Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mumeo anateswa, na ni kosa lako'
Svitlana mwanamke mwenye umri wa miaka 42 huko Kyiv, alikuwa anasubiri habari kuhusu mumewe Dima, daktari wa jeshi aliyekamatwa na Urusi, kwa zaidi ya miaka miwili na ghafla alipigiwa simu.
Sauti katika simu ilimwambia ikiwa atafanya uhaini dhidi ya Ukraine, Dima ataweza kupata matibabu bora gerezani, au hata kuachiliwa mapema.
"Ni nambari ya Ukraine ndio ilinipigia simu. Alijitambulisha kuwa anaitwa Dmitry," anaeleza Svitlana. "Alizungumza kwa lafudhi ya Kirusi."
"Dimtry alisema, 'unaweza kuchoma ofisi ya uandikishaji ya jeshi, kuchoma moto gari la jeshi au kuharibu miundombinu ya Shirika la Reli la Ukraine."
Kulikuwa na chaguo jingine: kufichua maeneo ya vikosi vya ulinzi wa anga vilivyo karibu - vikosi muhimu ambavyo huiweka anga ya Ukraine salama dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Urusi.
Dmitry alipotoa pendekezo lake, Svitlana anasema alikumbuka maagizo ambayo serikali ya Ukraine iliyasambaza kwa familia zote endapo wangetafutwa na mawakala wa Urusi: rekodi na kupiga picha kila kitu, na uripoti.
Svitlana aliripoti, na akapiga picha jumbe hizo, ambazo alizionyesha kwa BBC.
Idara ya Usalama ya Ukraine, SBU, ilimwambia aendelee kuzungumza nao wakati wao wanachunguza. Kwa hivyo alijifanya kukubali kulipua miundombinu ya reli ya eneo hilo.
'Mumeo anateswa na ni kosa lako!'
Tunapoketi naye kwenye sebule yake, huku ving'ora na mashambulizi ya anga yakilia nje, alitusikilizisha rekodi ya namna anavyoelekezwa kutengeneza bomu.
"Mimina lita moja ya mafuta ya taa na ongeza kidogo ya petroli," Dmitry anaelezea. "Nenda kwenye makutano ya reli. Hakikisha hakuna kamera za usalama. Vaa kofia."
Baadaye, SBU ilimwambia Svitlana kwamba mwanaume aliyekuwa akiongea naye alikuwa nchini Urusi, na anapaswa kuachana naye. Svitlana alimwambia Dmitry kuwa amebadilisha mawazo yake.
"Hapo ndipo vitisho vilianza," anasema Svitlana, "Alisema watamuua mume wangu, na sitamwona tena.
Kwa siku kadhaa, aliendelea kupiga simu, akisema: "Mume wako anateswa, na ni kosa lako!"
Katika taarifa kwa BBC, SBU inasema kushirikiana na mawakala wa Urusi "hakutaboresha hali za wafungwa, kinyume chake, kunaweza kutatiza uwezo wa kubadilishana wafungwa."
"Ikiwa jamaa wa wafungwa watakubali kufanya hujuma au ujasusi," inasema SBU, "hilo linaweza kuainishwa kama uhaini. Adhabu ni kifungo cha maisha."
Serikali hutangaza mara kwa mara kukamatwa kwa Waukreni wanaodaiwa kuchoma moto au kufichua eneo la kijeshi kwa ajili ya Urusi.
Vyombo vya habari vya vinavyounga mkono Kremlin vimejaa video zinazodaiwa kuwaonyesha raia wa Ukraine wakichoma magari ya jeshi au masanduku ya umeme ya reli.
Baadhi ya wahalifu hufanya hivyo kwa pesa, hulipwa na maajenti wanaoshukiwa kuwa ni wa Urusi, lakini inaamini pia kuna mashambulizi yanayofanywa na jamaa wa wafungwa kwa sababu ya kukata tamaa.
Haitosaidia wapendwa wao
Petro Yatsenko, kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Ukraine katika kitengo cha Matibabu ya Wafungwa wa Vita, anasema karibu 50% ya familia zote hupigiwa simu na mawakala wa Urusi.
"Wako katika mazingira magumu sana na baadhi yao wako tayari kufanya lolote," anasema Petro, "lakini tunajaribu kuwaelimisha kwamba haitasaidia [wapendwa wao walio shikiliwa]."
Petro anasema kitendo kama kuchoma moto gari la jeshi hakizingatiwi kuwa ni hasara kubwa kwa Wanajeshi wa Ukraine:
"Lakini kinaweza kuyumbisha umoja wa jamii ya Ukraine, kwa hivyo hilo ndilo tatizo kuu."
"Na ikiwa mtu atatoa taarifa kuhusu eneo la mfano, mifumo ya ulinzi wa anga, hilo ni tatizo kubwa kwetu," anaeleza.
Serikali haichapishi idadi ya Waukraine wanaoshikiliwa kama wafungwa wa vita, lakini idadi hiyo inadhaniwa kuwa zaidi ya 8,000.
Afisa wa ujasusi wa Ukraine aliiambia BBC kwamba idadi ya kesi ambapo jamaa wanakubali kufanya kazi na Urusi ni ndogo.
Serikali ya Urusi iliiambia BBC katika taarifa yake kwamba madai ya kuzitumia familia za wafungwa "hayana msingi," na Urusi inawatendea vyema "wafungwa wa Ukraine kwa ubinadamu na kwa kufuata kikamilifu Mkataba wa Geneva."
Taarifa hiyo inaishutumu Ukraine kwa kutumia njia kama hiyo:
"Waukraine wanajaribu kuwashurutisha wakaazi wa Urusi kufanya vitendo vya hujuma na uchomaji moto ndani ya ardhi ya Urusi, wakilenga miundombinu muhimu na maeneo ya kiraia."
Mume wa Svitlana Dima aliachiliwa zaidi ya miezi mitatu iliyopita.
Wanandoa hao sasa wako pamoja kwa furaha, na wanafurahia kucheza na mtoto wao wa miaka minne, Vova.
Dima alimwambia mke wake kwamba Warusi hawakutekeleza vitisho vyao vya kumwadhibu kwa kukataa kwake kutoa ushirikiano.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah