Wanaigeria wanaoingia kwenye mtego na kulaghaiwa kwa kuwa wapenzi wa jinsia moja
Na Ian Wafula & Tamasin Ford
BBC Africa Eye

Wakati Nigeria ilipopitisha sheria kali zaidi barani Afrika dhidi ya mapenzi ya jinsia moja, intaneti ilibadilika kuwa mahala pa wapenzi wa jinsia moja na watu wa jamii ya LGBT kwa ujumla pa kuwasiliana na wenzao kwa usalama zaidi – hadi magenge ya wahalifu yakaingia katika njia hiyo ya mawasiliano ya kidigitali pia. BBC Africa Eye inachunguza apu maarifu za kutafuta wapenzi zinavyowalaghai, na badala yake kuwapora, kuwapiga na hata kuwateka watu.
Onyo: Makala hii ina maelezo kuhusu kujiua...
Kuishi maisha ya usiri kama mwanaume mpenzi wa jinsia moja nchini Nigeria lilikuwa ni jambo hati kwa Mohammed.
Alikuwa mara kwa mara muangalifu wakati alipopanga kwenda kumuona mtu fulani – lakini mpango mmoja uliharibu maisha yake kabisa.
Baba huyu wa watoto watatu alikutana na Jamal mtandaoni. Walikuwa wamezungumza kwa muda wakati hatimaye alipoamua kukutana naye ana kwa ana. Anasema alikuwa amempenda, na hata kumuamini, na kwahiyo mchana mmoja alikutana na Jamal mjini na akarejea nyumbani. Lakini ulikuwa ni mtego.
Siku moja Mohammed alikuwa anaoga lakini alipokuwa amevua nguo, mara kikundi cha wanaume walimvamia na kuanza kumpiga na kudai awape pesa.
Jamal na genge la wanaume hao walitengeneza video yake, akiwa uchi, akiwaomba wamuache aende.
"Sikuamuni kuwa mtu niliyemuamini kiasi kile angenifanyia jambo hilo."
Wakati video ilipokwenda mtandaoni, Mohammed anasema maisha yake yaliharibika.
Alikuwa ametunza maisha yake ya kimapenzi – kwa siri kubwa mwenyewe – kwani kwa maisha yaliyoonekana nje na watu alikuwa ni mwanume aliyeoa ambaye anaitunza familia yake.
'Mwanangu wa kiume aliniokoa'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akizungumza huku akiwa amejifyunika kwa kofia ya sweta yake na barakoa ili kuuficha utambulisho wake, alikubali kuzungumza na BBC ili mradi apewa hakikisho kwamba hatatambulika.
"Nilikuwa ninalia. Nilitaka kujiua."
Alielezea wakati alipompigia simu watoto wake wa kiume waje amuokoe kama na kifo.
"Niliwapigia simu wanangu wa kiume, wote watatu.Kijana wangu aliniambia anampenda baba yake hata kama ni mpenzi wa jinsia moja, hana tatizo na hilo.
"Alinipa sababu ya nikwanini sipaswi [kujiua].
Muhammed aliangua kilio, alipokuwa akielezea haya, huku akijifunika kwa kofia ya sweta lake. Alisimama akajifunika uso wake na sweta lake, kisha akaanza kulia. Akionyesha kuumizwa na kile kilichomtokea.
Kulingana na wanaharakati wanaofanya kazi na wapenzi wa jinsia moja -LGBT nchini Nigeria, karibu watu 15 hadi 20 huwasiliana nao kila wiki wakiwa na hadithi sawa na za Mohammed.
Aina hii ya ulaghai, ambap mtu wa LGBT anajipata katika mtego, inafahamika miongoni mwa wapenzi wa jinsia moja kama "kito" – asili halisi ya jina hilo haiku wazi. BBC Africa Eye iiliwahoji watu 21 kuhusu uzoefu wao wa kuwa "kito'd".

Emmanuel, ambaye sio jina lake halisi , alielezea jinsi alivyoanza kuwa na mawasiliano na rafiki yake wa mtandaoni, lakini hakufahamu kuwa makaunti ya rafiki yake ilikuwa imetekwa. Wakati alipopanga kukutana naye, alijipata katika mtego wa genge la watu wanaume wapatao watano.
"Walitengeneza video yangu, na walikuwa wanauliza maswali ya ajabu. Walisema: 'Ulisomea shule inaitwaje? Unatoka wapi? Nilifahamu kuwa wataitumia video kunidhalilisha. Kwahiyo niliwapatia taarifa zisizo sahihi ."
Genge hilo halikuituma video yake mtendaoni, lakini lilimlazimisha atoe naira 500,000($1,000; au £860) kutoka kwenye akaunti zake za benki na wakamtesa kwa kwa chuma.
Alinyoosha mkono wake kuonyesha kovu ambalo limebaki katika kidole gumba chake alilopata kutokana na shambulio hilo. Baada ya kuwapatia pesa zake, genge lilimuacha akaondoka.
"IIliniumiza kiakili. Simuamini yeyote. Ninahisi siko salama."
Mnamo mwaka 2014, (Zuwio) la ndoa ya wapenzi wa jinsia moja , lilikuwa sheria nchini Nigeria, na hukumu mpya ya kifungo cha jela cha miaka 14 ilianzishwa kwa yeyote atakayepatkana katika mkataba wa ndoa ya jinsia moja au kuishi na mtu wa jinsia moja kimapenzi.
Pia ni hatia ya uhalifu kuonyesha hadharani mapenzi baina ya watu wa jinsia moja , kosa linaloweza kupelekea mhusika kuhukumiwa kifungo cha miaka 10.
Ilipiga marufuku klabu za wapenzi wa jinsia moja, na kuanzisha hukumu ya kifungo cha miaka 10 kwa yeyote anayesajiri, kuendesha, au kushiriki katika klabu za wapenzi wa jinsia moja, mashirika au makampuni, wakiwemo wale wanaounga mkono makundi hayo.
Kupitishwa kwa sheria kulingwa mkono na wengi nchini Nigeria, na hilo lilimaanisha kuwa Nigeria ndio nchi yenye sheria kali zaidi dhidi ya mapenzi ya jinsia moja barani Afrika, kulingana na utafiti.
Majimbo 12 ya kaskazini tayari yanaweza kuwahukumu kifo watu chini ya sheria ya Kiislamu, Sharia, kwa kujihusisha na vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Sheria mpya , kulingana na ripoti ya Human Rights Watch "rasmi inaidhinisha unyanyasaji dhidi ya watu wa jamii inayoshiriki mapenzi ya jinsia moja- LGBT , na kuwaweka katika hali mbaya zaidi".
Mwaka 2014, vyombo vya habari viliripoti ghasia, kuvamiwa na makundi na kudhalilishwa kwa wapenzi wa jinsia moja vilikuwa ni vitendo vya kawaida, na tangu wakati huo unyanyasaji huo umegeuka kuwa visa vya kito.

Mtengenezaji wa filamu Uyaiedu Ikpe-Etim, ambaye ameyaweka wazi maisa yake ya kuwa mpenzi wa jinsia moja kama mwanamke anayeshiriki mapenzi hayo nchini nigeria, anasema kulaghaiwa dhidi ya LGBT ni jambo "lililoshamiri".
"Kila siku kuna taarifa kwenye intaneti. Wakati mwingine tuna taarifa ambapo mtu ameteswa hadi kufa.
"Na ni jinsi Wanigeria wengine wanavyolichukulia. 'Oh ni vizuri sana, vizuri, wamewauwa. Hawapaswi kuruhusiwa kujitokeza .' Na hakuna haki."
Bi Etim alisema kuwa jambo linalofanya hata kuwa gumu zaidi ni kwamba waathiriwa wanahisi hawawezi Kwenda kwa polisi kutokana na hofu ya kukamatwa au hata kushambuliwa,
"Inasikitisha tu, unajua."
Alisema wapenzi wa jinsia moja, ambao walilazimishwa kuondoka mtandaoni, wanalazimika pia kuwa waangalifu sana.
"Hatuna haki ya kutembea mtaani bila wasiwasi sawa wale waliopo katika ndoa za mume na mke au Kwenda kwenye migahawa: 'Ninaweza kupata namba yako?'"
Hatahivyo, baadhi ya maafisa wa usalma wanashirikiana na wanaharakati kusitisha ulaghai.
BBC Africa Eye ilizungumza na afisa katika kikosi cha usalam na ulinzi nchini Nigeria (NSCDC). Anafanya kazi pamoja na timu ya wanaharakati wanajifanya kuwa watu wa LGBT wanaowatafuta wapenzi. Lengo ni kuwasaka walaghai.
"Kwangu mimi, hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria nchini. Ulaghai ni kosa baya sana. Ni uhalifu mkubwa ," alisema, akizungumza na BBC , bila kutaka jina lake litambulike.
"Kama mtu yeyote ataleta kesi mbele yangu kuhusu kisa chochote cha ulaghai wa mpenzi wa jinsia moja, nitamuwinda. Bila shaka."
Waathiriwa huwasiliana na wanaharakati wakiwa na majina ya walaghai na picha zao. Wanaharakati hutuma taarifa kwa NSCDC, ambao huanza mchakato wa kuwasaka na kuwakamata wahalifu.
"Kokote walipo, ninataka kuwambia hakuna mahala pa kujificha kwa walaghai katika Nigeria."
Tatizo wanalokabiliana nalo ni kuwashawishi waathiriwa kutoa ushuhuda mahakamani. Katika nchi ambapo mapenzi ya jinsia moja yanaweza kukupeleka jela, watu wachache ndio wanaweza kusimama na kuwa wakweli kuhusu jinsia hali yao ya kimapenzi.
Inamaanisha ni nadra kwa walaghai kushitakiwa.
Wengi wa watu waliohojiwa na BBC Africa Eye walikuwa wamepoteza kazi tangu video zao za ulaghai zilipotumwa mtandaoni. Baadhi walikuwa wamehamishwa kutoka kwenye nyumba zao, wengine walitengwa na familia zao. Wote walikuwa wanahangaika na matatizo ya afya ya akili.
Kwa Mohammed, ambaye hata alifikiria kuhusu kujitoa uhai, bado anakabiliwa na aibu kwani video yake ya utupu imeendelea kusalia mtandaoni.
"Ninafahamu bado wanaitazama video ," alisema.
















