Baby Musamba kwa miaka 26 alificha siri kuwa hana viungo vya siri vya kike wala vya kiume

Baby John Musamba kwa miaka 26 ameishi akiwa hana maumbile ya siri ya kiume wala ya kike

Chanzo cha picha, Baby John Musamba

    • Author, Anne Ngugi
    • Nafasi, BBC Swahili

Kwa miaka 26 , Baby John Musamba aliishi na siri kuu ambayo hakuwafichulia hata marafiki zake na jamaa.

Ni siri ambayo ilitunzwa kwa karibu sana na wazazi wake na jamaa wachache wa karibu, lakini tangu ajitambue na kufahamu kwamba kuna jinsia mbili, ilibaki kumsumbua usiku na mchana.

Kwa kiwango fulani, kulikuwa na kidokezo kuhusu siri hiyo kwenye jina ambalo wazazi wake walimpa. Lakini nani anaweza kudhani kwamba jina linaweza kuwa na fumbo lisiloweza kufumbuliwa na watu wa nje? Ni fumbo ambalo hata ulitolee mji, ni vigumu kulifumbua bila mhusika kuwa na nia ya kuifichua.

Haya yote yalianza vipi?

Kuzaliwa hospitalini

Baby John Musamba mwenye umri wa miaka 26 alizaliwa katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Lakini badala furaha ya wazazi wake kujaliwa mwana iligeuka mshangao. Mtoto wao alikuwa na maumbile ya ajabu.

Musamba alizaliwa bila sehemu za siri za mtoto wa kiume au kike.

Wazazi wa Musamba walichanganyikiwa na hawakujua jina stahiki la kumpatia mtoto wao.

Musamba aliishi kuificha hali yake hadi alipochukua fomu za shughuli ya mchujo wa wabunge alipojaza kuwa mtu asiyekuwa na jinsia.

Chanzo cha picha, Baby John Musamba

Baada ya kutafakari na kujadiliana kwa kipindi kirefu, waliamua kumpatia jina Babi. Kwa kawaida angekuwa wa kike pengine wangemrithisha jina la babu yake na angekuwa wa kike jina la bibi.

Sasa, amefika malaika ambaye si wa kurithishwa babu wala bibi. Waliamua awe wote wawili kwa pamoja, wakampa jina Babi ambalo ni ufupisho wa jina babu na bibi.

Baadaye kwa kuandikwa, kwani latamkwa kwa njia sawa, Musamba akawa Baby.

Kulingana na Musamba ameificha hali hii kwa muda mrefu sana na imekuwa siri kubwa aliyokuwa ameificha baina yake na jamaa zake wa karibu.

"Nilielezwa kuwa uamuzi huo ulifanywa kuwakilisha babu na bibi ili katika siku za usoni iwapo maumbile yangu yangedhihirisha jinsia kati ya kike na kiume ningeitwa Babu kama ningeashiria kuwa mwanamume," anasema.

"Ningeitwa Kibibi ikiwa maumbile yangu yangejidhihirisha kuwa ya binti. Ila hadi sasa bado sina jinsia yoyote iliyojidhihirisha, iwe ni ya kike au ya kiume."

Changamoto za maisha utotoni

Alianza kufahamu hali yake pindi alipotimiza miaka mitano hivi alipogundua kwamba alikuwa tofauti na watoto wengine.

Wakati huo wazazi wake walimpa nasaha ya kujikubali alivyo. Anasema kuwa jamaa zake wa karibu walisimama naye na kuhakikisha kuwa wamelinda kile kilichokuwa siri ya maumbile yake.

Anasema kuwa changamoto kubwa zilikuwa akiwa Shule ya upili, kwani alikuwa kwenye bweni.

Nguvu nyingi alizitumia kuficha hali yake kwani alijitambua kama binti.

Pamoja na kuwa na umbo la kike, Bi.Musamba anasema ana ukakamavu na nguvu kama za kijana wa kiume

Chanzo cha picha, Baby John Musamba

Anasema kuwa miaka yote aliyosomea huko hakuna aliyegundua kuhusu kasoro iliyopo katika maumbile yake.

Baby aliandikishwa kama mtoto wa kike alipozaliwa, na hata kwenye vitambulisho vyake vya kuzaliwa vimenakili hivyo.

Alipozaliwa wazazi wake walihesabu watoto wao kama mabinti wawili na kaka watatu. Hata hivyo, kwa ndani familia hiyo ilihesabiwa kuwa na binti mmoja na kaka watatu na yeye ambaye ana jinsia yenye utata

Musamba anasema kwa maumbile yake ya ndani, hana viungo vya uzazi vya kiume wala vya kike. Ana sehemu ndogo tu ya kwenda haja ndogo.

Kati ya sehemu hiyo na sehemu ya kwenda haja kubwa ni mfupa tu.

Pia anasema kuwa hana matiti ila, muonekano wake una umbo la kike .

Baby amefanyiwa uchunguzi mara nyingi maishani, akiwa na miaka miwili, akiwa na miaka sita, kumi na 20. Nyakati zote, uchunguzi umebaini kuwa hana viungo vyovyote vya kuashiria kama yeye ni wa kike au kiume.

Kufichua siri

Musamba aliishi kuificha hali yake hadi alipochukua fomu za shughuli ya mchujo wa wabunge alipojaza kuwa mtu asiyekuwa na jinsia.

Musamba kwa kujitambulisha hujitambulisha kama binti lakini anasema kwamba amechoka kuishi na siri hiyo kuhusu maumbile yake ya uzazi.

Tarehe 23 Julai mwaka huu wa 2020 aliutangazia ulimwengu kwamba yeye si mwanamke wala mwanaume.

Hafla yenyewe ilikuwa ya kujinadi kwa watu ili wampigie kura awe mgombea wa chama kimoja cha siasa nchini Tanzania katika uchaguzi wa mwezi Oktoba.

"Nilifahamu wakati wangu wa kuueleza ulimwengu kuhusu maumbile yangu ulikuwa umefika, kwa kuwa nimeishi kuficha maumbile tofauti kwa miaka mingi," anasema.

"Ninafahamu changamoto zinazowakumba watu walemavu hasa unyanyapaa , kwa hivyo nilitamani niwe kipaumbele kuhamasisha jamii kama kiongozi bungeni. Ndoto hiyo hata hivyo haikutimia," Musamba anasema

Tangu ajitambue na kufahamu kwamba kuna jinsia mbili, ilibaki kumsumbua usiku na mchana

Chanzo cha picha, Baby John Musamba

Matokeo ya kura yaliashiria kuwa alipigiwa kura 1 pekee kwenye mchujo. Kura 5 ziliharibika.

Lakini jinsi habari zake zilivyopokelewa pia zilimshangaza mwanadada huyu.

Anasema kuwa katika umati huo ambao kulikuwa na wanahabari pia. Wengi walilia na kushangazwa na habari hizo.

Hata swahiba wake wa karibu kwa jina Esther aliyemfahamu kwa miaka mingi pia alichanganyikiwa kusikia kuhusu maumbile yake.

"Tumekuwa marafiki na Esther rafiki wake wa karibu lakini sikuwahi kumueleza kuhusu maumbile yangu. Yeye alijua kuwa mimi ni mwanamke kamili na wakati mwingi alikuwa ananiuliza kuhusu maisha yangu ya kimapenzi, Ila nilikuwa nampeleka hivi hivi na maneno," anasema.

"Tangu wakati huo hatujaonana ila tunazungumza kwa simu karibu kila siku " Musamba alisema. -

Japo ulimwengu ulipokea habari hizo Julai, baadhi ya jamaa zake wa karibu wameishi kujua alivyo Baby John Musamba.

Mwanadada huyu anaomba serikali Iweke sheria zinazowatambua watu kama yeye.

Musamba angependa maisha yake ya kimapenzi yabaki faraghani kwa sasa.

Daktari Berno Mwambe anasema hali hii hutokea mara chache sana kwa watoto wa kike, kwa wastani mtoto 1 Kati ya 4,500 wanaozaliwa.

Chanzo cha picha, Dkt Berno Mwambe

Hali kama hii husababishwa na nini?

Kulingana na daktari wa afya ya uzazi wa wanawake nchini Tanzania Dkt Berno Mwambe, hali hii kwa Kiingereza hufahamika kama Disorder of Sex Development (DSD). Hii ni hali ya viungo vya uzazi kukosa kukomaa.

Anasema kuna aina nyingine ya ugonjwa unaojulikana kama Mayer-Rokitansky-Kuster-Hauser (MRKH) syndrome, ambao unahusu mwanamke kukosa viungo vyote vya sehemu za uzazi .

Daktari anaongeza kuwa hali hii inatokea mara chache sana kwa watoto wa kike, kwa wastani mtoto 1 Kati ya 4,500 wanaozaliwa.

Hali hii inasababishwa na mabadiliko katika vinasaba vinavyohusika katika ukuaji wa viungo vya mwanamke.

Na je marekebisho yanaweza kufanywa? Dkt Berno anasema kuwa inategemea usugu wa hali yenyewe.

Kwa mtu ambaye viungo vyake vya uzazi havijakua vizuri, basi mtu anaweza kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha.

Kwa mtu ambaye hana kabisa kwa mfano Bi Musamba, matibabu yake yanakuwa magumu hususan kwenye muundo na tamaduni za jamii za kiafrika zilivyo.

Aidha daktari anasema kuwa nchi za ng'ambo hufanya marekebisho na hata kumpandikiza mwanamke mji wa uzazi wa mtu mwingine na hata kutengeneza uke. Mwathirika anaweza kufanikiwa hata kushika na kuubeba ujauzito baada ya upasuaji na tiba ya homoni.