Waridi wa BBC: 'Mama yangu alinitelekeza kwenye shamba la bibi nikiwa mchanga'
Na Anne Ngugi
BBC Swahili Nairobi

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Ikiwa maisha ya mtu hulingana na mwanzo wa maisha yake yanavyokuwa basi huenda maisha ya Lydia Nyambura kutoka Kenya yangekuwa na taswira ya shida na umasikini mkubwa, aghalabu anavyosema yeye.
Akiwa leo hii ana miaka 45 mwanamke huyu hajaacha kurejesha mawazo yake nyuma hadi wakati alipokuwa mtoto wa mwaka mmoja na nusu kama anavyosimuliwa na wakubwa wake , alikutwa ameachwa katika shamba la kahawa, ambalo lilikuwa linamilikiwa na bibi yake.
Lydia anasema kwamba alijulishwa na bibi yake kwamba alisikia sauti ya mtoto ikilia kutoka upande wa shamba na walipoitikia kilio hicho walimkuta akiwa amefungwa kwa nguo za mtoto mchanga chini ya miti ya kahawa .
”Nilivyoelezwa ni hivy , kwamba mama alipomaliza kuninyonyesha alinyemelea hadi shambani mwa bibi na kuniacha hapo, kisha yeye alirudi alikokokuwa anaishi na kuendelea na maisha yake pasipo kufuatilia iwapo nilipatikana au mambo yalikuwa vipi” Lydia anasema

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Ni bibi yake aliyempa malezi yake ya mwanzo wa maisha, hadi wakati anakuja kupata ufahamu wa maisha yake ndiposa akaelewa kwamba alikataliwa na mama yake mzazi , japo hamlaumu anasema kwamba anasababu zake za kufanyiwa hivyo.
Malezi bila mama yalikuwaje?
Lydia alikulia mikononi mwa jamaa wake wa karibu hususan shangazi, kwa wakati mmoja anasema kwamba alikuwa mikononi mwa shangazi huyo ambaye pia alikuwa na watoto wake , wote walilelewa pamoja.
Kwa mujibu wa mwanadada huyu malezi katika makao ya jamaa wake wa karibu hayakuwa rahisi , kulikuwa na ugumu wa maisha , akiwa binti alikosa mtu wa kumkumbatia na kumpa mawaidha ya ulimwengu, anasema.
Kila siku alikuwa anahisi kwamba alikuwa hapewi huduma kama za watoto wengine katika jamii za watu aliyokulia, alihisi kana kwamba yeye ndio alikuwa anafanya kazi ngumu na kwa muda mrefu , anahisi kwamba yeye ndio alikuwa anaadhibiwa kwa kosa lolote licha ya kwamba wangekosa wakiwa watoto wengi.

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
”Nilikuwa msichana mwerevu shuleni , nilikuwa msichana ambaye alianza kufahamu mapema kwamba nisiposoma kwa bidii na kujituma huenda nitaambulia patupu , ila mazingira niliyokulia yalikuwa ya mahangaiko sio haba.
Kichapo cha kila siku licha ya kwamba yangekuwa makosa madogo sana , kifupi niliishi maisha yaliojawa na uoga na pia suitafahamu ya maisha yangu ya baadaye ”anakumbuka Lydia
Licha ya hayo lydia aliendelea kujipambania mwenyewe kwa kila jambo , na kitu ambacho kilikuwa kinampa afueni ni kutokana na uerevu wake shuleni , lakini nyumbani mwa shangazi wake hali ilikuwa sio hali.
Kisa ambacho hajasahau ni kwamba kutokana na uoga mwingi ambao alikuwa nao alikuwa anakojoa kitandani kila siku , hali hii ilipelekea yeye kuwekwa kwenye chumba kimoja na watoto wa kiume ambao walikuwa wanakojoa pia, hawa walikuwa binamu wake.
Ila anasema katika kila anachokitaja kukosa ufahamu wa maisha mara kadhaa binamu wake wa kiume walijaribu kumnajisi ila alikuwa anapiga kamsa na wangeogopa.
Ni hali ambayo Lydia anasema ilikuwa inamkosesha usingizi.
Anakumbuka wakati mmoja alipata fursa ya kukutana na bibi yake , bibi aligundua kuwa afya na hali ya mwanadada huyu ilikuwa inazidi kuwa mbaya na ni fursa hio ambayo alipata kumjulisha bibi kwamba mambo nyumbani mwa shangazi hayakuwa sawa. Bibi alichukua uamuzi kwamba lydia arudi nyumbani mwa bibi.
”Nilifurahi wakati bibi aliamua kunichukua , kwani maisha yalikuwa mazito kwangu katika nyumba ya shangazi yangu.
Nyumbani kwa bibi nilipata malezo na upendo ambao nilishtahili ,Bibi na babu walihakikisha kwamba kila nilichokihitaji cha msingi nimepata ”anakumbuka Lydia.

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Wakati mwanadada huyu alifika wakati wa kuingia shule ya upili , ndio wakati alianza kugundua mwanamke ambaye alikuwa anafika katika boma hilo mara kwa mara ni mama yake.
Lydia anasema kwamba kila wakati alihisi damu zao zikivutana , licha ya kwamba alifahamishwa kwamba mwanamke huyo alikuwa ni mama yake ilichukua muda kuweza kumuita mama .Uhusiano kati ya mama yake na yeye ulikuwa haupo kabisa japo mama alikuwa anatembea nyumbani mwa bibi
”Mimi nilikuwa namuona mama akiingia kumtembelea mama yake , wakati mwengine kukaa na kisha kuondoka kwenda zake , hatukuwa na uhusiano wowote baada ya salamu , pia mama hakuwa na shughuli nyingi na mimi pia” anakumbuka Lydia
Mwanadada huyu alipohitimisha masomo ya sekondari alikuwa na ndoto za kuwa msanii muigizaji , kwa hio alitangamana sana na kuzuru maeneo ambayo waigizaji hupata ajira na kufanya mazoezi jijini Nairobi.
Mara kwa mara alipata nafasi ya kuigiza katika tamthilia tofauti na pia kwenye vitambulisho vya kibiashara vya runinga na redio.
Wakati Lydia anatimiza miaka 24 mama yake mzazi alimtizama binti wake katika runinga, na hapo ndipo mama aliamua kumtafuta Lydia.

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Hatua ya msamaha na mapatano
Mama alipofunga safari kumtafuta Lydia , walikutana na wakawa na mazungumzo japo hayakuwa ya muda mrefu , Lydia anasema kwamba alikuwa ni kijana wa kike aliyekuwa amejawa na hasira machungu na maswali mengi ya kwanini mama na baba hawakuwa katika maisha yake ya utotoni .
Lydia aliamua kumtafuta na kumtembelea mama hadi alikokuwa anaishi ambapo ni mbali na mji mkuu Nairobi , Mkutano huo wao ulikuwa mwanzo wa mchakato mrefu wa kufahamiana , na pia wa kuomba na kutoa msamaha.
“Baada ya kukutana na mama niliamua kumtembelea alikokuwa anaishi, nilikuta mama akiishi kwa mazingira ambayo sio mazuri , pia nilifahamu kwamba mama alikuwa amejaaliwa watoto wengine baada ya mimi na ndugu zangu wawili ambão walikuwa wanaishi na bibi pia.
Nilichukua majukumu ya kuhakikisha kwamba mama amehama mazingira hayo mabovu , hadi mazingira angalau yenye nafuu ”.

Chanzo cha picha, Lydia Nyambura
Uhusiano wa Lydia na mama yake ulianza wakati huo , japo anasema kwamba kulikua na siku za giza ambapo hawangesikizana lakini pia kumekuwa na siku za mwanga na furaha .
Mwanadada huyu anasema kwamba hakuna kitu kibaya kama mtoto kutelekezwa na mama mzazi , kwani mtoto anakuwa na fikra kwamba hakupendwa na kwamba hatakikani .
Vile vile mwanadada huyu anasema kwamba kunakuwa na hatari nyingi sana hasa kwa mtoto wa kike anapoachwa bila mama , hasa ikiwa mama amemtelekeza kwa kusudi
Lydia anasema kwamba , kukosa malezi ya mama na ule upendo ndiko ambako kunampatia mtoto wa kike uoga wa kutangamana na watu , kwake yeye anasema kwamba hali ya kukojoa hadi wakati anaingia miaka 17 ni mmoja wapo wa dalili za kuathirika na hali ya kukosa mama .
Ni zaidi ya miaka kumi tangu Lydia na mama yake kuanza safari ya kujenga uhusiano na kuweka msamaha kama kipaumbele cha maisha ya usoni na anasema kwamba imekuwa ni safari yenye pandashuka kwani kuelewana na mtu wakati kila mtu amejenga maoni yake juu ya maisha sio kitu chepesi ila kwa upande wake yeye amekaza kamba kuhakikisha kwamba jamii yake ina mahusiano dhabiti
Lakini Lydia kila kukicha pia anamzungumzia bibi yake kwa tabasamu kubwa kama mtu ambaye ni shujaa wa maisha yake , kwani ni yeye aliyehakikisha amesoma , amekula na amepata chochote alichokuwa anahitaji tangu alipomtoa shambani akiwa mtoto mchanga hadi utu uzima.
Cha mno mwanadada huyu anasema daima atamkumbuka bibi kwa kumpigania , kuhakikisha kwamba amemlinda dhidi ya ukatili wa ulimwengu na pia alimpa mawaidha , kuchukua nafasi ya ya mama mzazi kwa miaka ambayo mama hakuwepo.















