Je, Raila Odinga anataka nini haswa?

Na Abdalla Seif Dzungu

BBC Swahili

.

Chanzo cha picha, bbcnews

Maelezo ya picha, Kiongozi wa upinzani Raila Odinga

Harakati mpya wa kisiasa zimeibuka nchini Kenya kati ya seriikali na upinzani baada ya kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Raila Odinga kusema kwamba hatambui uongozi wa rais William Ruto na serikali yake miezi mitano baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu nchini humo.

Raila Odinga badala yake amemtaka rais William Ruto na serikali yake kung’atuka mamlakani akidai kwamba hawakuchaguliwa kihalali katika uchaguzi uliokamilika tarehe tisa mwezi Agosti 2022.

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa 2022, William Ruto aliibuka mshindi baada ya kumshinda Raila Odinga kwa zaidi kura 200,000. Hatahivyo raila alipinga matokeo hayo katika mahakama ya juu ambayo baada ya vikao vyake ilimuishnisha Rais William Ruto kuwa rais aliyechaguliwa kihalali

Hatahivyo Raila anasema kwamba ana ushahidi kutoka kwa afisa wa IEBC aliyejitolea kwamba maafisa wa tume hiyo ya Uchaguzi walichakachua matokeo hayo ili kumpatia ushindi mpinzani wake William Ruto.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya uchunguzi ilio chini ya viongozi wa upinzani pekee, Raila Odinga anadaiwa kumshinda Rais william Ruto kwa zaidi ya kura milioni mbili katika uchaguzi uliopita.

Hatahivyo akijibu madai hayo ya Raila Odinga, Rais William Ruto alinukuliwa akisema kwamba Kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akijaribu kuishinikiza serikali yake kuingia makubaliano ya kufanya kazi naye maarufu kama handshake.

Rais huyo aliapa kwamba hatokubali kudanganywa na akafutilia mbali mapatano yoyote na Bw. Odinga .

“Nataka kuwaambia wasahau handshake, na usituambie hutaki handshake. Tunakufahamu na tunaweza kukuona,’’ Dkt Ruto alisema alipohutubia waombolezaji kaunti ya Kiambu wakati wa ibada ya mazishi ya Pauline Nyokabi, dadake Waziri wa Biashara Moses Kuria

“Hii maandamano yote wanafanya hawafanyi juu ya wananchi, wanafanya juu ya ubinafsi, familia zao na biashara zao, Ruto alinukuliwa akisema.

"Rafiki yangu, si ni wakati wa kubadilisha mbinu?" alisema. “Hakuna namna utanizidi ujanja. Sahau kuhusu mambo ya kupeana mikono.”

Kiongozi huyo wa nchi vilevile, ameonesha ari ya kumkabili Raila Odinga kupitia kuwavutia wandani wake katika Muungano wa Azimio kushirikiana nao katika serikali yake.

Raila: ‘Sitaki handshake na Ruto’

.

Chanzo cha picha, Ikulu ya rais Kenya

Maelezo ya picha, Rais William Ruto
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini akimjibu rais William Ruto katika mkutano uliojaa maelfu ya wafuasi wake katika uwanja wa Jacaranda mjini Nairobi Raila alisema kwamba hana haja ya kufanya makubaliano yoyote na bwana William Ruto na kwamba , William Ruto alipaswa kuondoka madarakani.

Raila alikariri madai ambayo aliyatoa kwa mara ya kwanza Januari 23 alipowasili nchini Kenya kutoka Afrika Kusini.

Aliitaka serikali ya Kenya Kwanza kujiuzulu mara moja na kuwasihi wafuasi wake kukataa utawala wa UDA na kupinga ushuru wa adhabu unaotolewa na utawala huo, akimfananisha Rais William Ruto na Zakeo wa Biblia ambaye alikuwa mtoza ushuru.

“Bwana Ruto sasa amekuwa yule Zakayo ambaye alikuwa anatoza ushuru kwa Bibilia. Tumeambia Wakenya wakatae kutoa ushuru kwa bwana Zakayo’’.

Pia alikashifu kuwa utawala huo umebadilisha maafisa wa serikali katika mashirika muhimu ya umma na badala yake kuwapatia nyadhfa hizo wapambe wa UDA, na hivyo kufungua njia ya uporaji wa rasilimali za umma ambao haujawahi kushuhudiwa.

Matamshi hayo pia yaliungwa mkono na mgombea mwenza wa Raila Odinga, Martha Karua katika uchaguzi wa 2022 aliyemtaka rais Ruto kuondoka madarakani mara moja akiongezea: ‘’Hatuogopi tulizaliwa siku moja na tutaondoka ulimwenguni siku moja’’.

Raila ambaye amekuwa akionekana kucheza karata yake ya 2017, ambayo ilisababisha kupeana mkono kati yake na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018, hatahivyo alisisitiza kwamba hataki ushirikiano wowote na kile anachodai kuwa ni 'Urais Haramu.'

"Wanasema kwamba tunapenda maandamano na kwamba tunataka kupeana mkono ninasema hapa leo, sitaki chochote cha kufanya na kupeana mkono," alisema.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Raila Odinga na wafuasi wake

Je Raila anataka nini haswa?

Na mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa David Burare

Kulingana na mchambuzi huyu , historia ya Raila katika serikali zilizopita inaonesha kwamba amekuwa akipigania makubaliano ya kumshirikisha katika serikali maarufu ‘handishake’.

‘’Licha ya kwamba hataki kukubali ukweli Raila amekuwa akipigania handshake, kwanini basi anaita jamii ya kimataifa, anafanya hivyo ili asionekane kwamba ni yeye anayetaka hivyo’’, alisema bwana Burare.

Bwana Burare anasema kwamba Raila anahisi kwamba hajamalizika kisiasa na kwamba bado ana ajenda ya kuongoza taifa hili ambayo hajaitimiza , hivyobasi hataki kupoteza wafuasi wake kote nchini .

‘’Raila hataki kupoteza ufuasi wake nchini hivyobasi amerudi kujiimarisha ili ajiaendae kwa uchaguzi wa 2027, ninakuhakikishia kwamba Raila atawania Urais 2027’’, aliongezea mchambuzi huyo.

Amesema kwamba sababu nyengine ambayo imemfanya Raila kuanza uadui na serikali ya William Ruto ni uhasama uliopo kati ya aliyekuwa rais Uhuru Kenyatta na William Ruto. Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, Uhuru anaamini kwamba rais William Ruto anaendeleza vita vya kulipa kisasi dhidi yake hivyobasi amekuwa akimfadhili Raila Odinga kwani anaamini ni yeye tu ambaye ana uwezo wa kumuondoa madarakani William Ruto.

 ‘’Kila akimaliza mikutano yake, kila mara Raila amekuwa akinukuliwa akisema serikali ya Ruto iwachane na Uhuru Kenyatta. Hili ni thibitisho kwamba huenda Uhuru ndiye mfadhili wa mikutano hiyo’’, aliongezea.

Vilevile mchambuzi huyu anasema kwamba Raila amesikika akisema hawezi kustaafu na haendi popote katika mikutano yake

Jinsi Raila Odinga alivyoshirikiana na serikali zilizopita

.

Chanzo cha picha, bbcnews

Maelezo ya picha, Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wakati wa maamkuzi ya handshake

Baada ya Raila kugombea katika uchaguzi mkuu wa 1997 na kushindwa na rais wa zamani Moi, Tarehe 18 Machi 2002 aliongoza muungano kati ya chama chake cha NDP na Kenya African National Union (KANU) kilichoongozwa na Rais Daniel arap Moi.

Kulingana na vyanzo vya habari, vyama hivyo viwili viliungana katika juhudi za kuongeza nafasi zao za kushinda uchaguzi mkuu wa 2002 kwani "NDP kilikuwa chama cha pili kwa ukubwa cha upinzani ambacho kiliungwa mkono na wapiga kura wa kabila la Luo la Odinga kutoka magharibi mwa Kenya"

Hata hivyo, Julai 2002 Rais Moi hakumuidhinisha Raila Odinga kama mgombea urais wa KANU, jambo ambalo liliripotiwa kuwa mojawapo ya masharti ya muungano wa KANU-NDP, lakini badala yake akamuidhinisha Uhuru Kenyatta.

Kutokana na hali hiyo, Raila Odinga na waliokuwa viongozi wa NDP pamoja na baadhi ya viongozi wa KANU waliongoza uasi na kuungana na kundi la “muungano mkubwa wa upinzani” unaoitwa National Rainbow Coalition (NRC).

Walimshinda Uhuru Kenyatta katika uchaguzi ambapo Mwai Kibaki alikua rais baada ya kuidhinishwa na Raila kupitia ‘Kibaki Tosha’.

Hata hivyo alitofautiana na Rais Kibaki na akafutwa kazi kama Waziri kuelekea uchaguzi mkuu wa 2007 baada ya Kibaki kukiuka ahadi kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mkataba wa maelewano na Odinga.

Mwaka wa 2007 alishindana na Rais Kibaki katika uchaguzi ambao ulikuwa na mzozo mkubwa baada ya Kibaki kutangazwa mshindi. Raila aliongoza maandamano nchini kote kupinga matokeo.

Jumuiya ya kimataifa ilijibu haraka. Kisha Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayehusika na masuala ya Afrika Jendayi Frazer alisafiri hadi Nairobi, akifuatiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Condoleezza Rice, kusukuma pande hizo mbili kufikia mwafaka kujpitia mpatanishi Koffi Annan, ambapo Raila alitajwa kuwa Waziri Mkuu na kugawana Serikali kwa misingi ya 50-50 na Rais Kibaki.

2017: Aliwania urais kwa mara ya nne kwa tiketi ya NASA na kushindwa na Uhuru Kenyatta

Odinga alifanikiwa kupinga ushindi wa Uhuru mahakamani, ushindi ukatangazwa kuwa batili na kulazimika kurudia uchaguzi, Odinga alijiondoa kwenye marudio ya uchaguzi ambapo Uhuru alitangazwa kuwa Rais.

Raila alijiapisha kama "rais wa watu" na akaitisha maandamano nchini kote dhidi ya Serikali.

2018: Kufuatia shinikizo za maandamano ya raila Oidnga , Uhuru aliamua kupatanisha pande pinzani kwa kupeana mikono mbele ya mamilioni ya Wakenya na kufanya kazi kama mshauri wa Rais Uhuru katika masuala mengi ya serikali.