Ujauzito wa miezi 15!: Fahamu sakata la mimba za 'muujiza' Nigeria

Chioma anasisitiza kuwa Hope ni mwanae
Muda wa kusoma: Dakika 6

Chioma anasisitiza kuwa Hope, mtoto wa kiume anayembeba mikononi mwake, ni mwanawe. Baada ya miaka minane ya majaribio ya kupata mimba kushindikana, anamwona kama mtoto wake wa miujiza.

"Mimi ndiye mmiliki wa mtoto wangu," anasema kwa kujiamini.

Ameketi karibu na mume wake, Ike, katika ofisi ya afisa wa serikali ya Nigeria ambaye hutumia muda kuwahoji wanandoa hao.

Kama kamishna wa masuala ya wanawake na ustawi wa jamii katika jimbo la Anambra, Ify Obinabo ana uzoefu wa kutosha katika kusuluhisha migogoro ya familia - lakini safari hii sio wa kawaida.

Ndugu watano wa familia ya Ike, ambao pia wapo katika chumba hicho, hawaamini kuwa Hope ni mtoto wa kibiolojia wa wanandoa hao, kama Chioma na Ike wanavyodai.

Chioma anadai "kubeba" mimba ya mtoto huyo kwa takriban miezi 15. Kamishna na familia ya Ike hawaamini madai hayo.

Chioma anasema alikabiliwa na shinikizo kutoka kwa familia ya Ike kubeba mimba. Walimwomba hata aoe mwanamke mwingine.

Katika hali yake ya kukata tamaa, alitembelea "kliniki" inayotoa "matibabu" yasiyo ya kawaida - kashfa ya ajabu na ya kutatanisha inayowakabili wanawake wanaotamani kuwa mama ambayo inahusisha usafirishaji haramu wa watoto.

BBC iliruhusiwa na mamlaka kuhudhuria mazungumzo ya kamishna na Chioma kama sehemu ya uchunguzi wetu kuhusu sakata la ujauzito.

Tumebadilisha majina ya Chioma, Ike na wengine katika makala haya kwa usalama wao katika jamii zao.

Kamishna wa jimbo Ify Obinabo anajaribu kukabiliana na udanganyifu huo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nigeria ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya kuzaliana duniani, huku wanawake mara nyingi wakikabiliwa na shinikizo la kijamii kushika ujauzito na hata kutengwa au kunyanyaswa ikiwa hawawezi.

Chini ya shinikizo hili, baadhi ya wanawake huvuka mipaka ili kutimiza ndoto yao ya kuwa mama.

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, BBC Africa Eye imekuwa ikichunguza kashfa ya "mimba isiyoeleweka".

Walaghai wanaojifanya kuwa madaktari au wauguzi huwashawishi wanawake kwamba wana "matibabu ya kimuujiza ya uwezo wa kuzaa" ambayo yamehakikishwa kuwasaidia kupata mimba.

"Matibabu" ya awali kwa kawaida hugharimu mamia ya dola na huwa na sindano, kinywaji, au kitu kinachoingizwa kwenye uke.

Hakuna hata mmoja wa wanawake au maafisa tuliozungumza nao wakati wa uchunguzi wetu anayejua kwa uhakika ni nini kilicho katika dawa hizi.

Lakini baadhi ya wanawake wametuambia kililisababisha mabadiliko katika miili yao - kama vile matumbo ykuwa makubwa - ambayo yaliwashawishi kuamini kuwa walikuwa wajawazito.

Wanawake waliopewa "matibabu hayo" huonywa kutotembelea madaktari au hospitali zozote za kawaida, kwani hakuna kipimo au kipimo cha ujauzito kitakachogundua kuhusu "mtoto" huyo, ambaye walaghai wanadai anakua nje ya tumbo la uzazi.

Wakati wa "kujifungua" mtoto ukifika, wanawake wanaambiwa uchungu utaanza mara tu wanapodungwa sindano yenye "dawa adimu na ya gharama kubwa", inayohitaji malipo zaidi.

Namna ya kujifungua inavyofanyika hutofautiana, lakini zote zina utata. Wengine hutulizwa tu na kuamka na alama kama ya kovu la kujifungua kwa kisu.

Wengine husema wanachomwa sindano ambayo husababisha usingizi, hali ya kuona kwamba wanaamini kuwa wanajifungua.

Vyovyote vile iwavyo, wanawake hupata watoto wanaopaswa kuwazaa.

Chioma anamwambia kamishna Obinabo kwamba wakati wake wa "kujifungua" ulipofika, yule anayejiita daktari alimdunga sindano kiunoni na kumwambia asukume.

Haelezi jinsi alivyoishia kumpata mwanae Hope, lakini anasema kujifungua kulikuwa na "uchungu".

Dr Ruth anaendesha kliniki ya ujauzito bandia katika jimbo la Anambra

Timu yetu inafaulu kujipenyeza katika mojawapo ya "kliniki" hizi za siri ikizungumza na mwanamke anayejulikana kwa wateja wake kama "Dr Ruth" kwa kujifanya kama wanandoa ambao wamekuwa wakijaribu kupata mimba kwa miaka minane.

Huyu anayefahamika kama "Dk Ruth" huendesha kliniki yake kila Jumamosi ya pili ya mwezi katika hoteli ya zamani mjini Ihiala, katika jimbo la kusini-mashariki la Anambra.

Nje ya chumba chake, wanawake wengi wanamngoja kwenye korido za hoteli, wengine wakiwa na matumbo yanayoonekana dhahiri.

Mazingira yote yanaonekana yenye taarifa njema. Kuna nyakati, shangwe kubwa ziliibuka ndani ya chumba hicho baada ya mwanamke kuambiwa kuwa ni mjamzito.

Ilipofika zamu ya wanahabari wetu walioficha utambulisho wao,"Dkt Ruth" anawaambia matibabu yamethibitishwa kuwa na matokeo mazunri.

Anampa mwanamke sindano, akidai itawawezesha wanandoa "kuchagua" jinsi ya mtoto wao ajaye - jambo lisilowezekana kimatibabu.

Baada ya kukataa sindano, "Dk Ruth" huwapa kifurushi cha vidonge vilivyosagwa pamoja na vidonge vingine vya kunywea nyumbani, pamoja na maagizo ya wakati wa kushiriki tendo la ndoa.

Matibabu haya ya awali yanagharimu naira 350,000 ($205; £165).

Mwandishi wetu wa siri hatumii dawa hizo wala kufuata maagizo yoyote ya "Dk Ruth" na anarudi kumuona wiki nne baadaye.

Baada ya kutumia kifaa kinachoonekana kama cha ultrasound kwenye tumbo la ripota wetu, sauti kama ya mapigo ya moyo inasikika na "Dkt Ruth" anampongeza kwa kuwa mjamzito.

Wote wawili wanashangilia kwa furaha.

Baada ya kuwasilisha habari hiyo njema, "Dk Ruth" anaeleza jinsi watakavyohitaji kulipia dawa "adimu" na ya gharama kubwa inayohitajika ili mtoto azaliwe, inayogharimu kati ya naira milioni 1.5 hadi mbili ($1,180; £945).

Bila dawa hii, ujauzito unaweza kudumu zaidi ya miezi tisa, "Daktari Ruth" anadai bila kuzingatia ukweli wa kisayansi, akiongeza: "Mtoto atakuwa na utapiamlo - tungehitaji kumuimarisha tena."

"Dr Ruth" hajajibu madai ambayo BBC imemuuliza.

Makumi ya wanawake walikuwa wakisubiri kumuona "Dk Ruth"

Kiwango ambacho wanawake waliojihusisha katika mchakato huo wanaamini kwa dhati madai hayo hayajulikani.

Lakini sababu za kuathiriwa na uongo huo mbaya zinaweza, kwa sehemu, kupatikana katika vikundi vya mtandaoni ambapo habari zisizo sahihi kuhusu ujauzito zimeenea.

Mtandao wa taarifa potofu

Mimba ya siri inayotambulika kitaalamu kama ’Cryptic’’ ni jambo la matibabu linalotambulika, ambalo mwanamke anakuwa hajui kuhusu ujauzito wake hadi hatua za mwisho.

Lakini wakati wa uchunguzi wetu, BBC ilipata taarifa potofu zilizoenea katika vikundi vya Facebook kuhusu aina hii ya ujauzito.

Mwanamke mmoja kutoka Marekani, ambaye hutumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kuzungumzia "mimba yake ya siri", anadai kuwa mjamzito "kwa miaka" na kwamba safari yake haiwezi kuelezewa kisayansi.

Katika kurasa za mtandao wa Facebook, machapisho mengi hutumia misamiati ya kidini kusifu "matibabu" ya uongo kama "muujiza" kwa wale ambao wameshindwa kupata ujauzito.

Taarifa hizi zote potofu husaidia kuimarisha imani ya wanawake katika ulaghai huo.

Wafuasi wa vikundi hivi sio tu kutoka Nigeria, lakini pia kutoka Afrika Kusini, Caribian, na Marekani.

Walaghai pia wakati mwingine huendesha na kuweka machapisho katika vikundi hivi, na kuweza kuwafikia wanawake wanaoonyesha nia ya kupata "matibabu".

Mara mtu anapoonyesha kuwa tayari kuanza mchakato huo wa kilaghai, anaingizwa katika vikundi vilivyo salama zaidi vya WhatsApp.

Huko, wasimamizi hutoa taarifa kuhusu "kliniki za siri" na namna mchakato wote unavyofanyika.

Bado nachanganyikiwa

Mamlaka zinatuambia kwamba ili kukamilisha "matibabu", walaghai hao huhitaji watoto wachanga wanaozaliwa na kufanya hivyo wanatafuta wanawake waliokata tamaa na walio hatarini, wengi wao wakiwa wenye umri mdogo na wajawazito, katika nchi hiyo ambayo utoaji mimba ni kinyume cha sheria.

Mnamo Februari 2024, wizara ya afya ya jimbo la Anambra ilivamia kituo ambapo Chioma "alijifungulia" mwanae Hope.

BBC ilipata picha za uvamizi huo, ambao ulionyesha eneo kubwa lililokuwa na majengo mawili.

Katika jengo moja kulikuwa na vyumba vyenye vifaa vya matibabu – kwa ajili ya wateja - wakati katika chumba kingine kulikuwa na wajawazito kadhaa waliowekwa hapo kinyume na matakwa yao. Wengine walikuwa na umri wa miaka 17.

Wengine wanatuambia walidanganywa kwenda huko, bila kujua watoto wao wangeuzwa kwa wateja wa matapeli.

Wengine, kama vile Uju, ambalo si jina lake halisi, waliogopa sana kuiambia familia kuwa walikuwa wajawazito na wakatafuta njia ya kujinasua.

Alisema alipewa naira 800,000 ($470; £380) kwa ajili ya mtoto huyo.

Alipoulizwa ikiwa anajutia uamuzi wake wa kumuuza mtoto wake, anasema: "Bado nimechanganyikiwa."

Kamishna Obinabo, ambaye amekuwa sehemu ya juhudi katika jimbo lake kukabiliana na ulaghai huo, anasema matapeli huwawinda wanawake walio katika mazingira magumu kama vile Uju ili kupata watoto.

Uju angemuuza mtoto wake mchanga, kama mamlaka hazingemuokoa

Mwishoni mwa mahojiano makali, kamishna Obinabo anatishia kumchukua mtoto Hope kwa Chioma.

Lakini Chioma anamsihi, na hatimaye kamishna anakubali maelezo yake kwamba yeye mwenyewe ni mwathirika na kwamba hakuwa ametambua kilichokuwa kikiendelea.

Kwa msingi huu anawaruhusu Chioma na Ike kumtunza mtoto - ikiwa wazazi wa kibaolojia wasipojitokeza kumdai.

Lakini wataalam wanaonya kuwa ulaghai kama huu utaendelea kushamiri,hadi pale mitazamo itakapobadilika dhidi ya wanawake, utasa, haki za uzazi na kuasili mtoto.

Imetafsiriwa na Martha Saranga