Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
M23 Kujiondoa Kwenye Mazungumzo ya Amani DRC: Nini Kinachofuata?
Mazungumzo ya amani yaliyopaswa kufanyika leo nchini Angola kwa lengo la kutafuta suluhu kwa mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) yamepata pigo kubwa baada ya kundi la waasi la M23 kujiondoa.
Uamuzi huu unazua maswali kuhusu hatima ya mazungumzo, mustakabali wa usalama mashariki mwa DRC, na hatua zitakazochukuliwa na pande husika ili kudhibiti hali ya mambo na mzozo unaoendelea DRC.
M23, ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali mashariki mwa DRC tangu 2021, linadai kupigania haki za jamii ya Watutsi wa Kongo lakini limekosolewa kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na uhusiano wake na mataifa ya kigeni.
Kujiondoa kwa kundi hili kwenye mazungumzo kunazidisha mvutano wa kidiplomasia na kunatishia kurejesha mapigano katika maeneo yaliyoathirika tayari.
Serikali ya DRC kuendelea na mazungumzo bila M23
Pamoja na kujiondoa kwa M23, serikali ya DRC imeashiria kuwa itaendelea na mazungumzo na makundi mengine ya waasi. Juhudi hizi zinaungwa mkono na Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambazo zinaamini kuwa mazungumzo ni njia bora ya kupata suluhu ya kudumu kwa mgogoro huu.
Wakati M23 wakisusia, ujumbe unaoiwakilisha DRC uko Luanda tayari kwa mazungumzo, msemaji wa Rais wa DRC Felix Tshisekedi aliambia shirika la habari la AP na kunukuliwa na Aljazeera, kwamba wenyewe watashiriki mazungumzo.
Hata hivyo, kuna changamoto kubwa: M23 ndilo kundi lenye nguvu zaidi kijeshi miongoni mwa makundi ya waasi mashariki mwa DRC. Kutoshiriki kwao kunamaanisha kuwa hata kama makubaliano yatapatikana na makundi mengine, bado hali ya usalama haitaimarika kikamilifu.
Swali kuu linabaki: Je, mazungumzo haya yanaweza kuwa na maana gani bila ushiriki wa M23? Na je, serikali ya DRC itatafuta njia nyingine, kama operesheni za kijeshi, ili kuikabili M23?
Juhudi za kidiplomasia: Je, Angola itaweza kurejesha M23 mezani?
Angola, ambayo imekuwa msuluhishi muhimu katika mzozo huu, huenda ikaongeza shinikizo kwa M23 kurejea kwenye mazungumzo. Hii inaweza kufanyika kwa njia mbalimbali, ikiwemo mazungumzo ya moja kwa moja na viongozi wa M23, shinikizo kutoka kwa mataifa yenye ushawishi, au hata kuhusisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya kundi hilo.
Juhudi hizi zinahitaji mshikamano wa kimataifa. Ikiwa Angola, kwa kushirikiana na AU na EAC, itashindwa kuwarejesha M23 kwenye meza ya mazungumzo, basi hatari ya kurejea kwa mapigano makali inakuwa kubwa.
Mchambuzi wa siasa za DRC, Didier Bitaki anasema ni muhimu kwa Jumuia za kimataifa kuingilia kati kwa sababu mzozo huo una chimbuka la mbali na unashirikisha makundi mengi.
Hatari ya kuongezeka kwa machafuko Mashariki mwa DRC
M23 ni mojawapo ya makundi yapatayo 100 yenye silaha ambayo yamekuwa yakigombea eneo lenye utajiri wa madini mashariki mwa DRC, karibu na mpaka na Rwanda.
Kujiondoa kwa M23 kunazidisha wasiwasi wa kuzuka kwa mapigano mapya katika maeneo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako kundi hilo lina nguvu kubwa. Tayari, jeshi la DRC (FARDC) linaendelea na operesheni za kijeshi dhidi ya waasi, na hatua hii ya M23 inaweza kusababisha mashambulizi mapya pande zote mbili.
Aidha, kuna hofu kwamba hali hii inaweza kuathiri zaidi uhusiano kati ya DRC na Rwanda. Serikali ya DRC imeendelea kuituhumu Rwanda kwa kusaidia M23, tuhuma ambazo Kigali imekanusha. Ikiwa mapigano yataendelea, kuna uwezekano wa mvutano wa kidiplomasia kati ya mataifa haya mawili kuongezeka, jambo ambalo linaweza kuvuruga juhudi za kikanda za amani.
Mzozo huo umezua mojawapo ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Zaidi ya watu milioni saba wameyakimbia makazi yao, huku watu 7,000 wakiripotiwa kufariki tangu mwanzoni mwa mwaka huu, huku mamilioni wakilazimika kuhama makazi yao. Kuendelea kwa mgogoro huu kunamaanisha mateso zaidi kwa raia wa kawaida ambao tayari wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.
Nini kinachofuata?
Ikiwa juhudi za kidiplomasia hazitafanikiwa kuwarejesha M23 kwenye mazungumzo, kuna uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi:
1. Mashambulizi Zaidi: M23 inaweza kuendelea na mashambulizi dhidi ya vikosi vya FARDC, jambo ambalo litazidisha machafuko.
2. Uwezekano wa Majibu ya Kijeshi: Serikali ya DRC inaweza kuamua kutumia nguvu zaidi kuwakabili waasi, hatua ambayo inaweza kuzua madhara kwa raia wa kawaida.
3. Shinikizo la Kimataifa: Mataifa ya kanda na jumuiya ya kimataifa inaweza kuingilia kati kwa kujaribu kuweka shinikizo kwa M23 kurejea mezani.
Mchambuzi wa siasa za DRC, Didier Bitaki anasema kama M23 imejitoa, haoni kama suluhu inaweza kupatikana bila kushirikishwa Rwanda.
'Wakati mwingine yeyote yule atatafuta ufumbuzi wa mzozo huu, ikiwa hataishirikisha Rwanda, hatuwezi tukafikia muafaka', alisema Bitaki.
Maneno ya Bitaki yanaashiria kwamba, bado safari bado ni ndefu kwwenye kutafuta mzozo huo kupitia mazungumzo. Kama Rwanda inayotajwa kuwa nyuma ya M23 inakataa kuwa sehemu ya mzozo huo na wanaiunga mkono M23, ni nani ataiwakilisha Rwanda kwenye mazungumzo yoyote yajayo?
'M23 inawasilisha maslahi ya Rwanda, Serikali ya DRC izungumze na Rwanda, muafaka utapatikana', anasema Bitaki.
Je nani ataialika Rwanda? na Rwanda itakubali mualiko kwa namna inavyokataa kuwa na ushiriki kwenye mzozo wa DRC?
Mazungumzo ya amani mara nyingi ni mchakato mrefu na mgumu. Hata hivyo, bila suluhu ya kisiasa inayojumuisha pande zote, mzozo wa DRC unaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi, huku raia wakiendelea kuathirika. Kwa sasa, hatua zinazofuata zitategemea juhudi za kidiplomasia za Angola na mshikamano wa mataifa jirani katika kutafuta suluhisho la kudumu.