Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mzozo wa DRC unavyotia majaribuni mahusiano ya kidiplomasia ya China
- Author, Jack Lau
- Nafasi, Global China Unit, BBC World Service
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Juhudi za China za kujenga maslahi makubwa ya kibiashara barani Afrika zimeambatana na sera makini ya kudumisha hali ya kutoegemea upande wowote, lakini mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umesababisha mabadiliko ya uelekeo.
Rwanda imekuwa ikilaumiwa vikali kwa kuchochea mapigano katika eneo hilo lenye utajiri wa madini na Beijing, ambayo ina uhusiano wa karibu na DR Congo na Rwanda, katika wiki za hivi karibuni imejiunga na ukosoaji huo.
Lakini inajaribu kudumisha mahusiano mazuri ya kidiplomasia na nchi zote mbili, wakati pia ikiendelea kufanya biashara zake na kununua madini muhimu.
Je, mwitikio wa China kwa mzozo huu ni tofauti kivipi?
Kwa miongo kadhaa, China imekuwa makini kutoshiriki katika mizozo barani Afrika, ili kuepuka kusababisha matatizo ambayo yanaweza kuingilia maslahi yake makubwa ya kibiashara.
Hadi sasa imejiepusha na kukosoa serikali za Afrika kwa kuunga mkono washiriki katika mzozo.
Kwa mfano, China haijazungumza kuhusu msururu wa mapinduzi tangu mwaka 2020 katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi, isipokuwa kuwataka viongozi kuzingatia maslahi ya wananchi.
Beijing kwa muda mrefu imekuwa ikifuata sera ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, anasema Prof Zhou Yuyuan, ambaye ni mtaalamu wa maendeleo na usalama wa Afrika katika Taasisi za Mafunzo ya Kimataifa ya Shanghai (SIIS).
Kwa hivyo inaepuka kupendekeza suluhu za mizozo, mbali na kutoa wito wa juhudi za kidiplomasia au kisiasa na mashirika ya kimataifa kama vile UN au Umoja wa Afrika.
Machafuko yaliyohusisha waasi wa M23 wanaounga mkono Rwanda mashariki mwa DR Congo yaliibuka tena mwaka 2021. Wapiganaji hao wanaongozwa na Watutsi wa kabila ambao wanasema walichukua silaha kulinda haki za kundi la walio wachache , na kwa sababu mamlaka ya Congo ilikataa makubaliano ya awali ya amani.
Katika maoni yake ya mapema kuhusu haya, China ilijiwekea kikomo kwa kukosoa "majeshi ya kigeni" ambayo hayakutajwa kwa kutoa msaada kwa wapiganaji wa M23.
Lakini katika wiki chache zilizopita imeachana na mazoea yake ya kawaida na kuitaja Rwanda kwa jina.
Hii inafuatia mafanikio makubwa ya M23, ambayo tangu Januari imeteka miji muhimu ya Goma na Bukavu.
"China inasisitiza matumaini yake kwamba Rwanda itasimamisha msaada wake wa kijeshi kwa M23 na kuondoa mara moja vikosi vyake vyote vya kijeshi katika eneo la DRC," balozi wa China wa Umoja wa Mataifa alisema mwezi Februari.
Prof Zhou anabainisha kuwa ingawa ni muhimu, "maneno kwa ujumla bado hayatoshi".
"China 'ilitumai' kuwa Rwanda ingesimamisha uungwaji mkono wake lakini haikulaani," anasema.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye China iliunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linatoa wito kwa Wanajeshi wa Ulinzi wa Rwanda "kusitisha msaada kwa M23 na kuondoka mara moja kutoka kwenye ardhi ya DRC bila masharti".
Kwa nini China imefanya mabadiliko haya?
Kulingana na Prof Zhou, kauli za China huenda zilichochewa na ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa, ambazo zimetoa ushahidi wa kutosha wa Rwanda kuunga mkono kundi la M23.
"Haya ni makubaliano ya kimsingi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa," aliongeza.
"Tatizo limekuwa likiendelea kwa muda mrefu vya kutosha, na kila mtu anajua katika mioyo yao hali ilivyo kimsingi. Hakuna haja ya kunyamaa kimya tena."
Si ujumbe wa China katika Umoja wa Mataifa wala ubalozi wake mjini London uliojibu kwa nini China iliikosoa Rwanda.
Lakini umuhimu mkubwa kwa China wa utajiri wa madini maarufu wa DR Congo unaweza kuwa sababu.
Mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yamekithiri katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, maeneo yenye migodi mingi ya dhahabu inayomilikiwa na Wachina.
Jinsi migodi hii ilivyoathiriwa na mapigano hadi sasa haijulikani.
M23 pia imekamata eneo lenye migodi ya madini ya coltan, ambayo China inaagiza kwa wingi kutoka nje.
Tantalum ya chuma, inayotumika katika magari na vifaa vya elektroniki vya kila siku kutoka kwenye runinga hadi simu za mkononi, hutolewa kutoka kwenye madini haya, na DR Congo ndio chanzo cha 40% ya usambazaji duniani.
Kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilisema mnamo Desemba 2024 kwamba M23 walisafirisha coltan kwenda Rwanda kutoka DR Congo. Pia ilibainisha kuwa mauzo ya coltan nchini Rwanda yalipanda kwa 50% kati ya 2022 na 2023.
Ingawa Rwanda ina migodi yake ya coltan, wachambuzi wanasema wanaweza kuchangia ongezeko hilo kubwa la uzalishaji.
Bado haijabainika iwapo kiasi au bei ya coltan iliyoingizwa nchini China imeathirika.
Madini mengine ambayo China inaagiza kutoka DR Congo ni cobalt, ambayo ni muhimu kwa sekta ya betri ya lithiamu.
Hata hivyo, shughuli za uchimbaji madini ya kobalti nchini China kimsingi ziko kusini mwa DR Congo, mbali na maeneo yenye migogoro ya mashariki.
Makumi ya makampuni ya Kichina, ambayo mengi ni ya serikali, pia yanajenga barabara, mawasiliano ya simu na vituo vya kuzalisha umeme kwa maji nchini DR Congo. Lakini inaonekana kwamba athari kwa shughuli hizi hadi sasa imekuwa ndogo.
Je, China inatoa msaada wa kijeshi kwa Rwanda au DR Congo?
China inasambaza silaha kwa Rwanda na DR Congo.
Katika miongo miwili iliyopita, jeshi la Rwanda limenunua magari ya kivita ya China, mizinga na makombora ya kukinga vifaru, kulingana na Taasisi ya Utafiti wa Amani ya Kimataifa ya Stockholm (Sipri).
Wakati wataalamu wa Umoja wa Mataifa wakisema kuwa jeshi la Rwanda limewapa silaha M23, haijafahamika iwapo kundi hilo la waasi linatumia silaha zozote za China.
Wanajeshi wa DRC wamenunua meli za kivita za China na ndege zisizo na rubani.
Pia wanamiliki mizinga ya Wachina, ambayo ilinunuliwa mnamo 1976 lakini bado ilikuwa inatumika hivi karibuni kama 2022.
Inaripotiwa kuwa ndege hizo zisizo na rubani, angalau, zimetumika katika vita dhidi ya M23.
Je, uhusiano wa China na nchi zote mbili umeathirika?
Ubalozi wa Rwanda mjini Beijing ulisema uhusiano na China umesalia kuwa "bora na wenye tija", na Rwanda haikutoa maoni yake kuhusu kauli ya China kuhusu mapigano mashariki mwa DR Congo.
Balozi wa China nchini DR Congo, Zhao Bin, alifanya mazungumzo na Rais wa Seneti ya Congo Sama Lukonde mwanzoni mwa mwezi Februari lakini hakuna maelezo ya mkutano huo yaliyowekwa wazi.
Shughuli za kiuchumi za China katika nchi hizo mbili zinakwenda kwa kina sana. Zote ni sehemu ya mpango wa China wa Ukanda na Barabara, ulioundwa ili kuunganisha China karibu na ulimwengu kupitia uwekezaji na miradi ya miundombinu.
Nchini Rwanda, China imefadhili viwanja vya michezo, shule na barabara kuu. Mikopo ya China pia inafadhili miradi ya miundombinu, mkopo wa kufadhili bwawa na mfumo wa umwagiliaji, wenye thamani ya wastani wa $40m (£31m), ulithibitishwa Januari.
Kwa miaka mingi bidhaa nyingi zinazoingizwa nchini Rwanda zimetoka China.
Linapokuja suala la uhusiano wa kiuchumi wa China na DR Congo, Hifadhidata ya Umoja wa Mataifa ya Comtrade inaonesha kwamba kwa miaka China imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa DR Congo.
China imejitahidi sana kupata utajiri wa madini nchini DR Congo.
Iliongeza $3.2bn (£2.5bn) ya mikopo kwa nchi kati ya 2005 na 2022, kulingana na Database ya China ya Mikopo kwa Afrika inayoendeshwa na Chuo Kikuu cha Boston, hasa kufadhili ujenzi wa barabara na madaraja, na gridi ya umeme ya nchi hiyo.
China imefadhili na kujenga miradi mingine mikubwa ya miundombinu nchini DR Congo, ikijumuisha mitambo ya kuzalisha umeme kwa maji na bandari kavu.
Uwekezaji huu unaweza kusema ni kwa manufaa ya muda mrefu ya China kupata suluhu la mzozo huo haraka.
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga