekodiwa yanapatikana kwa urahisi kwa lengo la kuhifadhi sehemu ya historia yetu.

g

Chanzo cha picha, SAS ARCHIVES

Maelezo ya picha, Matumaini yetu ni kwamba Tovuti ya Kumbukumbu ya Salim Ahmed Salim itawahimiza viongozi na serikali za Afrika kueleza zaidi habari ya yale yaliyojiri huko nyuma, ili kuonyesha jukumu la Afrika katika kuunda siasa za kimataifa

Ulianza kama mpango unaoendeshwa na familia, tovuti ya kumbukumbu hizi ni mradi wa kitaifa na wa Kiafrika na fursa ya kusimulia kipekee habari za Afrika kuhusu siasa za kimataifa kwa mtazamo wetu.

Tumezoea kuona mawasiliano kutoka kwa viongozi wa kigeni kwenda kwa wakuu wa nchi au serikali za Kiafrika, lakini ni mara chache mno kuona majibu.

Tumezizoea hizi siri, ikiwa ni pamoja na matukio yetu ya kihistoria, kufichuliwa na watu wengine – mtazamo huu unapaswa kubadilika na kukumbatia historia zetu. Kufahamu mambo yaliyojiri katika vyumba na koridoo zilizounda historia, ni muhimu kwa Waafrika na vizazi vijavyo.

Matumaini yetu ni kwamba Tovuti ya Kumbukumbu ya Salim Ahmed Salim itawahimiza viongozi na serikali za Afrika kueleza zaidi habari ya yale yaliyojiri huko nyuma, ili kuonyesha jukumu la Afrika katika kuunda siasa za kimataifa .

Kwa kufanya hivyo, wanadiplomasia wa Afrika wataweza kuunda na kushawishi mustakbali wa usoni - ambapo inakadiriwa 25% ya idadi ya watu ulimwenguni itakuwa ni kutoka bara hili ifikapo 2050.

Ahmed Salim ni mtoto wa Dkt Salim. Kumbukumbu kadhaa za kazi na mawasiliano ya Dkt Salim yanapatikana katika tovuti hii:

www.salimahmedsalim.com