Viwango vya mimba kuharibika viko juu kwa 40% miongoni mwa wanawake weusi, utafiti umebaini

Wanawake weusi wanakabiliwa na uwezekano mkubwa wa hatari ya kuharibikiwa mimba kuliko wazungu, utafiti unasema.
Uchambuzi wa jarida la Lancet wa taarifa kuhusu mimba za wanawake milioni 4.6 katika nchi saba unaonesha kuwa mwanamke mweusi ana hatari ya 43% ya mimba yake kutoka
Lancet linatoa wito kwa watu nchini Uingereza kupewa usaidizi baada ya mimba zao za kwanza kutoka.
Kwa sasa, agizo la mwanamke kwenda katika kliniki maalumu kwa kawaida hutolewa baada ya mwanamke kupata tatizo la kutoka kwa mimba mara tatu pekee.
Nchi nyingi, ikiwemo Uingereza, hazikusanyi taarifa(data) za kuharibika kwa mimba.
Lakini tafiti zinakadiria kuwa:
- 15% ya mimba huishia kuharibika
- 1% ya wanawake watapata tatizo la kutoka kwa mimba zao linalojirudia
Baadhi zinakadiria kiwango cha kutoka kwa mimba kuwa cha juu zaidi ,lakini hivi ni kutokana na tofauti katika jinsi nchi zinavyoelezea kuharibika kwa mimba, ambako kunaweza kuwa ni katika aina ya kipimo cha mimba au kutokana na uchunguzi wa kitaalam kwa njia ya picha au video.
Ripoti hiyo pia imebaini kwamba wanawake wanaopatwa na tatizo la mimba zao kuharibika, kutokana na jamii zao, wanakabiliwa zaidi na matatizo ya muda mrefu ya kiafya, kama vile kuganda kwa damu, magonjwa ya moyo na msongo wa mawazo.
Unaweza pia kusoma:
Doreen Thompson-Addo na mumewe Reggie walipata tatizo la kuharibika kwa mimba saba.
"Nilipopata mimba kwa mara ya kwanza, nilifurahi sana ," alisema Doreen..
"Niliwaambia rafiki zangu na familia, nilianza kufikiria majina nitakayomuita mtoto wangu na kujiandaa kwa baby shower."
Lakini katika kipindi cha miezi miwili baada ya kutambua kuwa ana ujauzito, Doreen alianza kuvuja damu na akapoteza ujauzito.
"Unasikia jinsi tatizo la kutoka kwa mimba lilivyo la kawaida " alisema, "lakini hudhani kabisa kwamba litatokea kwako."

Doreen, ambaye alipata mtoto wake Arielle mwaka 2017, aliambiwa tu "jaribu tena" baada ya mimba yake ya kwanza kutoka.
Baada ya mimba yake ya tatu, aliagizwa kwenda kumuona daktari bingwa ili kuchunguzwa kuhusu tatio la mimba zake kuharibika, lakini hakuwahi kubaini ni kwanini amepoteza mimba nyingi
Ni nini kinachoongeza hatari za kutoka kwa mimba?
- Kuwa na umri wa chini ya miaka 20 au zaidi ya 40
- Kuwahi kutoka kwa mimba hapo awali
- Kuwa na uzani mdogo sana au mkubwa sana wa mwili
- Kufanya kazi saa nyingi na zamu za usiku
- Kuwa mweusi
- Uvutaji wa sigara
- Unywaji wa pombe wa kiwango cha juu
Ni usaidizi gani unaweza kupata ?
Utafiti uliochapisha katika Lancet unasema:
- Usaidizi wa kabla ya mimba ili wanawake wawe katika hali bora iwezekanavyo kwa ajili ya mimba
- Uchunguzi wa mapema wa mimba kwana usaidizi kutoka mwanzoni mwa mimba
- Vipimo vya tumbo vya ultrasounds kuangalia muundo wa kizazi
- Matibabu ya homoni
- Sindano za aspirini na heparini ili kupunguza hatari ya kuganda kwa damu
- Wanawake wanaotokwa damu katika kipindi cha mwanzo wa mimba zao wapewe progesterone
- Vipimo na matibabu vitolewe kwa wale wenye tumbo dhaifu la uzazi.
Nyingi kati ya tafiti zilifanyika katika mataifa ya Sweden, Ufini na Denmark, baadhi ya nchi chache ambao zilikusanya takwimu , kupitia data kutoka Marekani, Uingereza, Canada na Norway pia zilitumiwa.
"Tunafahamu kuna ongezeko la hatari ya kufa miongoni mwa wanawake weusi wajawazito' Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Tommy cha kitaifa cha masuala ya uavyaji mimba Profesa Siobhan Quenby, kutoka Chuo kikuu cha Warwick, ambaye alifanya kazi katika utafiti huo alisema.
"Lakini nilishtushwa sana pia kubaini ongezeko la hatari ya kuharibika kwa mimba ."
Wanawake weusi wako katika hatari ya kupata kisukari aina ya 2 na ugonjwa wa moyo - na mangonjwa yote haya yanaongeza hatari ya kuharibika kwa mimba.
Lakini Profesa Quenby alisema kuwa wanasayansi walikuwa wanachunguza pia iwapo hatari za matatizo mengine ya afya, kama vile uvimbe katika kizazi (kama fibroid na kuyumba kwa mfumo wa kinga, vinaweza kuwa sababu ya kiwango hicho kuwa cha juu zaidi miongoni mwa wanawake weusi.
Mabadiliko ya kimaisha
Takribani 75% ya wale ambao mimba zao zinaharibika wataendelea kuwa na mimba zenye afya, jambo ambalo kwa sehemu linawafanya wanandoa kwa kawaida kuendelea kujaribu kupata mtoto bila kufanya uchunguzi zaidi wa afya yao.
Lakini Profesa Quenby - ambaye kwa sasa anaendesha kliniki ya wenye matatizo ya kupoteza mimba alisema: "Kuna mambo tunayoweza kufanya kuzuia kuharibika kwa mimba.
"Sio hali ambayo haileti matumaini ."
Kubadilisha mtindo wa maisha kunaweza kusaidia-na kwa karibu 30% ya watu wanaokwenda katika kliniki yake walikua ni wavutaji wa sigara, walikuwa wana kisukari ambacho hakikudhibitiwa, ukubwa wa mwili kupita kiasi au shinikizo la damu.
"Hiyo inamaanisha huduma za afya zilikosa fursa tatu za kuwaweka katika hali nzuri kwa ajili ya ujauzito kabla ya kubeba mimba ," Profesa Quenby alisema.
'Suala hilo linafaa kushughulikiwa' aliongeza, kwa kutoa :
- Ushauri uliowalenga baada ya mimba ya kwanza kuharibika
- Vipimo vya ziada baada ya kuharibika kwa mimba ya pili
- Uchunguzi zaidi wa kimatibabu baada ya mimba ya tatu kuharibika
'Kujichukia'
Utafiti unaonesha pia kwamba ongezeko kubwa la hatari ya kujiua, msongo wa mawazo na wasiwasi kwa wale ambao wamekumbwa na tatizo la kutoka kwa mimba na unasema athari kwa wenzi wao zinahitrajika kuchunguzwa zaidi.
Baada ya kupoteza mimba nane, Charlotte alikuwa anatarajia mapacha lakini scan ikabaini kuwa pia alikuwa amepoteza ujauzito wake.
"Nilijichukia ," alisema.

"Mume wangu alikuwa akijaribu kunitia moyo na kunifariji.
"Na nilikuwa tu ninapiga mayowe na kuongea maneno yasiyoeleweka.
"Sikutaka kuishi tena ."
Kipindi cha msongo wa mawazo baada ya kiwewe
Awali, Charlotte alipewa tu kijikaratasi.
Ni wakati tu alipoanza kuzungumza kuhusu kujiua ndipo alipopewa usaidizi na, hatimaye akapata matibabu ya msongo wa mawazo baada ya kiwewe.
Baadaye alipata mtoto wa kiume mwenye afya, Ansel, mwaka jana, na sasa anahisi kuwa mwenye uwezo wa kuongea wazi kuhusu aliyoyapitia.
"Ni furaha kubwa kuwa na mtoto wangu wa kiume," alisema.
"Ninafahamu ni kwa jinsi gani nilivyo na bahati kufika pale.
"Sio kila mtu anafikia pale."












