Kwanini ni vigumu kutekeleza marufuku dhidi ya michango ya Harambee Kenya?

Chanzo cha picha, IKULU KENYA
- Author, Na Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Gumzo la Harambee limeibuka tena nchini Kenya katika siku za hivi karibuni kufuatia agizo la Rais William Ruto kuwapiga marufuku watumishi wa serikali kujihusisha na shughuli za kutoa michango hiyo ya kijamii.
Hii sio mara ya kwanza agizo kama hilo kutolewa kwani hata watangulizi wa Rais Ruto pia waliweka mikakati ya kuhakikisha Harambee haitatumiwa kuendeleza maovu katika jamii ikiwa ni pamoja na ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma lakini changamoto imekuwa utekelezaji.
Rais Ruto mwenyewe alijikwaa ulimi hivi karibuni alipojitolea kufadhili ujenzi wa kanisa moja huko Nyandarua katika eneo la Kati mwa Kenya siku kadhaa baada ya kutoa agizo lake la kupiga marufuku Harambee.
''Nimeona mumejitahidi sana na ujenzi wa kanisa lenu, sasa pale palipobakia niachieni. Naomba Gachagua(Naibu wa Rais) na mchugaji wakae pamoja wapige hesabu halafu mimi nitaandika cheki (hundi),'' Bw Ruto alisema.
Baadaye msemaji wa Serikali ya Kenya Isaac Mwaura alijaribu kurekebisha dosari hiyo lakini ilikuwa vigumu. Alipoulizwa kuhusiana na msimamo huo wa Ruto katika kikao na wandishi wa habari alisema: ''Wachana na hayo mambo.''
Katika makala hii tutaangazia chimbuko la Harambee nchini Kenya na jinsi michango hiyo ya kijamii ilivyoingizwa siasa, kutumiwa kama mbinu ya kuendeleza ufisadi na utakatishaji fedha.
Harambee ni nini?
Michango ya kijamii maarufu Harambee imekuwa utamaduni wa muda mrefu wa Wakenya, ambao umejikita katika maadili ya nchi.
Neno Harambee linamaanisha "kuja pamoja" na linaashiria kuweka mbele maslahi ya watu kwa pamoja badala ya kuzingatia maslahi ya mtu binafsi.
Kwa Wakenya, Harambee ni mchango usio rasmi ambao hutolewa kwa ukarimu bila kujali tabaka, kabila, jinsia au dini ili kumsaidia yeyote anayehitaji.

Chanzo cha picha, Ludovic Marin/Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Profesa Hezron Mogambi, Mchambuzi wa siasa za Kenya na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anasema neno Harambee liliibuka mara ya kwanza nchini wakati wafanyakazi Waswahili walipohitaji kuungana ili kuinua kitu kizito.
Kila wakati mmoja wao aliposema kwa sauti neno “Harambee!”, wafanyakazi wangenyanyua kitu hicho pamoja kwa wakati mmoja.
Kulingana na ngano za Kenya, neno Harambee lilitokana na wahamiaji 30,000 wa Kihindi waliotua mjini Mombasa katika Pwani ya Kenya miaka ya 1890 kusaidia kujenga reli ya Kenya-Uganda kwa amri ya Uingereza.
Walipokuwa wakifanya kazi wafanyakazi wa Kihindi waliomba kwa kutumia maneno mawili. Kwanza Hare, kumaanisha uwezo wa Mungu usio na kifani, na pili Ambe, kumuelekea mungu wa kike mwenye nguvu ya kutoshindwa.
''Wakenya ambao walifanya kazi na wajenzi hao wa Kihindi, waliwasikia wakitamka kwa sauti maneno "Hare" na "Ambe", kwa kuwa hawakuweza kuyatenganisha wao wakaamua kusema ''Harambe'' na hapo ndipo maneno hayo yakageuka kuwa wito wa kipekee wa Kenya wa kuungana.'', anasema Mogambi.
Neno hili lilipata umaarufu wa kitaifa mnamo Mei 1963 wakati rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, alipotamka wakati wa hotuba yake ya ushindi siku ya uchaguzi.
Kenya ndio mwanzo tu imepata uhuru kutoka kwa Waingereza na Wakenya walikuwa na shauku ya kuungana kama nchi ili kujenga taifa jipya, baada ya ukoloni na kuanza safari ya kujitawala.

Chanzo cha picha, Buena Vista Images/Getty Images
Siasa zilivyoingizwa katika michango ya Harambee
Rais wa pili wa Kenya Daniel Arap Moi alipoingia madarakani alifuata nyayo ya rais mtangulizi Jomo Kenyatta. Ili kuimarasha utendakazi Moi alihakikisha Ripoti ya Tume ya Ndegwa ya 1972 inatekelezwa kikamilifu, na hivyo kuwazuia watumishi wa umma kujihusisha na biashara za kibinafsi wakati wanashikilia nyadhifa serikalini.
Uongozi wa Moi uliendelea vyema hasa baada ya kuponea jaribio la mapinduzi ya 1982.
Kiongozi huyo alijihusisha zaidi na ujenzi wa taifa kupitia michango hiyo ya kijamii. Lakini kufikia miaka ya 1990, Harambee ilikuwa imegeuzwa kuwa silaha ya mapamambo ya kisiasa .
Mnamo Januari 2002, serikali ya Rais mstaafu Moi iliagiza kampuni ya Uingereza, Risk Advisory Group Ltd, kufanya tathmini ya maendeleo ya Kenya katika vita dhidi ya ufisadi.
Shirika hilo katika ripoti yake ya kurasa 61 lilipendekeza kuwa Hharambee au 'moyo wa kuvuta pamoja' ikomeshwe, kwa sababu ilikuwa chanzo cha hongo na ulafi. miomgoni mwa maafisa wa serikali.
"Inatumiwa isivyofaa kwa manufaa ya kisiasa na wapiga kura na wale wanaotafuta nafasi za kuchaguliwa"
Katika muhula wake wa uongozi, rais wa tatu Mwai Kibaki alikabiliwa na kibarua kigumu kudhibiti michango hiyo ya kijamii kwani viongozi waliendelea kutumia mbinu hiyo kujileta karibu na wananchi.
Kupitia Sheria ya Maadili ya Maafisa wa Umma iliyotungwa mwaka wa 2003, Wabunge na Mawaziri walipigwa marufuku kusimamia michango ya Harambee. Wakati huo ilisemekana kuwa katika baadhi ya visa, wanasiasa walielekeza pesa zilizokusanywa katika mikutano ya kuchangisha pesa kufadhili kampeni zao.
Hata hivyo, walipuuza sheria na kuendelea, kutumia mbinu hiyo kwa kukiuka masharti yake. Kulingana na ripoti za vyombo vya habari nchini Kenya, baadhi ya wabunge na mawaziri walikuwa na marafiki au jamaa zao walioorodheshwa kama wageni wakuu. Walijitokeza baadaye kuchangia kiasi kikubwa cha fedha .
"Kwa njia hiyo, waliweza kutii sheria husika, wakati kiuhalisia bado wanatumia michango hiyo kujizolea umaarufu," gazeti moja liliripoti.
Doa la ufisadi lachafua 'nia njema Harambee'
Kwa miaka mingi Harambee imewezesha jamii kuchangisha fedha kwa maendeleo ya mtu binafsi au jamii.
Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, Harambee imekuwa chombo cha matumizi ya kipekee na watu wachache walio na ushawishi wa hali ya juu.
Wanasiasa waliotumia nyadhifa zao kujilimbikizia mali kwa njia za kiufisadi wamekuwa wakishirikiana na wandani wao kuelekeza fedha hizo katika ''miradi ya kijamii'' kama njia ya kukwepa mitego ya sheria zilizopo za kukabiliana na ufisadi.
Licha ya kamati na tume mbali mbali kuwahi kubuniwa nchini Kenya kama njia moja wapo ya kupambana na ufisadi , tatizo hilo limesalia kuwa jipu kubwa.
Suala la ufisadi limeendelea kutawala siasa za Kenya na kila kiongozi anayeingia madarakani amepata ugumu wa kulimaliza jinamizi hilo
.Rais wa wa sasa William Ruto anapendekeza katiba ifanyiwe marekebisho ili kuimarisha sheria ya kukabiliana na ufisadi.
Kupigwa marufuku kwa Harambee sio suluhisho wataalamu wa masuala ya kijamii wanasema.
Kufanya hivyo kutarudisha nyuma hatua zilizopigwa tangu zamani kwa sababu watu wengi bado wanategemea wahisani kufanikisha mambo muhimu kwa jamii kama vile kufadhili masomo ,huduma za afya na ujenzi wa mkundo msingi ya umma .
Iwapo hakutakuwa na ari kamili ya kisiasa kumaliza ufisadi,Harambee zingali zitatumiwa kwa manufaa ya viongozi wenye ushawisho kuendeleza maovu ya kifedha kutumia mpango huo uliokuwa na dhamira nzuri ya kusaidia maeneo ya jamii.
Imehaririwa na Yusuf Jumah












