Vita saba kati ya Israel na wapiganaji wa Gaza tangu 2006

c

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wapiganaji wa Palestina walimteka mwanajeshi wa Israel, Gilad Shalit na kumpeleka Ukanda wa Gaza 2006

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amepigana vita vitano na makundi yenye silaha katika Ukanda wa Gaza, kati ya vita saba tangu Israel ilipotangaza kujiondoa katika Ukanda huo mwaka 2005 - Hamas ikashika hatamu kuanzia 2006.

Netanyahu, alichukua wadhifa huo kwa mara ya kwanza 1996 akiwa Waziri Mkuu mwenye umri mdogo zaidi tangu kuanzishwa kwa Israel, na hivi vya sasa ni vita vyake vya tano katika Ukanda wa Gaza.

Operesheni ya Summer Rains - 2006

fdcv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Israel, Gilad Shalit (katika picha) aliachiliwa kwa mabadilishano na wafungwa 1,027 wa Kipalestina kutoka magereza ya Israel

2006 wapiganaji wa Kipalestina walimkamata mwanajeshi wa Israeli, Gilad Shalit wakati wa shambulio la Juni 25 na kumpeleka Gaza.

Siku mbili baadaye, jeshi la Israel lilianzisha operesheni ya kijeshi iitwayo "Summer Rains," ilianza kwa mashambulizi makubwa ya makombora na kufuatiwa na uvamizi wa ardhini katika Ukanda wa huo.

Shambulio hili lilikuja miezi kumi tu baada ya Israel kuondoa vikosi vya kijeshi na walowezi kutoka Ukanda wa Gaza.

Operesheni ya kijeshi, ilikuwa na lengo la kumkomboa kumwanajeshi huyo, kusitisha urushaji wa makombora kuelekea kusini mwa Israel na kufichua mtandao wa mahandaki yanayotumiwa na makundi ya wapiganaji wa Palestina.

Israel na wapiganaji wa Gaza walifikia makubaliano ya kusitisha mapigano Novemba 26, 2006, ingawa Israel ilishindwa kubaini ni wapi Shalit alikuwa anashikiliwa.

Aliachiliwa huru baada ya mazungumzo magumu ya zaidi ya miaka mitano, Oktoba 18, 2011, ambayo pia yalisababisha kuachiliwa kwa Wapalestina 1,027 kutoka magereza ya Israel.

Yalijumuisha kuachiliwa kwa Yahya Sinwar, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, ambaye Israel kwa sasa inamtuhumu kupanga mashambulizi ya Oktoba 7, pamoja na Mohammed al-Deif kamanda wa kijeshi wa Hamas.

Operesheni ya Cast Lead 2008 - 2009

cv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wapiganaji wa Palestina hurusha mamia ya makombora kwenda kusini mwa Israel

Wakati wa Urais wa Ehud Olmert, asubuhi ya Disemba 27, 2008, vikosi vya Israel vilianza Operesheni "Cast Lead" kwenye Ukanda wa Gaza, na wapiganaji wa Palestina walijibu mashambulizi kwa operesheni iliyoitwa "The Battle of Al-Furqan."

Lengo la opereseheni hii ilikuwa ni kukomesha mashambulizi ya makombora yaliyolenga Israel. Mapigano yaliendelea hadi Januari 18, 2009, Israel na Hamas zilipotangaza kusitisha mapigano.

Idadi ya wahanga wa Palestina ilizidi 1,400, wakiwemo watoto wapatao 300, na maelfu walijeruhiwa. Maeneo ya Ukanda wa Gaza yaliharibiwa na maelfu walikimbia makazi yao.

Raia wa kusini mwa Israel pia walikabiliwa na mashambulizi ya kila siku ya roketi kutoka kwa makundi ya wa Palestina na kusababisha raia watatu kuuawa na wengine kujeruhiwa, na wanajeshi sita wa Israel waliuawa.

Vita vya Pillar of Defense - 2012

fdcv

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Jeshi la Israel lilishambulia karibu maeneo 1,500 katika vita vya 2012

Novemba 14, 2012, jeshi la Israeli lilimlenga Ahmed Al-Jaabari, kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas, na Muhammad Al-Hams, mwanachama wa Brigedi ya Al-Qassam, katika shambulizi la gari walilokuwa wakisafiria katika mtaa wa Omar Al-Mukhtar katika Jiji la Gaza.

Gazeti la Israel la Haaretz liliripoti Al-Jaabari alikuwa akijadiliana kuhusu mapatano ya kudumu na Israel saa chache kabla ya kuuawa.

Israel iliita operesheni hiyo "Pillar of Defense," na Hamas iliita operesheni yake "Shale Stones." Mwishoni mwa vita, jeshi la Israel lilikuwa limepiga takriban shabaha 1,500, huku vuguvugu la upinzani la Wapalestina lilifyatua takriban makombora 1,500, ambapo Israel inasema mfumo wa Iron Dome ulinasa 420 kati yao.

Kwa jumla, Wapalestina 165 waliuawa wakiwemo watoto 42. Wengine 1,220 walijeruhiwa, wakiwemo watoto 430. Raia 4 wa Israel na wanajeshi 2 waliuawa, na 240 walijeruhiwa. Usitishaji mapigano ulifikiwa jioni ya tarehe 21 Novemba.

Operesheni ya Protective Edge - 2014

fdvc

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Athari ya mashambulizi ya Israel huko Gaza 2012

Operesheni hii ilikuja kutokana na uamuzi wa Baraza la Usalama la Israel, linaloongozwa na Benjamin Netanyahu, kufanya shambulio kwenye Ukanda wa Gaza. Lengo ni kuzuia urushwaji wa makombora dhidi ya Israel na kuzuia mashambulio zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu iliyochapishwa tarehe 3 Oktoba, idadi ya Wapalestina waliouawa ni 2,189.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa asilimia 70 ya watoto 513 waliouawa walikuwa chini ya umri wa miaka 12. Na idadi ya waliojeruhiwa ilifikia Wapalestina 11,100, wakiwemo watoto 3,374.

Makumi ya Waisraeli walijeruhiwa kwa makombora na kiwango cha uharibifu huko Gaza ilikuwa ni nyumba 113,000, kulingana na maafisa wa Ukanda huo.

Vita vya 2019

fdvc

Chanzo cha picha, EPA

Asubuhi ya Novemba 12, 2019, mlipuko mkubwa ulitikisa kitongoji cha Shuja'iya huko Gaza, baada ya hapo ikatangazwa kiongozi wa harakati ya Jihad ya Kiislamu ya Palestina, Bahaa Abu Al-Atta, ameuawa.

Harakati ya Islamic Jihad ilijibu kwa kuanzisha vita - mamia ya maroketi yalirushwa katika maeneo ya Israel. Israel haikupata hasara ya kibinadamu wala mali.

Lakini mashambulio ya anga ya Israel yalisababisha kuuawa kwa Wapalestina 34 na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa, wakiwemo wapiganaji wa Brigedi za Al-Quds, pamoja na idadi kubwa ya raia.

Vita vya 2021

fdvc

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Israel ilizuia watu kuinga katika msikiti wa Al-Aqsa Mosque mwezi Mei 2019
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Aprili 2021, wakaazi wa kitongoji cha Sheikh Jarrah huko Jerusalem Mashariki walianza kuandamana kupinga kile wanachosema ni "mipango" ya kuwafurusha Wapalestina katika kitongoji hicho.

Mvutano na walowezi uliongezeka na baadhi yao walijaribu kuteka mali za baadhi ya familia za Wapalestina. Jerusalem inayokaliwa kwa mabavu ilishuhudia maandamano ya kila siku na mapigano kati ya Wapalestina, walowezi na vikosi vya usalama vya Israel.

Makabiliano hayo yalisababisha wengi kujeruhiwa na wengine kukamatwa, na Mei 7, Israel ilizuia watu kwenda katika Msikiti wa Al-Aqsa na kuwatawanya waumini kwa nguvu.

Tarehe 10 mwezi huo huo vikosi vya usalama vya Israel vilivamia Msikiti wa Al-Aqsa na kuwajeruhi waandishi wa habari, wahudumu wa afya na raia wengine, idadi ya waliojeruhiwa ilifikia Wapalestina 300.

Vikosi vya Al-Qassam vilirusha makombora kuelekea Israel, na Israel ikajibu kwa mashambulizi makali huko Gaza. Baada ya siku 11 za mapigano, pande hizo mbili zilikubaliana kusitisha mapigano.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za maafisa wa Ukanda wa Gaza, idadi ya vifo vya Wapalestina ni 243, wakiwemo watoto 66, wanawake 39 na wazee 17, huku 1,910 wakijeruhiwa.

Mashambulizi hayo pia yalisababisha zaidi ya Wapalestina 75,000 kuyahama makaazi yao, 28,700 kati yao wakikimbilia katika shule zenye uhusiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kusaidia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Kwa upande wa Israel, idadi ya waliouawa ni 12 na waliojeruhiwa 335. Makombora 4,300 yalirushwa dhidi ya Israel, lakini Iron Dome ilinasa asilimia 90, na jeshi la Israeli lilishambulia zaidi ya maeneo 1,700 huko Gaza.

Operationi ya Breaking Dawn - 2022

fdvc

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Wakaazi wa kitongoji cha Sheikh Jarrah, Mashariki mwa Jerusalem wakipambana na vikosi vya Israel katika maandamano

Siku ya Ijumaa, Agosti 5, 2022, Israel ilimuua kamanda wa Brigedi za Al-Quds, kitengo cha kijeshi cha harakati ya Islamic Jihad katika Ukanda wa Gaza, na alilengwa ndani ya nyumba katika kitongoji cha Al-Rimal, kwa ndege isiyo na rubani.

Israel iliita operesheni hii Breaking Dawn. Kundi la Islamic Jihad lilijibu kwa operesheni iliyoitwa Unity of the Squares, na kurusha mamia ya maroketi katika miji ya Israel.

Kundi hilo lilisema katika taarifa yake kwamba operesheni hii ni ushirikiano kati ya Brigedi za Al-Quds, Brigedi ya National Resistance, Mujahideen, na Al-Aqsa Martyrs - ambayo ni tawi la kijeshi la harakati ya Fatah.

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza iliripoti idadi ya waliopoteza maisha katika vita hivi ni watu 24, ikiwa ni pamoja na watoto sita. Watu 203 walijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Israel.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah