Keir Starmer: Je, Waziri Mkuu mpya wa Uingereza ni nani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Sir Keir Starmer amekuwa waziri mkuu mpya wa Uingereza, baada ya kukiongoza chama cha Labour kwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu.
Sir Keir alichukua nafasi ya mwanasiasa wa msimamo mkali kutoka mrengon wa kushoto Jeremy Corbyn kuwa kiongozi wa chama cha Labour miaka minne iliyopita na amefanya kazi ya kukirudisha chama katikati, ili kukifanya kiweze kuchaguliwa zaidi. Chama cha Labour kilikuwa kimeondoka madarakani kwa takriban miaka 14.
Chama cha Conservative cha Waziri Mkuu wa sasa, Rishi Sunak, kimekumbwa na anguko kubwa.
Maisha yake kabla ya siasa
Starmer sio mwanasiasa wa kawaida. Hakuingia Bungeni hadi alipokuwa na umri wa miaka 50, baada ya kazi nzuri kama mwanasheria.
Na tofauti na wabunge wengi, aliingia katika Baraza la Commons kwa kuteuliwa na Malkia Elizabeth II mwaka 2014, kwa kutambua jukumu lake kama Mkurugenzi wa mashtaka, cheo cha juu zaidi cha mwendesha mashtaka ya jinai nchini Uingereza na Wales.
Starmer, mwanasheria wa haki za binadamu mwenye umri wa miaka 61; Baba yake alikuwa ni mtengeneza vifaa kiwandani na mama yake alikuwa nesi.
Baada ya kumaliza skuli, alikua mtu wa kwanza katika familia yake kwenda chuo kikuu. Alihitimu sheria katika Chuo Kikuu cha Leeds na baadaye akamaliza masomo yake na shahada ya uzamili huko Oxford.
Alibobea katika masuala ya haki za binadamu na kazi yake ilimpeleka katika visiwa vya Caribbean na Afrika, ambako alitetea wafungwa waliohukumiwa kifo.
Maisha yake ya London

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika miaka yake ya mwanzo huko London, Starmer alikuwa akiishi katika "ghorofa yenye mimea mingi" juu ya danguro.
Mmoja wa marafiki zake wa wakati huo, mwandishi wa habari Paul Vickers, alimuelezea Stermer kama "kijana aliyependa kujirusha."
Kuhusu baba yake, Starmer anasema alikuwa ni mtu wa maisha ya peke yake, asiye na marafiki wengi. Lakini anakiri kuwa amejifunza kutoka baba yake, "kuwa muwajibikaji, heshima na kujivunia kazi yako.”
Mama yake aliteseka kwa muda mrefu kutokana na ugonjwa uliomfanya kutoweza kuzungumza au kutembea. Kudorora kwa hali yake, kulipelekea madaktari kumkata mguu mmoja.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kuhusu mke wake, Starmer anakiri mambo hayakuanza vizuri na mke wake. Katika mahojiano na kituo cha ITV, mwanasiasa huyo alieleza jinsi alivyokutana na Victoria.
"Nilikuwa napeleka kesi mahakamani na matokeo yalitegemea iwapo stakabadhi hizo zilikuwa sahihi au la," anasema.
"Niliuliza timu yangu ni nani aliyeziandika. Wakasema ni mwanasheria anayeitwa Victoria, nikasema, ngoja nimpigie."
Alipozungumza naye, alimhoji kuhusu nyaraka hizo lakini kabla ya mazungumzo kuisha, alimsikia akisema.
"Hivi anajiona yeye kama nani? Na kisha akakata simu. Na sikuwa na chaguo ila kukubaliana na matokeo," aliongeza.
Ili kusuluhisha hilo, Starmer alimwomba Victoria waonane baa. Hiyo likuwa mwanzoni mwa miaka ya 2000 na baadaye walifunga ndoa mwaka 2007. Wana watoto wawili.
Aliingiaje madarakani?
Baada ya ushindi wa Brexit, na mchakato wa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya (EU), kwa miaka minne Starmer alisimamia shughuli zote za chama cha Labour zilizohusu Uingereza kuondoka EU.
Mwanasiasa huyo, ambaye kuna wakati alijitokeza kuunga mkono kura ya pili ya maoni, wakati wote huo alikuwa na uhusiano wa kutatanisha na mtangulizi wake wa chama, Jeremy Corbyn.
Baada ya kushindwa vibaya kwa chama cha Labour katika uchaguzi mkuu wa 2019, ambao ulimweka madarakani mwanasiasa wa kihafidhina Boris Johnson, Starmer aligombea uongozi wa chama na alishinda Aprili 2020.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika hotuba yake ya ushindi, aliahidi kukiongoza chama hicho "katika enzi mpya za kujiamini na matumaini." Lakini kulikuwa na changamoto njiani.
Mwaka 2021, Conservative walichukua kiti cha jimbo la Hartlepool kutoka Labour, mji wa kaskazini-mashariki mwa Uingereza ambao haujawahi kuwa na Mbunge wa Conservative.
Hilo lilileta pigo kwa juhudi za Starmer za kupata uungwaji mkono katika ngome za muda mrefu za chama cha Labour.
Matokeo yalikuwa mabaya kiasi kwamba, kiongozi huyo, aliwaambia wafanyakazi wake, anajiuzulu kwa sababu kilichotokea kilionyesha chama kinarudi nyuma na alijiona yeye ndiye anakataliwa.
Hakujiuzulu, lakini kilichotokea kilimsukuma kufikiria tena kuhusu sera na upangaji upya wa timu yake katika ngazi ya juu ya uongozi.
Lengo lilikuwa ni kuwarudishia wapiga kura wa chama cha Labour, waliokwenda kwa mhafidhina Boris Johnson, katika ngome za zamani za Labour - zinzojuulikana kama Red Wall.
Marekebisho ya ndani yalitokea. Starmer alimsimamisha kazi mtangulizi wake, Jeremy Corbyn, wakati uchunguzi kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi ndani ya chama ukifanyika.
Hilo lilimaanisha Corbyn hakuweza kusimama kama mgombeaji wa Ubunge wa chama cha Labour katika uchaguzi huu. Lakini alisimama kama mgombea huru na ameshinda.
Ukosolewaji

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasiasa wengine wa chama cha Labour pia wanasema wamezuiwa kugombea na kumtuhumu Starmer kujaribu kuwaondoa watu wa mrengo wa kushoto katika chama.
Vilevile wanamtuhumu, kushirikiana na mwanachama wa muda mrefu wa chama cha Labour: Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair.
Starmer alijaribu kuziondoa hofu za Waingereza kwa kusema; Labour haitaingia kwenye matumizi yasiyo ya lazima.
Mwezi Februari, aliitupilia mbali moja ya ahadi zake kubwa kuhusu matumizi ya pauni bilioni 28 (dola bilioni 35), kwa mwaka katika sera rafiki na mazingira.
Hilo limechangia kuwa na mvuto kwa wapiga kura wengi lakini pia wapiga kura wengine wanamuona kama mwanasiasa asiye madhubuti.
Siku zijazo, Uingereza itajifunza mambo mengine kuhusu mwanasiasa huyu wa chama cha Labour, atakapohamia 10 Downing Street, ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza.
End of Pia unaweza kusoma
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla












