Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, utajiri wa madini ndio imegeuza DR Congo kuwa eneo la vita?
- Author, Bella Nininahazwe & Jill Namatsi
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Ushindani katika kuyapata madini ni chanzo kikubwa cha vita kati ya vikosi vya DR Congo (FARDC) na kundi la waasi la March 23 Movement (M23), linaloungwa mkono na Rwanda, katika mikoa ya mashariki ya Kaskazini na Kusini mwa Kivu. Hifadhi ya madini ya DR Congo ni mojawapo ya hifadhi kubwa ya madini duniani.
DR Congo kuna bati, tantalum, tungsten (3T) na coltan, pia nchi nchi hiyo ina takriban 70% ya hifadhi ya cobalt duniani, nyingi ikiwa mashariki. Vilevile taifa hilo la Afrika ya kati lina akiba kubwa ya shaba, almasi, dhahabu, lithiamu, mafuta na gesi.
Ingawa baadhi ya rasilimali hizi bado hazijatumiwa, cobalt, ambayo ni muhimu kwa kuwasha betri za lithiamuion katika simu za rununu, magari ya umeme na sigara za kielektroniki, imekuwa muhimu sana kwani ni muhimu kwa makampuni makubwa ya teknolojia duniani kote.
M23 waliuteka mji mkuu wa Kivu Kaskazini wa Goma, tarehe 26 Januari na mji mkuu wa Kivu Kusini wa Bukavu.
M23 na madini ya DR Congo
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa muda mrefu imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la M23 ili kutwaa udhibiti wa rasilimali zake za madini.
Rwanda inakanusha madai hayo, huku ikiishutumu DR Congo kwa kushirikiana na wanamgambo wa Kihutu wa FDLR wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.
Kundi la M23 limeonyesha nia ya dhati ya kuchukua maeneo yenye madini mengi na kudhibiti njia muhimu za ugavi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kutekwa kwa Goma kuliashiria ongezeko kubwa zaidi la mzozo huo tangu uanze tena mwaka 2021.
Goma, iliyoko kwenye mwambao wa kaskazini wa Ziwa Kivu na inayopakana na Rwanda, ni nyumbani kwa zaidi ya watu milioni mbili na iko katika moja ya maeneo tajiri zaidi ya madini duniani. Jiji hilo pia hutumika kama lango la kuingilia katika baadhi ya maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.
M23 inadhibiti sehemu kubwa ya uchumi wa madini huko Kaskazini mwa Kivu, haswa kwa kukamata eneo la uchimbaji madini la Rubaya mwezi Aprili 2024, mgodi mkubwa zaidi wa coltan katika eneo la Maziwa Makuu. Kundi hilo la waasi lilipoteka Rubaya, lilianzisha "utawala," kutoa vibali vya uchimbaji madini na kutoza ada za kila mwaka kwa wachimbaji na wafanyabiashara.
Serikali inapambana kurejesha udhibiti wa eneo hilo. Maeneo yote ya uchimbaji madini yaliyo katika maeneo ya Masisi na Kalehe, hasa eneo la Rubaya na Nyabibwe yako chini ya udhibiti wa M23/AFC [Congo River Alliance].
Vyombo vya habari vya ndani vinasema hifadhi ya madini ya M23 imeongezeka na inazalisha kiasi kikubwa cha fedha. Tovuti ya Taarifa inayomilikiwa na watu binafsi ya Rwanda iliripoti tarehe 27 Januari kwamba, "pamoja na silaha, M23 sasa ina rasilimali muhimu za madini kama vile kobalti, coltan, na dhahabu."
Redio ya Virunga Businnes ya DR Congo iliripoti tarehe 18 Novemba 2024 kwamba M23, ilikuwa ikizalisha takriban dola za kimarekani 970,000 kwa mwezi kutokana na uchimbaji haramu wa coltan huko Rubaya.
Ilinukuu ripoti ya tovuti ya iliyofuatilia madini na nishati ya DR Congo ya Mines.cd. Idadi hii ni zaidi ya mara tatu ya makadirio ya Umoja wa Mataifa. Kulingana na ripoti hiyo, madini hayo yanayochimbwa kinyume cha sheria husafirishwa hadi Rwanda, ambako makampuni makubwa ya kimataifa kama vile Apple hupata madini hayo muhimu.
Ripoti hiyo iliongeza kuwa fedha zinazokusanywa na M23 hununua silaha kwa ajili ya upanuzi wa eneo lake na kuajiri wapiganaji wapya, "ikiwa ni pamoja na vijana kutoka Rwanda, Uganda na sehemu za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo."
Chombo cha habari kinachomilikiwa na watu binafsi kutoka Congo kiliripoti tarehe 29 Septemba 2023 kwamba M23, walichimba kinyume cha sheria kilo 5,440 za koltan na kilo 3,250 za cassiterite kutoka Rubaya, ambazo zote zilisafirishwa kwenda Rwanda.
Hata hivyo, taarifa kutoka katika tovuti ya Rwanda inayounga mkono serikali ya New Times ya tarehe 26 Februari, inayashutumu mataifa ya magharibi kwa kuufanya mgogoro wa DR Congo kuwa ni kuhusu tu utajiri wa madini."
Inasema simulizi hii "inatumika kuficha kuhusika kwa mauaji ya kimbari" katika mgogoro huo. Ripoti hiyo inasisitiza uwepo wa muingiliano kati ya unyonyaji wa rasilimali na migogoro katika eneo.
Wahusika wa kimataifa ni akina nani?
Tarehe 9 Septemba, shirika la habari la Reuters lilimnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, akisema utawala wa Trump unafuatilia makubaliano na DR Congo ambayo yatayapa makampuni ya Marekani haki ya kuchimba madini ya cobalt, lithiamu, uranium na madini mengine.
Kauli hiyo ilikuja baada ya tovuti ya Africa Intelligence yenye makao yake Paris kuripoti tarehe 5 Machi kwamba rais wa DR Congo, Felix Tshisekedi, alikuwa "akitumia kwenye rasilimali za madini" kutafuta kuungwa mkono dhidi ya M23.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, "maafisa wa DR Congo walitumwa kwenda Marekani mwezi uliopita ili kuipa serikali ya Donald Trump sehemu ya rasilimali kubwa ya madini ya nchi yao ili Washington iweke shinikizo kwa Kigali".
Tovuti hiyo iliongeza kuwa Tshisekedi alimtuma mshauri wake, Théo Mbiye kwenda Moscow mwezi Februari, ziara ambayo "ilichochea mazungumzo juu ya makubaliano ya uchimbaji wa madini kwa makampuni ya Kirusi."
Katika mahojiano ya Februari 3 na CNN, Rais wa Rwanda Paul Kagame alidai kuwa Afrika Kusini, ambayo ina wanajeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kama sehemu ya Misheni ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika nchini DR Congo (SAMIDRC), pamoja na nchi za Ulaya ambazo hazikutajwa majina, zilikuwa zikinufaika na madini.
Shutuma hizo zimezua mzozo wa kisiasa. Tarehe 12 Februari, wabunge watatu wa Bunge la Ulaya walitoa wito kwa Umoja wa Ulaya (EU), kuweka vikwazo mara moja kwa madini kutoka Rwanda, wakitaja kuhusika kwake katika mzozo huo.
Wiki chache baadaye, tarehe 24 Februari, EU ilisitisha mashauriano ya ulinzi na Rwanda na kuanza kupitia upya mkataba wake juu ya malighafi na Kigali. Rwanda imesema nchi ambazo zimetishia kuiwekea vikwazo zinachukua upande katika mzozo huo na kueleza "simulizi ya upande mmoja."
Ubelgiji pia imeingizwa kwenye simulizi ya madini, huku tovuti ya KT Press ya Rwanda ikitaja "mashirika mawili ya uchimbaji madini ya Ubelgiji yenye mabilioni ya dola lakini hayana mgodi haya mmoja."
Ripoti ya tarehe 4 Machi KT ilinukuu kampuni ya "Union Minière du Haut-Katanga (UMHK)— kampuni kubwa ya uchimbaji madini enzi za ukoloni- na kampuni yake mama ya Société Générale de Belgique, kampuni ambazo urathi wa wao unaendelea leo kupitia kampuni za Groupe Bruxelles Lambert (GBL) na Suez. Kampuni zote mbili zina mtaji katika soko wa zaidi ya dola za kimarekani bilioni 50 bilioni na zaidi ya dola bilioni 200 bilioni katika mapato ya kila mwaka.
Ripoti hiyo imesema, kampuni hizi zimekusanya mabilioni ya pesa huku zikiiacha Congo ikiwa masikini. Hazina mgodi hata mmoja katika ardhi ya Ubelgiji. Utajiri huu wote unatoka wapi?
Wahusika wengine wa kimataifa, wakiwemo mamluki na mashirika ya kimataifa, wanahusika katika mzozo huo. Desemba 2024, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo iliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya Apple kwa madai ya kutumia madini yanayotoka katika maeneo yenye mzozo, katika bidhaa zake. Apple ilijibu kwa kusitisha kuchukua madini ya 3T kutoka DR Congo na Rwanda.
Kipi kitatokea baadaye?
Vita vya mashariki mwa DR Congo ni mwingiliano wa masuala ya kikabila, kisiasa na kiuchumi, huku rasilimali za madini zikihusika kwa sehemu kubwa. Wakati jumuiya ya kimataifa ikisaka juhudi za kidiplomasia kuleta amani, mzozo huo hauonyeshi dalili ya kupungua.
Hali inazidi kuwa ngumu kutokana na ushiriki wa wahusika wengi wa kikanda na kimataifa, kila mmoja akiwa na maslahi yake katika eneo hilo lenye utajiri wa madini.
DR Congo imekataa mara kwa mara kufanya mazungumzo na M23. Hata hivyo, kuongezeka kwa wito wa kimataifa wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la waasi kunaweza kuilazimisha serikali kukubali. Hili likitokea, kunaweza kuwa na matumaini ya kumalizika kwa mzozo.
M23 pia ina msimamo wake. Katika mahojiano Mei 2024, kiongozi wa waasi Sultan Makenga alisema hawataacha kupigana hadi watakapoiangusha serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Rwanda imesisitiza kuwa jumuiya ya kimataifa lazima ielewe wasiwasi wa usalama wa Rwanda na kusema kuwa haitaruhusu mauaji mengine ya halaiki, na kuahidi kuchukua hatua zinazohitajika ili kujilinda.
Wakati vita hivyo pia vikitishia kusambaa katika mataifa jirani na kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo la Maziwa Makuu - Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amechukua msimamo mkali akimshutumu Kagame wa Rwanda kwa kupanga njama ya kuendeleza mzozo hadi nchini mwake.
Burundi imetuma maelfu ya wanajeshi kupigana pamoja na jeshi la DR Congo. Jeshi la Uganda lilisema tarehe 31 Januari kwamba iko tayari "kujihami" ili kulinda maslahi ya nchi.
Wasiwasi mkubwa kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ni iwapo M23 hatimaye itafikia mji mkuu, Kinshasa, kama kundi hilo linavyotishia.