Waridi wa BBC: Kimada alilala kwangu wakati nilipokwenda kujifungua hospitalini

Chanzo cha picha, Esther Nduku
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Bi.Esther Nduku anasema anapoyakumbuka maisha yake ya ndoa, hushangaa ni vipi alivyoweza kustahimili na kujivunia ndoa hiyo.
Ni ndoa iliyojaa kudharauliwa na mateso ya kila aina.
Jambo kubwa zaidi katika matukio ya kustajabisha yaliyowahi kumtokea ni pale alipokuwa amekwenda hospitalini kujifungua mtoto wao wa pili.
Ni jambo ambalo mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 32 hakuamini linaweza kuwa linafanyika kwenye ndoa yake.
Ujumbe wa kushangaza
Nduku anadai kuwa akiwa hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wa kujifungua, pindi tu alivyoanza kupata nafuu alipitia tukio la kuogofya.
Alipokea picha na ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.
Picha zenyewe anasema zilikuwa zimetoka kwa mwanamke ambaye baadaye aligundua kuwa alikuwa kimada wa mume wake.
Nduku anasema kuwa picha alizozipokea zilikuwa zinamuonyesha mwanamke huyo akiwa kwenye chumba chao cha kulala.
Mwanamke huyo alionekana akiwa amevalia nguo zake za ndani na alizokuwa anazivalia wakati wa kulala.
Mwanamke huyo, kwenye ujumbe wake, mambo yote waliyokuwa wakiyafanya na mume wake katika nyumba yake.
Baadhi ya picha alizotumiwa ziliwaonyesha wawili hao wakistarehe kimapenzi na hata wakiwa utupu.
Asijue la kufanya, Nduku anasema alisikia baridi sana ghafla mwilini mwake, asiamini macho yake kuwa aliyekuwa mume wake angemsaliti na pia kusaliti ndoa yao kwa kiasi hicho.
Bi Nduku anakiri kuwa ndoa yao ilikuwa na misukosuko lakini hakutaka kuamini mumewe angefikia hatua kama hiyo.
Walikuwa wameishi pamoja kama mume na mke kwa miaka minne.
"Nilipopata nguvu, nilimtumia aliyekuwa mume wangu picha hizo. Cha kusikitisha zaidi ni kuwa licha ya kumpigia simu na kumuuliza kuhusiana na picha zile alipuuza tu na kuniuliza kipi kikubwa alichokuwa anakifanya , kuashiria kuwa nilikuwa nikubali matendo hayo," anakumbuka Nduku
Mwanadada huyu anasema kuwa kwa kipindi alichokaa hospitali aliyekuwa mumewe hakumjali.
Hata siku ya kwenda hospitalini kujifungua mume wake hakuandamana naye.
Baada ya siku kadhaa, mwanamke huyu anasema kuwa baba ya watoto wake hatimaye alikwenda hospitalini kumchukua yeye na mtoto aliyezaliwa.

Chanzo cha picha, Esther Nduku
Kurejea nyumbani
Kwa kawaida tukio la mama aliyejifungua mtoto anaporejea tena nyumbani, huandamana na mbwembwe kutoka kwa wanafamilia na jamaa wa karibu.
Lakini kwake Nduku aliyekuwa mume wake alipotokea hospitalini kuwarejesha nyumbani badala ya furaha - ilikuwa ni simanzi na kiza kikuu.
Badala ya mume wake kupakata mtoto kwa machozi ya furaha, ilikuwa kinyume. Wanandoa hao hawakuwa na uwezo wa kuangaliana usoni.
"Badala ya hata kuomba pole mume wangu alinieleza kuwa ni shetani aliyekuwa amemzingira, na kwamba hata yeye mwenyewe hakujua ni kipi kilichokuwa kinatendeka," Nduku anakumbuka.
Kwa kurejea nyumbani mwanamke huyu hakuhisi kama aliyependwa.
Aidha, alifahamu kuwa majirani na wale waliokuwa wanaishi karibu na nyumbani kwao tayari walikuwa wamefahamu yaliyokuwa yanafanyika nyumbani kwao wakati alipokuwa hospitalini.
Mkasa nyumbani
Bi Nduku anasema kuwa uhusiano wao uliendelea kudorora.
Baada ya siku tatu za kukaa nyumbani kwake kama mama aliyejifungua alipokea simu kutoka nyumbani iliyomfahamisha kuwa mama yake mzazi alikuwa amepata ajali ya barabara iliyokuwa mbaya mno.
Kisa hicho kilimhitaji nyumbani kama kifungua mimba wa mama yake ambaye hakuwa na mume.
Na kwa hivyo kwa upesi Nduku aliamua kufungasha virago na kuondoka na mtoto mchanga hadi nyumbani kwao ili amshughulikie mama yake.
Kipindi hicho kilikuwa kigumu kwani kama anavyosema ni kana kwamba mume wake wakati huo aliamua kuendeleza urafiki wake na kimada yule.
Nduku anasema uhusiano huu haukufichika tena na yule kimada alitosheka na kukaa katika nyumba yake.
Mwanamke huyu anasema kuwa kipindi hicho cha kati ya 2015-2016 kilikuwa na changamoto nyingi mno kwenye ndoa yake na maisha yake.
Unaweza pia kusoma:
Kurejea nyumbani
Baada ya muda wa miezi sita mwanadada huyu aliamua arejee nyumbani kwake kwa kuwa binti yao wa kwanza alikuwa amebaki na (baba) mume wake mjini na alihitaji amuone.
Uhusiano wa mume wake na yule kimada ulikuwa tayari umesambaratika. Alikuwa ameondoka kule nyumbani kwake.
Mambo hayakurejea kama kawaida.
Nduku anasema kuwa alijawa na hofu na huzuni kuu kila wakati.
Anakiri kuwa tukio la kimada wa aliyekuwa mume wake alichokifanya cha kutuma picha za mapenzi yake na mume wake kilimpatia mawazo mengi mno kiasi cha kushindwa kufanya chochote.
Ni wakati huo ambapo Esther Nduku alihisi kuwa hangeweza kuendelea na ndoa ile tena kwani wakati huo majirani na wote tayari walikuwa wanazungumza na mtaa wote ulijawa na minong'ono kuhusu kisa cha mume wake kuishi na kimada kwenye nyumba ya ndoa .
Nduku anadai kuwa baba wa watoto wake na yule kimada hawakuwa wanaficha mambo yao.
Nduku anasema hangeivumilia aibu hii na aliamua kuondoka.
Nduku alikutana vipi na mumewe?

Chanzo cha picha, Nduku
Esther Nduku alizaliwa nchini Kenya katika Kaunti ya Makueni.
Hakufanikiwa kuwa na baba na kwa hivyo mama alikuwa mzazi wa kipekee na alijizatiti sana kuwapa malezi bora Nduku na dada yake.
Baada ya kumaliza masomo ya sekondari, alielekea mjini na kujiunga na taasisi ya filamu na uzalishaji wa vipindi kwa mafunzo.
Yeye na marafiki kadhaa wa kike walikuwa wanaishi kwenye nyumba mmoja, kama njia ya kuokoa fedha za malipo ya kodi.
"Ilifika wakati ambapo mimi na marafiki wangu hatukuwa tunaelewana na ikabidi mimi nihame kutafuta makao mengine ghafla," anasema.
„Sikumfahamu yeyote mjini ila nilikumbuka kuhusu mwanamume mmoja ambaye tulikuwa tunasoma naye kule kwenye taasisi . Nilipomuomba ikiwa angekubali niishi kwake kwa muda hakukataa," Nduku anakumbuka
Mwanamke huyu anasema kuwa hapo ndipo ndoa yake ilianza kwani muda mfupi tuu wa kuishi kwenye nyumba hio walijipata kwenye mahusiano ya kimapenzi .
Vile vile baada ya muda pia aligundua kuwa alikuwa ameshika ujauzito .

Chanzo cha picha, Esther Nduku
"Tulipogundua kuna ujauzito tulikubaliana ni vyema tuanze kuishi pamoja kama mume na mke. Tulipanga taratibu zote za kuwaona wazazi wa upande wa kwangu na upande wa kwake na basi hapo ndipo tulianzia ndoa yetu," Nduku anakumbuka
Mwanamke huyu anahisi kuwa ndoa kati yake na baba wa watoto wake ilianza kwa misingi ambayo haikuwa sawa.
Alipomuomba awe mwenyeji wake kwa muda, walikuwa ni marafiki wa kawaida na wala hawakuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Anahisi kuwa wao wawili hawakuchukua muda kufahamiana vizuri kabla ya kuamua iwapo wangeingia kwenye ndoa au la.
Esther Nduku anasema kuwa alikaa na picha alizotumiwa na kimada wa aliyekuwa mume wake kwa muda. Ila alipoamua kumsamehe na kuachilia tukio hilo maishani mwake alizifuta zisiwe zinamkumbusha aliyoyapitia.
Esther anasema kuwa kupitia msongo wa kimawazo na mfadhaiko alifahamu kuwa huenda kuna watu wanaopitia madhila mengi au majaribu wakiwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na hawajui wafanyeje.
Alianzisha shirika ambalo linatoa nafasi kwa wahanga kukutana na kujadili changamototo za kiakili wanazopitia wanapokuwa kwenye mahusiano.
Anasema wengi wamefaidi kupitia mradi huo.













