Ligi ya Mabingwa Ulaya: Nyota 10 chipukizi wa kuwatazama msimu huu

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
- Author, Michael Emons
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Desire Doue alikuwa mmoja wa nyota vijana wa msimu uliopita, alipoisaidia Paris St-Germain kushinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza.
Lamine Yamal wa Barcelona, kijana mwingine, aliyekuwa katika timu hiyo wakati wa mashindano hayo.
Ligi ya Mabingwa imerejea - kuna mechi ilichezwa jana Jumanne, zingine zinachezwa leo Jumatano na kesho Alhamisi. Je, ni nyota gani wachanga watavutia katika mashindano ya mwaka huu?
BBC inawatazama vijana 10 ambao wanatarajiwa kufanya vyema msimu huu.
Vasilije Adzic (Juventus)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 19. Nafasi: Kiungo. Raia: Montenegrin.
Kiungo wa kati wa Montenegro, Vasilije Adzic alijiunga na Juventus kwa mkataba wa miaka mitatu mwaka 2024 baada ya kuisaidia Buducnost Podgorica kushinda taji la ligi nchini kwao katika msimu wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 16 tu.
Aliichezea Juve mara tisa mwaka 2024-25, ikijumuisha mechi moja ya Ligi ya Mabingwa, na alicheza katika mechi yao ya kipigo katika Klabu Bingwa ya Dunia dhidi ya Manchester City 26 Juni.
Adzic tayari ameiwakilisha nchi yake, akifunga bao kwenye mechi yake ya kwanza, tarehe 9 Juni, katika sare ya 2-2 dhidi ya Armenia.
Jobe Bellingham (Borussia Dortmund)

Chanzo cha picha, Getty
Umri: 19. Nafasi: Kiungo. Raia: Uingereza.
Kama vile kaka mkubwa Jude alivyofanya, Jobe Bellingham alihama Uingereza na kwenda Borussia Dortmund, akiondoka Sunderland majira ya joto baada ya kuwasaidia kupanda daraja kwenda Ligi Kuu England.
Jobe Bellingham, ambaye aliwagharimu wababe hao wa Ujerumani pauni milioni 27, anacheza kwa kiasi kikubwa kama kiungo mlinzi, ingawa mara kwa mara alicheza kama mshambuliaji wa kati wa Sunderland.
Ameiwakilisha England katika timu ya chini ya miaka 21 na atarejea nchini kwake kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa, pale Dortmund watakapo cheza mechi za ugenini huko Manchester City na Tottenham.
Claudio Echeverri (Bayer Leverkusen)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 19. Nafasi: Kiungo mshambuliaji. Raia: Argentina.
Mashabiki wa Manchester City watakuwa na shauku kubwa ya kuona jinsi Claudio Echeverri atakavyocheza baada ya kwenda kwa mkopo Bayer Leverkusen. City wana chaguo la kumrejesha Muargentina huyo kwenye Uwanja wa Etihad Januari kama wanataka.
Echeverri alijiunga na City kwa mkataba wa pauni milioni 12.5 Januari 2024, lakini akabaki kwa mkopo River Plate kwa miezi 12 iliyofuata. Alianza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya England siku ya mwisho ya msimu wa 2024-25 na kisha akatokea kama mchezaji wa akiba katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA kati ya City dhidi ya Crystal Palace.
Alifunga bao lake la kwanza la City kwa mtindo kwa mkwaju mzuri wa adhabu dhidi ya Al-Ain wakati wa Kombe la Dunia la Klabu msimu wa joto.
Jorrel Hato (Chelsea)

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Umri: 19. Nafasi: Beki. Raia: Uholanzi.
Akiwa na umri wa miaka 19, Jorrel Hato amecheza zaidi ya michezo 120 ya klabu na kucheza katika timu ya wakubwa ya Uholanzi mara sita.
Hato, ambaye anaweza kucheza kama beki wa pembeni au katika safu ya ulinzi ya kati, alicheza mechi yake ya kwanza akiwa na Ajax akiwa na umri wa miaka 16 na kuwa nahodha wa timu hiyo akiwa na umri wa miaka 17 - na kuwa nahodha mdogo zaidi wa Ajax katika mechi ya Ulaya.
Msimu uliopita uchezaji wake ulimfanya kutajwa kuwa mchezaji bora wa chini ya miaka 21 katika ligi kuu ya Eredivisie ya Uholanzi kabla ya kuhamia Chelsea kwa pauni milioni 37 mwezi Agosti.
George Ilenikhena (Monaco)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 19. Nafasi: Mshambuliaji. Raia: Nigeria/Ufaransa.
Kipaji cha mshambuliaji mwenye kasi na nguvu George Ilenikhena kinaendelea kukuwa kwa kasi kubwa.
Alicheza ligi daraja la pili la Ufaransa akiwa na timu ya Amiens, kisha akawa na kiwango kizuri msimu wa 2023-24 huko Royal Antwerp, na kuisaidia timu hiyo kushinda Kombe la Ubelgiji Super Cup mnamo 2023.
Baada ya kupata mabao 14 katika mechi 49 msimu huo, alihamia Monaco. Amefunga dhidi ya Barcelona kwenye Ligi ya Mabingwa katika misimu miwili iliyopita - katika ushindi wa 3-2 wa Antwerp mwezi Desemba 2023 akiwa na umri wa miaka 17, na tena katika ushindi wa 2-1 wa Monaco mwezi Septemba 2024.
Franco Mastantuono (Real Madrid)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 18. Nafasi: Kiungo. Raia: Argentina.
Mshambuliaji wa Real Madrid, Franco Mastantuono anachukuliwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotarajiwa kung'ara katika soka duniani.
Tarehe 13 Juni, Real ilitangaza kwamba Mastantuono atajiunga na klabu hiyo katika siku yake ya kuzaliwa ya 18, 14 Agosti, akisaini mkataba wa miaka sita baada ya kukubali kulipa pauni milioni 39 (euro 45m) ili kumnunua kutoka River Plate.
Alianza mechi yake ya kwanza ya kimataifa akiwa na Argentina akiwa na umri wa miaka 17 mwezi Juni na amecheza mechi tatu akiwa na Real katika La Liga hadi sasa 2025-26.
Senny Mayulu (Paris St-Germain)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 19. Nafasi: Kiungo. Raia: Ufaransa.
Akiwa na umri wa miaka 19, Senny Mayulu ana mataji mawili ya Ligue 1 ya Ufaransa. Alifunga katika ushindi wa fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Paris St-Germain na kucheza fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Alianza kucheza PSG kwa mara ya kwanza 2024 na ameiwakilisha Ufaransa katika timu ya chini ya miaka 20.
Kiungo Mayulu kwa kiasi kikubwa amekuwa akicheza kutokea benchi, lakini amezidisha kiwango chake akitokea benchi na kuifungia klabu hiyo bao la tano katika ushindi wao wa 5-0 dhidi ya Inter Milan kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mwezi Mei.
Rio Ngumoha (Liverpool)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 17. Nafasi: Kiungo mshambuliaji. Raia: Uingereza.
Rio Ngumoha alikuwa katika akademi ya Chelsea kabla ya kuhamia Liverpool mwaka 2024 na alikuwa na umri wa miaka 16 alipocheza kwa mara ya kwanza akiwa na Reds, katika ushindi wa 4-0 wa Kombe la FA raundi ya tatu dhidi ya Accrington Januari 2025.
Ana kasi na ustadi, Ngumoha alifunga mabao katika mechi za kujiandaa na msimu huu dhidi ya Yokohama na Athletic Club.
Kisha akajihakikishia nafasi katika vitabu mwezi Agosti kwa kuwa mfungaji wao mdogo zaidi kwenye Ligi ya England na mfungaji katika ushindi wa kusisimua wa 3-2 dhidi ya Newcastle - akiweka bao siku nne kabla ya siku yake ya kuzaliwa kutimiza miaka 17.
Ethan Nwaneri (Arsenal)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 18. Nafasi: Kiungo mshambuliaji. Raia: Uigereza.
Baada ya kutoka katika akademi ya Arsenal, Ethan Nwaneri, akiwa na umri wa miaka 15, alikua mchezaji mdogo zaidi katika ligi kuu ya England alipocheza dhidi ya Brentford Septemba 2022.
Alianza katika mechi 16 za mashindano yote kwa Arsenal ya 2024-25, na mechi nyingine 21 akitokea benchi, huku akifunga mabao tisa, yakiwemo mawili kwenye Ligi ya Mabingwa.
Uchezaji wake ulimfanya ateuliwe kuwania tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa PFA na wakati wa majira ya joto aliisaidia England kushinda Ubingwa wa Ulaya wa Vijana chini ya miaka 21.
Geovany Quenda (Sporting)

Chanzo cha picha, Getty Images
Umri: 18. Nafasi: Winga/beki wa pembeni. Raia: Ureno.
Mashabiki wa Chelsea watakuwa wakimtazama Geovany Quenda katika msimu huu, kwani winga huyo raia wa Ureno atajiunga na The Blues msimu ujao wa joto kwa ada ya pauni milioni 44.
Alicheza akiwa na Sporting ilipochukua ubingwa wa ligi kuu ya nchi hiyo mwaka 2024-25, na kuhamia kwake Chelsea kulitangazwa mwezi Machi.
Baadaye Quenda alionyesha kiwango kizuri kwenye michuano ya Ulaya ya Vijana chini ya miaka 21, akiifungia Ureno mabao matatu.















