Waridi wa BBC: Jinsi ‘ushamba’ ulivyomponza msaidizi wa nyumbani ambaye hakukata tamaa ya maisha licha ya changamoto

Chanzo cha picha, Esther Nyokabi
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Esther Nyokabi hataisahau siku ya kwanza alipotafuta kazi ya ajira kama mfanyakazi wa nyumbani , kwani anasema haikuwa rahisikwa sababu hakuna yeyote aliyemtafutia kazi bali alichukua mkoba wake na kutembea kwenda nyumba hadi nyumba na kubisha huku akiuliza iwapo kulikuwa na hitaji la msichana wa kazi.
''Nilitembea sana siku ile'', aliniambia katika mahojiano haya.
Akiwa na umri wa miaka 36, Bi Esther ni mama wa mtoto mmoja na ni mama wa kambo wa watoto wawili. Ameolewa na mjasiriamali ambaye maisha yake ya hapo awali anayatumia kama daraja la mafunzo nchini Kenya.
Hii inahusu hasa maisha yake alipokuwa mfanyikazi wa nyumbani .
'Maisha ya kuwa mfanyakazi za nyumbani'
Anasema chaguo lake la kuwa mfanyakazi wa nyumbani lilitokana na maisha yake yaliyojaa masaibu tangu alipokuwa na umri mdogo wa miaka 25.
Hatua yake ya kukatiza masomo ilikuwa ndio chanzo cha mahangaiko makubwa ya kuajiriwa kama yaya kutoka nyumba moja hadi nyingine.
Anasema amekuwa kwenye kazi hiyo katika familia zisizopungua ishirini.
"Unajua unapokuwa hauna masomo yoyote, huna budi kukubali kufanya kazi kazi yoyote ya mikono kwa mfano kufua, kupika kulea watoto, ujenzi na kadhalika, ndio yalikuwa maisha yangu hapo awali, sikuwa na chaguo ila kukubali kazi za nyumba kama njia ya kukidhi mahitaji yangu", anasema Esther.
Esther anakiri kuwa wakati anaajiriwa kama mfanyakazi wa nyumbani, alikuwa hana vyeti vyovyote au ujuzi wowote wa kitaaluma kilichoingia akili mwake ni wepesi wa kuwa msaidizi wa nyumbani kwani angeimudu kwasababu ni kazi aliyokuwa akifanya akiwa nyumbani kwao
"Nakumbuka kwamba nilizunguka mno huku na kule nikibisha hodi kwenye milango ya watu , nikiomba kazi na kwa kweli nilifanikiwa.
Kitu nilichokigundua ni kwamba kila nyumba ina sheria zinazotolewa kwa wasaidizi wa nyumbani na nilipokea yote kama sehemu ya kazi ", anasema Esther.
'Ushamba mwingi ulimponza'

Chanzo cha picha, Esther Nyokabi
Wakati alipoanza kazi hiyo, hakujua kwamba maisha ya vijijini ni tofauti na ya mijini, kwa hiyo alipoanza kazi alijipata akiwa katika hali ya kutoelewa mtindo wa maisha katika nyumba za mijini, akisema alijiona mwenye 'ushamba' mwingi katika mazingira ambayo hakuwa ameyazoea.
Makosa madogo madogo kutokana na kutojua jinsi ya kutumia hasa vyombo vya kisasa vya umeme vilimuweka kwenye matatizo na waajiri wake, alisema.
Huku akiangua kicheko, mwanamke huyu anakumbuka siku ya kwanza alipopigwa na mwajiri wake aliposhindwa kutumia kifaa cha kupasha chakula moto almaarufu microwave , na licha ya kupokea kichapo Esther anasema kwamba aliendelea kufanya kazi zake katika nyumba ile.
Wakati huo anakiri kwamba hakuelewa haki zake kama msaidizi wa nyumbani na hivyo alipiga moyo konde na kuendelea kuvumilia unyanyasaji yakiwemo matusi asijue ni wapi anaweza kupata usaidizi.
"Nilipoingia mjini nilikuwa sielewi mengi tuseme nilikuwa tu mshamba, nakumbuka wakati mmoja nilikuwa nimeagizwa na mwajiri wangu nipike soseji , sikufahamu hupikwa vipi , mimi niliweka soseji kwenye sufuria na kuanza kuzichemsha , nilishangaa ni kwanini haziiivi kama nilivyoagizwa "Esther anakumbuka.
'Kushawishika kimapenzi na mwajiri'

Chanzo cha picha, Esther Nyokabi
Mwanadada huyu anasimulia safari ya kutoka nyumba moja hadi nyengine na wakati mwingine hali na mazingira ya kazi za nyumbani haikuwa rafiki.
Anadai baadhi ya wanaume walikuwa na tabia ya kutongoza wafanyikazi wa nyumba,jambo analosema alilipitia .
"Kwa kusema ukweli mimi nimefanya kazi za nyumba, kwa zaidi ya miaka mitano, katika muda huo nimekuwa ndani ya nyumba zaidi ya ishirini nchini Kenya, nimekumbana na watu wazuri sana na watu ambao wanawadharau wafanyikazi wanyumbani na wengine pia wana nia mbaya ya kuwatumia wafanyakazi ambao hawajielewi au kufahamu haki zao ", anasema Esther.
Mwanadada huyu anatoa taswira ya baadhi ya nyumba alizofanyia kazi na maisha yake yakawa na sonona, kwa mfano anasema kwamba wakati anafanya kazi alikumbana na wenye nyumba wanaume ambao walikuwa na tabia ya kumsumbua sumbua kwa kutaka mahusiano ya kimapenzi ya siri au kama alivyosema awe 'mpango wa kando'.
Esther anasema kwamba hali kama hiyo imemtokea mara nyingi tu.
"Haya mambo nimeyapitia katika baadhi ya nyumba nilizofanyia kazi, na ilikuwa ni changamoto kwa sababu mimi sikuwa tayari kwa mahusiano ya kando , kuwazia tu kwamba ningeshiriki mapenzi ndani ya nyumba ambayo mimi ni mfanyakazi ilinitatiza mno na kwa hiyo nilijipata katika njia panda na kujipata bila ajira "anakumbuka Esther.
Anakumbuka kisa kimoja ambapo anakiri nusura aingie kwenye mtego wa mahusiano kama hayo ambapo mume wa mwajiri wake alikuwa amemuahidi makubwa , kwa mfano anasema kwamba alikuwa ameahidiwa kurejeshwa chuoni , kupangiwa nyumba pamoja na maisha ya juu.
Esther anasema kwamba kishawishi kikuu kilikuwa kwamba alikuwa kwenye umasikini mkuu na alitamani maisha ya juu , ila alijitoa kabla ya hatari kuingia.
Anasema :"Kama mwanamke nilihisi iwapo ningejihusisha na mahusiano ya kando katika nyumba ya mwajiri wangu , ningeharibu familia na kutenganisha watu katika ndoa , nilikuwa nawaza kwamba siku za usoni pia mimi nilitamani ndoa na sikutaka nijiharibie kwa kuharibu familia za watu "anasema Esther.
Ushauri kwa wasaidizi wengine wa nyumbani na jamii

Chanzo cha picha, Esther Nyokabi
Ni matukio kama haya ambayo yalimsukuma mwanadada huyu kuzungumzia hadharani changamoto na masaibu yaliompata kama mfanyikazi wa nyumbani.
Esther anasema kwamba miaka aliyohudumu kama msaidizi wa nyumbani ilimfunza mengi kuhusiana na jamii inavyowatazama wahudumu kama yeye .
Esther aliamua kuacha kazi ya nyumba na kuanza masomo maalum yanayohusu ushauri kwa wanaoishi na virusi vya HIV(VVU) , alihitimu na kuanza kufanya kazi katika taasisi mbali mbali.
Esther anajiona kama kielelezo chema katika jamii , na anatoa ushauri kwa wafanyikazi wa nyumbani kwamba inawezekana ukaanza kwa kazi hiyo na baadaye maisha yakaboreka
Unaweza pia kusoma:
Anasema kwamba kuwa mfanyakazi wa nyumba haimaanishi kwamba hautakuwa na maisha mazuri baadaye, bali kazi ya nyumbani inaweza kuwa daraja la kuvuka katika maisha mengine .
Anaisihi jamii kutowadharau wafanyikazi wa nyumbani, kwani wao huwa ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa shughuli ndani ya familia hususan zile zinapohusu malezi ya watoto wadogo.













