'Nilikeketwa nikiwa na umri wa miaka 16 lakini sitaruhusu tukio hilo kuamua nitakavyoishi'

th

Chanzo cha picha, Valerie Lolomari

Maelezo ya picha, Valerie anataka kushiriki hadithi yake ya ukeketaji ili kuwahimiza waathiriwa wengine kutafuta usaidizi

Alipokuwa akilelewa nchini Nigeria, nyanya ya Valerie Lomari ndiye mtu pekee aliyewahi kumwonyesha upendo.

Akiwa na umri wa miaka 16, alichukuliwa na bibi huyo hadi kijiji kingine, ambako alikatwa sehemu ya viungo vyake vya siri bila onyo.

Sasa akiwa na umri wa miaka 52, Valerie bado anaishi na kiwewe cha kihisia na kimwili kutokana na ukeketaji wa wanawake (FGM) na amedhamiria kuutokomeza utamaduni huo.

Mama huyo wa watoto watatu husaidia waathiriwa wa ukeketaji huko Cambridgeshire, Essex, Hertfordshire na London.

Hapa, kwa maneno yake mwenyewe, anaelezea jinsi alivyojifunza kusamehe bibi yake na kuishi bila aibu.

Makala hii ina maelezo ambayo baadhi ya wasomaji wanaweza kukerwa nayo.

"Bibi yangu alisema tunaenda likizo"

th

Chanzo cha picha, Valerie Lolomari

Maelezo ya picha, Valerie alichukuliwa na nyanya yake akiwa na umri wa miaka 16 hadi kijijini, ambako alikeketwa.

Nilipozaliwa Lagos, Nigeria, mama yangu alikuwa na umri wa miaka 17 tu na hakuwa na usaidizi wa kutosha. Alinipeleka kwa familia ya baba yangu na nililelewa na bibi yangu. Alikuwa mzee na alikuwa na duka kwa hivyo nililazimika kufanya kila kitu ndani ya nyumba.

Nikiwa na umri wa miaka 11, babu yangu alikufa na nikahamia jiji jipya kwa nyumba ya jamaa yangu. Nikawa kijakazi na nikapitishwa kwenye familia tofauti. Sikuhisi kama kuna mtu ananijali kweli na nilimkosa sana bibi yangu.

Nilipofikisha miaka 16 alikuja kunitembelea na kusema tunaenda likizo. Nilifurahi sana na nilipakia mizigo yangu. Tukiwa njiani, bibi yangu alisema ilibidi tusimame ili kwenda kuona mtu katika kijiji hiki ambacho sikuwahi kufika hapo awali.

th

Chanzo cha picha, Valerie Lolomari

Maelezo ya picha, Valerie alihisi kusalitiwa na nyanya yake kwa sababu ndiye pekee ambaye Valerie alikuwa amewahi kumpenda
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nilipokuwa nikipita kwenye geti la nyumba hiyo, ghafla nilihisi kuumwa na tumbo. Mwanamke mmoja mrefu na mwenye sura ya kutisha alituingiza ndani na kufunga mlango. Niliona visu, nyembe na bakuli lililokuwa na mafuta likiwa limewekwa juu ya meza, huku wanawake wengine wawili wakiwa wamekaa na kunikazia macho. Nilimuuliza bibi kwa nini tulikuwa pale. Alifikiri ilikuwa inanifanya kuwa msafi na kunitayarisha kwa ajili ya ndoa.

Niligundua nini kitatokea na niliamua kupigana. Sikuwapa kazi rahisi kwa hivyo nilipiga kelele na kupiga mateke kwa nguvu zangu zote. Kabla sijajua, nilikuwa chini na wakanibana. Nilihisi maumivu makali na nikafikiri nitakufa. Nilipiga kelele hadi sikuweza kupiga kelele tena. Nilimuona bibi yangu akiwa amesimama pembeni na kumbania macho. Alikuwa akilia.

Nilihisi kusalitiwa na bibi yangu. Alikuwa ni mtu pekee niliyempenda na alikuwa ameruhusu hili linifanyikie. Nililazimishwa kulala chini kwa saa kadhaa ili damu yangu isimame. Ningejitoa uhai ikiwa ningeachwa peke yangu. Baada ya siku mbili za kuwa katika nyumba hiyo, bibi yangu alinichukua hadi alipoishi na nilikaa huko kwa muda, nikiugua magonjwa na wasiwasi mwingi wa kiafya kwa sababu ya kukeketwa

"Nilimwambia mume wangu kila kitu"

Mwishoni mwa majira ya joto, nilirudi shuleni na kuingia chuo kikuu. Nilificha kilichotokea kwa sababu nilikuwa na aibu, nilidhani ni kosa langu. Wakati wa mwaka wangu wa mwisho kwenye chuo kikuu, nilipokuwa na umri wa miaka 26, nilikutana na mume wangu Tony, ambaye alikuja kutoka London kumtembelea dada yake. Sikumsemesha sana kwani nilikuwa na woga sana ila nilimweleza kila kitu kilichonipata. Nilitaka kumweka kando kwa sababu sikufikiri kwamba nilistahili kupendwa, lakini hakunihukumu.

Ndani ya mwaka mmoja, tulifunga ndoa na kuhamia Uingereza. Hata tulipooana, ilikuwa vigumu kwangu kuongea naye, bado nilikuwa na wasiwasi mwingi. Nilikuwa nikizungumza naye kutoka chumba kingine au ningeandika mambo. kwenye kijikaratasi. Ilibidi aniamini lakini aliniamini zaidi ya nilivyojiamini.

Kushiriki tendo la ndoa daima imekuwa vigumu kwangu. Sehemu ya uke wangu imetolewa hivyo sihisi chochote na wakati mwingine inanifanya nijisikie kama mimi sio mwanamke kamili. Lakini najua nimebarikiwa kuwa na mtu ninayempenda.

Kwa bahati mbaya tulipoteza mimba nyingi kutokana na maambukizo na yalinirudisha katika utoto wangu na maumivu yangu. Baada ya ile ya tano, mume wangu alinishawishi niende kwa daktari, lakini niliogopa sana kuruhusu mtu yeyote anichunguze. Nilidhani hata ningekamatwa. Lakini daktari wangu aliniunga mkono sana na kunielekeza kwa mtaalamu wa ukeketaji.

Ninashukuru sana kwamba tuliweza kupata watoto watatu wa ajabu pamoja, wasichana wawili na mvulana. Kuzaa kulikuwa na uchungu sana ingawa kwa wiki ya kwanza au zaidi sikuweza kushikamana na watoto kwa sababu nilikuwa nikiuguza majeraha.

th

Chanzo cha picha, Valerie Lolomari

Maelezo ya picha, Valerie na mume wake Tony wamepata watoto watatu, lakini walipoteza mimba nyingi kutokana na ukeketaji na kusababisha maambukizi.

Baada ya kupata mtoto wa tatu, nilipata ujasiri wa kuzungumza na nyanya yangu kuhusu kile kilichotokea. Nilikata tiketi ya ndege na kurudi nyumbani. Nilimweleza yote niliyopitia na akaanza kulia. Ninaelewa sasa kwamba alifanya hivyo kwa upendo, alifikiri ilikuwa ni bora kwangu. Aliniuliza nizungumze juu ya uovu huo na kuhakikisha kuwa watu wanajua ukweli.

Nilianza kuwaambia watu juu ya kile kilichonipata na wanawake wengine waliniambia kwamba wao pia walikuwa wamepitia haya. Miaka mitano iliyopita, niliamua kuanzisha shirika la Women of Grace , shirika linalounga mkono waathiriwa wa FGM, na tumesaidia 168 kati yao hadi sasa. Tunakaribisha vikundi vya misaada , tunatengeneza nafasi salama na tunatuma wanawake kwa ushauri nasaha. Tunaelimisha familia na mimi huzungumza shuleni kuhusu hatari za ukeketaji. Ni ukiukwaji na unahitaji kukomeshwa kupitia elimu. Watoto wanapaswa kujua kwamba miili yao ni yao.

Nilikumbana na pingamizi mwanzoni kwa sababu kijiji ninachoishi Essex wengi wao ni wazungu. Ukeketaji unaathiri zaidi jamii za wahamiaji nchini Uingereza, lakini pia unaweza kuathiri watu ambao wameishi hapa kwa miaka mingi. Tatizo limezidi kuwa baya hapa tangu janga la Corona. Mara nyingi hufanywa na mpendwa, kisiri. Wanafikiri ni jambo la kawaida na ni sehemu ya utamaduni au mila zao. Kuna aibu nyingi na unyanyapaa na wasichana wengi hawataki kuzungumza vibaya kuhusu familia zao au jamii yao. Nimechapisha vipeperushi kuhusu FGM katika lugha tofauti ili niweze kuwafikia wanawake katika jamii zote.

th

Chanzo cha picha, Valerie Lolomari

Maelezo ya picha, Valerie alialikwa New York kutoa hotuba kuhusu FGM kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa

Ninajivunia kuwa balozi wa Healthwatch Essex, kikundi ambacho kinalenga kuelimisha wengine kuhusu kuishi na kiwewe. Hivi majuzi nilitoa hotuba kuhusu FGM katika mkutano wa Umoja wa Mataifa huko New York. Nilijikumbusha kuhusu siku nilipokuwa mdogo, nikiwa kijakazi, kisha kujipata New York, nikizungumza mbele ya watu wengi. Nilitokwa na machozi sana, nikijua ningeweza kutumia maumivu yangu na sauti yangu kuwasaidia wengine.

Mambo mengi yalichukuliwa kutoka kwangu na niliishi kwa maumivu, aibu na upweke kwa muda mrefu sana. FGM ni kifungo cha maisha na bado ninaishi na kiwewe cha kimwili na kihisia. Lakini ninakataa kuiruhusu initeke nyara na kuamua mkondo wa maisha yangu. Nina nguvu na ninapendwa na sitaacha kusimulia hadithi yangu hadi utamaduni huu wa kikatili utokomezwe.

Kama alivyosimuliwa Charlie Jones

Ikiwa umeathiriwa na masuala yoyote katika makala hii, ikiwa ni pamoja na hisia za kukata tamaa, unaweza kupata maelezo ya mashirika ambayo yanaweza kukusaidia kupitia BBC Action Line .

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah