'Wanajeshi wa Urusi waliojisalimisha, tuliwachukua kama wafungwa waliotushambulia, tuliwaua'

Muda wa kusoma: Dakika 6

Kwa takriban saa 72 zilizopita, kimbunga cha kutisha kilicho juu ya vichwa vyetu kimekuwa cha ndege zisizo na rubani za Urusi ambazo zimekuwa, zikipita na kisha kushambulia malengo yao.

Sasa gumzo linaelekezwa kwenye ndege ya Ukraine isiyo na rubani ambayo haijatumwa kuua, bali kusambaza picha kutoka uwanja wa mazoezi hadi kwa makamanda chini Ukraine.

Tumeletwa kwenye eneo la mafunzo la siri katika eneo la Chernihiv ambapo usajili wa wanajeshi wapya unaharakishwa katika juhudi mpya za kulizuia jeshi la Urusi kusonga mbele.

Katika mvua ya milio ya risasi na amri za waalimu, kinachovutia zaidi katika eneo hilo ni umri wa wanajeshi wapya. Wengi wanaonekana kuwa kati ya miaka ya 40 na 50.

Miongoni mwa kundi la watu wenye mvi, ni Rostyslav, ambaye mke wake na watoto wawili wanamngojea nyumbani katika mkoa wa Odesa.

Mwezi mmoja uliopita alikuwa dereva. Mwezi ujao anaweza kujikuta akipigana katika ardhi ya Urusi, huku Ukraine ikiapa kushikilia ardhi ambayo iliiteka katika eneo la Kursk wakati wa uvamizi wake mwezi mmoja uliopita.

"Nadhani hili ni jambo sahihi kufanya," anasema kuhusu operesheni hiyo.

"Tazama ni muda gani wamekaa kwenye ardhi yetu. Tumeteseka kwa muda mrefu, tunapaswa kufanya kitu. Huwezi tu kukaa pale wakati wanateka eneo letu. Tutafanya nini baadaye? Je, tutakuwa watumwa wao?"

Ratiba ya mafunzo tunayoshuhudia inaonyesha mpango unaoharakishwa ambao wanajeshi wapya wanaojiunga na jeshi wanapitia wakati Ukraine inapojaribu kukabiliana na kundi kubwa la wanajeshi ambao Urusi imewaweka kwenye mstari wa mbele.

Wizara ya Ulinzi huko London ilikadiria kuwa kulikuwa na wanajeshi 70,000 wa Urusi nchini Ukraine mwezi Mei na Juni pekee.

Chini ya jua kali, wanajeshi wapya wa Ukraine wanaonekana wakiruka kutoka kwenye magari ya kivita yaliyotengenezwa na Marekani na kufyatua risasi kwenye maeneo ya adui.

Wanajeshi, wakiwa na wasiwasi kwamba eneo la mafunzo haya bado ni siri, waliomba kuona picha tulizorekodi kwenye eneo kabla ya habari hii kuripotiwa kote katika Habari za BBC - lakini hawakuona hati zozote wala kuwa na udhibiti wowote wa uhariri.

Katika msitu ulio karibu, shambulio la Urusi lililoigizwa kwenye handaki la wanajeshi wa Ukraine linazuiwa huku mazoezi ya kulenga shabaha ya guruneti yakitetemesha eneo hilo.

Miaka miwili na nusu ya vita, na Ukraine inatamani sana wanajeshi zaidi na imeanzisha sheria mpya ya kuwasajili raia jeshini ambayo inapunguza umri wa wanaume kujiunga kutoka umri wa miaka 27 hadi 25.

Huduma ya kijeshi kwa wanawake sio lazima.

Msukumo wa kuandikishwa kwa vijana haujafikia kundi hili la wanaume.

Askari wapya wote wapo mbele yetu na tayari wamekuwa na siku 30 za mafunzo ya kimsingi na leo ni mafunzo ya huduma ya kiafya - kukabiliana na kuvunjika kwa mifupa, majeraha ya risasi na kuvuja damu kwa wingi - kwa kutumia vifaa vya matibabu vilivyotumwa kutoka Uingereza.

Kuna mafunzo ya hapa na pale kuhusu kutumia kifaa cha tourniquet kuwafunga wanaovuja damu.

Ukweli ni kwamba huduma ya dharura inayotolewa inaweza kuhitajika katika hali mbaya katika kipindi cha wiki na miezi ijayo.

Askari mmoja ambaye ameandamana nasi katika eneo hilo anasema kwamba ikiwa wanajeshi wapya hawajapata ujuzi wa kutosha wa kupigana hawatatumwa mstari wa mbele.

"Hatutawapeleka kwenye vifo vyao," anasema kwa ukali.

Bado, tumesikia malalamiko, hasa kutoka kwa wanajeshi walio na uzoefu zaidi kwamba, wanajeshi wapya wametumwa katika mstari wa mbele wengine bila mafunzo ya kutosha na kuingizwa kabla ya muda katika mapambano ya mstari wa mbele.

Ukraine inarudi nyuma katika sehemu muhimu za uwanja wa vita nyumbani, haswa karibu na mji muhimu wa kimkakati wa Pokrovsk huko Donetsk.

Lakini uvamizi wa mwezi uliopita nchini Urusi umeongeza ari namwelekeo mpya wa vita.

Hata hivyo, Kyiv sasa inapigana vita katika upande mwingine na hii ni kama kucheza kamari kwa Rais Zelensky.

Majenerali wake wana maamuzi magumu ya kimkakati ya kufanya kuhusu wapi pa kupeleka wanajeshi wao wapya.

Maxim, mjenzi mwenye umri wa miaka 30, anaonekana kuwa mwenye umri mdogo zaidi kati ya kundi hilo.

"Tunahitaji kujifunza, kujifunza na kujifunzo tena. Kadiri tunavyofundisha ndivyo tutajifunza zaidi hapa. Itatusaidia kwenye mstari wa mbele.”

Hiyo itakuwa wapi, nauliza? "Tuko tayari kutetea ardhi yetu huko Donbas - au Kursk," anasema kwa fahari lakini kwa kicheko cha wasiwasi.

Hapo awali, katika eneo la Sumy, nchini Ukraine, tulikuwa tumesafiri chini ya ulinzi wa kijeshi hadi kwenye kambi mpya ya Ukraine yapata maili chache tu kutoka mpaka wa Urusi.

Njiani, tulipita mitaa iliyolipuliwa na vifaru vya Urusi.

Raia walikuwa wameondoka , na maisha pekee ya binadamu yalikuwa yamefunikwa na kijani kibichi na wanajeshi wanaoendesha magari ya jeshi.

Tunapowasili kambini, gari linalobeba silaha za kivita likiwa limetoka kutoka uvamizi wa Kursk linanguruma na kurudi nyuma kwenye maficho yake yaliyo chini .

"Wanajeshi wa Urusi waliojisalimisha, tuliwachukua kama wafungwa wa vita. Warusi waliotushambulia, tuliwaua.”

Ni tangazo kali kutoka kwa kamanda wa Ukraine ambaye kwa jina la utani anaitwa ‘Storm".

Brigedi yake ya 22 ilikuwa ya kwanza kuingia katika eneo la Urusi na sasa amerudi kusimulia hadithi yake.

"Tulienda katika mkoa wa Kursk. Tulikuwa peke yetu kama timu ya mbele. Tulikuwa katika nchi ya kigeni na tulihisi kama wageni. Sio nyumbani kwetu."

Akiwa baba wa watoto watano na mmiliki wa shahada tano, Storm ni jitu lenye miraba , ana mvi na tatoo za kijeshi kwenye ngozi ambayo haijafunikwa na vazi alilovaa.

"Ni sisi, hapa ndani," anasema akituonyesha video kwenye simu yake ya APC wakipitia mashamba ya Urusi.

Ilikuwaje kupigana na Warusi kwenye ardhi yao wenyewe, niliuliza?

"Nilijijali mwenyewe na kikundi changu, kwa kila mtu. Bila shaka, kulikuwa na hofu. "

Kama wanajeshi wote wa Ukraine nilivyokutana nao, Storm inaeleweka kuwa anasitasita kutoa taarifa yoyote ya uendeshaji ambayo inaweza kuwasaidia Warusi.

Kwa hivyo ninapouliza ikiwa anajua ni muda gani atasalia kwenye eneo la Urusi atakaporudi, ni jibu linalotabirika kwa uzalendo na fupi juu ya mambo maalum.

“Tunatekeleza agizo. Tutakuwa huko mradi tu tumeambiwa. Tukiambiwa tusonge mbele, tutasonga mbele. Wakituambia tujitoe, tutajiondoa.”

Anaendelea katika hali hiyo hiyo: "Ikiwa tuna agizo la kusonga mbele, tunaweza kufika Moscow - na tutaonyesha nini maana ya Ukraine na jinsi watu wetu walivyo - Jasiri halisi."

Imeripotiwa kuwa Ukraine ilituma hadi wanajeshi 10,000 wa wasomi nchini Urusi kama sehemu ya kupiga hatua za haraka.

Wizara ya ulinzi ya Urusi inadai Kyiv imepata maelfu ya majeruhi.

Mkuu wa jeshi la Ukraine, Jenerali Oleksandr Syrskyi, alitangaza kwamba Warusi sasa wametuma wanajeshi 30,000 kulinda Kursk.

Takwimu hizi zote ni ngumu kuthibitisha.

Katika eneo lingine la siri, wanajeshi wengine wanashuka kutoka kwa gari la uokoaji la kivita la Bergepanzer lililoundwa na Ujerumani.

Dereva, ambaye anaitwa jina la utani ‘Producer’ ni baba wa watoto wawili ambaye hajawaona kwa miaka mitatu.

Walitorokea Italia na mama yao wiki chache baada ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo Februari 2022.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla