WARIDI WA BBC: ‘Nilishuhudia watoto wengi wakifariki kando ya mwanangu’

th

Chanzo cha picha, Racheal Muireithi

    • Author, Na Anne Ngugi
    • Nafasi, Bbc Swahili

Racheal Muireithi , ni mama mwenye umri wa miaka 28 kutoka Kenya , kuzaliwa kwa mwanae wa kiume miaka 6 iliyopita kulikuwa mwanzo wa safari ya aina yake maishani mwake .

Mwanae anafahamika kama Kingsley , katika umri alionao ambao kawaida watoto wa umri huo sasa wako katika mwaka wa pili wa chekechea au darasa la kwanza , Kingsley ni mtoto ambaye hadi sasa hana uwezo wa kuzungumza , kutembea na pia hana uwezo wowote wawa kujifanyia chochote .

Majukumu yote yako mikononi mwa mama yake .

Masaibu yalianzia wapi ?

th

Chanzo cha picha, Racheal Muireithi

Akiwa na miaka 22 , Racheal alikuwa bado ni kijana wa kike ambaye hakufahamu alikuwa ameshika mimba licha ya kwamba ilikuwa imefikia miezi minne , ila kilichokurupua hali yake kujulikana ni wakati aliposikia kuwa kaka yake alikuwa ameaga dunia ghafla , mwanadada huyu anasema kwamba kutokana na mshtuko alizimia na ikabidi afikishwe hospitalini

“Mara nilipofahamishwa kuwa kaka yangu alikuwa ameaga dunia , nilishtuka sana , kilichofwatia ni afya yangu kuanza kudhoofika , kumbe wakati huo nilikuwa na ujauzito wa miezi minne na sikuwa na ufahamu wa hali hio ” anakumbuka Racheal

Ilibidi mwanamke huyu akae hospitalini kwa muda , masaibu ya hali ya majonzi yalimzidi na anasema kwamba alijifungua mtoto wake kabla ya wakati unaofaa kwa mwanamke wa miezi tisa , yeye alijifungua wakati mimba ikiwa na miezi 6 .

Kwa kawaida wanawake hupokezwa wana wao pindi wanapozaliwa ila kwa mwanadada huyu ilibidi mtoto awekwe dharura kwenye machine maalum ilikumuwezesha kupumua hali kadhalika kuongeza uzani kwani wataalam walishauri kwamba alikuwa na uzani mdogo wa kuruhusiwa kurudi nyumbani. Aidha mwanadada huyu anasema kwamba pia wakiwa pale hospitalini iligunduliwa kwamba mwanaye mchanga alikuwa na kichwa kikubwa kuliko mtoto wa kawaida anapozaliwa , asijue kwamba hali hio ingekuwa mwanzo wa matatizo makubwa katika Maisha yake kama mama , na pia Maisha ya mtoto .

Ila baada ya muda waliruhusiwa kurudi nyumbani , kitu ambacho Racheal aligundua ni kwamba mwanae hakuwa na uwezo wa kunyonya maziwa ya mama mwenyewe , ilibidi akayakamua na kisha kumpa kwa mrija , jambo ambalo anasema kwamba lilimpa siku nyingi za kutolala na mawazo mengi kwani hakufahamu ni kwanini mtoto hakuwa anatabia kama za watoto wachanga .

w

Chanzo cha picha, Rachael Muirethi

Wataalam wa ubongo kwa mujibu wa mama huyu walipendekeza mwanae afanyiwe upasuaji wa kuweka kifaa kama mrija ndani ya ubongo wake ilikuondoa maji yaliokuwa yanasababisha uvimbe wa kichwa au kile wataalam wanakitaja kama Congenital Hydrocephulus , na ndio hatua ambayo Racheal aliichukua na mtoto alifanyiwa upasuaji huo .

Ila mama huyu anasema kwamba uvimbe huo ulikuwa umesababisha uharibifu mkuu katika ubongo wa mwanae kwa kiasi kuwa madakatri waliokuwa wanamuuguza walimpa ushauri kuhusu hatma ya Kingsley

“Madaktari walinieleza kuwa huyu mtoto wangu alikuwa ameharibika ubongo kutokana na uzito wa maji , na hali yake ya kuishi itakuwa ni ngumu sana , nilikataa kusikiliza ushauri huo , nilimuuliza Mungu kimoyomoyo ni kwanini ni mimi tu nimepewa mtoto mwenye matatizo kiasi hicho , sikupata jibu hadi leo ”anakumbuka Racheal

Hali ya matibabu ya Kingley .

th

Chanzo cha picha, Racheal Muireithi

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Racheal anasema kwamba ilikuwa sio rahisi kukubali utabiri wa wataalam , na kwa siku nyingi alikuwa analia mno , anasema kwamba tumaini lake kubwa lilikuwa ni watu wa jamii yake ambao baada ya mtoto kuhitimisha mwaka mmoja waliruhusiwa kwenda nyumbani , ila mara kwa mara ilibidi warejee hospitalini kutokana na dharura moja au nyengine ya mtoto wake .

“Dharura za kumkimbiza mwanangu hospitalini zilikuwa nyingi mno , mara hapumui , mara joto liko juu na kadhalika hadi nilikuwa najiuliza kwani Maisha yangu yote nitaishia kuishi mazingira ya hospitalini ”anakumbuka Racheal

Mama huyu anasema kwamba wakati mwanae anafikisha miaka miwili alikuwa anapata kifafa cha kila mara na hakuwa anamudu hali ya kumpa madawa yaliokuwa yanatakikana kwa hio jukumu kubwa lilikuwa jinsi ya kumfikisha hospitalini baada ya tukio kama hilo kufanyika ghafla .

“Nilikuwa mama wakuingia hospitali na kutoka , uchungu mwingi ulikuwa kumtizama mwanangu akipitia uchungu na kama mama sina uwezo wa kumsaidia na lolote ila kumtizama tu kwa macho ya huruma “anakumbuka Racheal .

Wakati mmoja mama huyu anasema kwamba mwanaye alikuwa amewelazwa kwenye wodi ya Watoto wanaougua saratani , katika wodi hio Racheal anasema kwamba alishuhudia Watoto wakifariki kila kuchao na aliingiwa na hofu na uoga kwamba huenda siku mmoja atakaye fuata ni mwanae .

“Kuna wakati tulikuwa kwenye wodi ambayo watoto wawili wagonjwa walikuwa wanalala kitanda kimoja , nilishuhudia baadhi ya Watoto waliokuwa wamelala kitanda kimoja na mwanangu wakifariki , yaani nilihesabu Watoto ambao walikuwa wanafariki nikiwa pale , ni wakati ambao sitawahi kusahau kamwe ”anakumbuka Racheal

Mama huyu anasema kwamba hali hii ilimpa hofu mno , kwani alikuwa na mazoea kwamba kwenye wodi yao wakati wa usiku angesikia wazazi wengine wakipiga mayowee baada ya Watoto wao kufariki ,angeshuhudia miili ya watoto hao wachanga wakiondoshwa usiku , wengine kufunikwa hadi nyakati za asubuhi , anasema kwamba kwa macho yake alishuhudia Zaidi ya Watoto 200 wakiaga dunia walipokuwa kwenye wodi ni hali inayompa machozi hata leo .

Kukubali hali ya mwanake

th

Chanzo cha picha, Racheal Muireithi

Mama huyu anasema kwamba amekubali hatma ya mwanaye , licha ya kwamba yuko katika kiti cha magurudumu , anaona mwanaye anapiga hatua japo ni za mwendo wa pole .

Kwa mfano anasema kwamba Mwanae Kingsley anauwezo wa kushikilia kikombe chake kwa muda wakati anakunywa chai , kwa wakati huu mwanae anaweza kunena japo matamshi machache ya kuamkua na yale anayoyasikia kutoka kwa watu waliokaribu na yeye .

Ilimbidi mama huyu pia kuacha kazi zake za ususi kwa wakati huu ilikumlea mtoto wake , anahisi kwamba nguvu na kujitolea ilikuhakikisha kwamba mwanaye angalau atakuwa na nafuu.

Mama huyu hajakata tamaa kwamba mwanae atakua tu kama watoto wengine licha ya kwamba yuko nyuma sana katika maendeleo ya kukua kwake kimwili kiakili na kisaikolojia 

“Najaribu sana kumuweka mtoto wangu sehemu ambayo kuna Watoto wengine , naamini kwamba akiwa kwenye mazingira ambayo watoto wanatangamana atajifunza mengi , kwa sasa naona anajifunza kujishika kichwa , anajifunza angalau kutohoa neno moja la salamu na hilo kwangu kama mzazi naridhika ”anasema Racheal

Yote tisa kumi ,mama huyu anatoa nasaha kwa jamii kuhusu unyanyapaa ambao unapatikana kwa wazazi na kwa watoto ambao wanaishi na kuzaliwa na ulemavu, vile vile anatoa matumaini kwa wanawake ambao wanawalea watoto wenye mapungufu kutokata tamaa licha ya changamoto zinazokuwepo .