Jane na mumewe Donah Omondi wamekuwa kwenye ndoa kwa miaka 12 bila mtoto

Chanzo cha picha, Jane Aller
- Author, Anne Ngugi
- Nafasi, BBC Swahili
Unapozitazama video za Jane Aller na nyimbo zake kwenye mitandao ya kijamii, huwezi kamwe kudhani kwamba anaupitia mtihani mgumu maishani.
Kwa muda mrefu, yeye na mumewe Donah Omondi walikuwa wakifanya juhudi za kupata mtoto.
Lakini kila walipokaribia kupata, bahati haikuwa upande wao.
Ni safari ambayo Jane anaamini wanawake wengi wanaipitia kimya kimya bila kujitokeza hadharani.
Jane, ambaye ni mwanamuziki wa nyimbo za Injili nchini Kenya anasema ameamua kuzungumzia changamoto zake kuwatia moyo wengine.
Je, aliingiaje kwenye maisha ya ndoa? Alijaaliwa mtoto mwishowe?

Chanzo cha picha, Jane Aller
Ndoa na matumaini
Jane Aller amekuwa kwenye ndoa kwa miaka 12. Kwa miaka ya kwanza minne ya kwa katika, ndoa yake kulitokea msururu wa matukio ambayo hayakuwa ya kawaida.
"Mwaka wa kwanza tu baada ya ndoa nilishika mimba, na ikawa ni furaha kuu kwangu na mume wangu. Lakini kwa bahati mbaya ile mimba ilitoka yenyewe baada ya kipindi cha miezi mitatu tu," anakumbuka.
Na kwa kuwa ilikuwa ni tukio la kwanza alihisi kuwa ilikuwa ni ajali na kwa hayo hakuwa na wasiwasi wowote. Alijua fika kwamba angeshika mimba tena na kujifungua.
Kwa kawaida mwanamke anaposhika mimba, mchakato mzima hufanyika katika mfuko wa uzazi ambapo yai la mwanamke hutungishwa mbegu ya mwanamume ndani ya mfuko huo. Hapo ndipo mtoto huanza kukua. Lakini kwake Jane, mara ya pili mchakato wa kushika mimba yake ulifanyika katika mishipa ya uzazi. Mimba ya aina hiyo hujulikana kama ectopic.
Nusura apoteze uhai wake wakati huo.
"Kwa siku nne nilitokwa na damu ndani ya tumbo langu (kizazi), nisijue kuwa mimba ilikuwa imeharibika na maisha yangu yalikuwa hatarini," anasema.
"Kwa siku nne hizo nilikuwa nahisi uchungu mwingi mno. Kwa kuwa daktari aliyekuwa ananihudumia hakuwa jijini ilibidi kusubiri hadi arejee ofisini."
"Wakati huu wote sikujua kuwa mtoto alikuwa amefariki, na ndani ya tumbo langu mlikuwa kumejaa damu iliyokuwa imeshikamana," Jane anakumbuka
Ilibidi mwanamke huyu alazwe hospitalini na kufanyiwa upasuaji kuyaokoa maisha yake.
Ni kipindi anachokitaja kuwa cha uchungu mwingi sio tu wa mwili bali pia msongo wa mawazo kwa kupoteza mtoto wao wa pili .
"Kabla ya kuingia kwenye chumba cha upasuaji ilibidi nitolewe damu kwa vipimo vya kawaida. Hapo ndipo daktari aliuliza ni vipi mimi niko hai ilhali damu yangu ilikuwa imeshikana na kuganda,"Jane anasema.
Kipindi hicho Jane alianza kujiuliza maswali mengi mno ,vile vile akaanza kuwa na kero akiuliza Mwenyezi Mungu ni kwanini alikuwa anakubali yeye apitie hali hiyo.
Jane anasema kuwa walirejea nyumbani bila mtoto.
Lakini baada ya muda alishika mimba nyingine ila haikuchukua muda kwa mimba ile kutoka tena.

Chanzo cha picha, Jane Aller
Kujiuliza maswali mengi
Mwanadada huyu anasema kuwa licha ya kuwa mtumishi wa Mungu yeye na mume wake walishikwa na hisia za hasira na akawa na majonzi mengi mno.
Hawakupata majibu stahiki kutoka hata kwa madaktari wake kwani alikuwa anaelezwa kuwa kila kitu katika kizazi chake kilikuwa sawa.
"Msimu ambao nilimpoteza mtoto wangu wa tatu nilikuwa katika pilikapilika za uimbaji, na kwa kuwa nilikuwa nimefanyiwa upasuaji , sehemu iliyoshonwa ilianza kuwa na matatizo katikati ya uimbaji wangu," anasema.
"Wakati huo nilishindwa kuelewa ni kwanini licha ya utumishi wangu wa uimbaji kwa Mungu nilipitia mapito hayo,"Jane anakumbuka.

Chanzo cha picha, Jane Aller
Mwanadada huyu anasema kuwa hakuelewa ni vipi Mwenyezi Mungu alikuwa anamtumia katika hali ya kupoza maisha na nyoyo za watu kupitia uimbaji wake , ilhali yeye alikuwa anawapoteza watoto kila aliposhika mimba.
Kwa hivo msimu huo alipokuwa anashika kipaza sauti katika uimbaji wake alikuwa anadondokwa na machozi mengi.
"Wakati huo nilipokuwa nalia watu walikuwa wanafikiria kuwa niko kwenye maombi makubwa, wasijue kuwa nilikuwa nalilia hali yangu ya kupoteza watoto wangu," Jane anakumbuka
Kwa hivyo aliposhika mimba yake ya mtoto wa wanne alikuwa na msisimko , lakini Jane na mumewe waliamua kwenda hospitalini ili afanyiwe uchunguzi ilikubaini kuwa kila kitu kilikuwa sawa.
Matokeo ya uchunguzi huo yalikuwa ya kukatisha tamaa.
Daktari alimueleza kuwa mimba ilikuwa imeshika katika mshipa wake; alionywa kuwa ikiwa mshipa huo ungepasuka , basi maisha yake yangekuwa hatarini. Kwa hivyo alishauriwa kuwa mimba hiyo lazima itolewe ili asipoteza maisha yake.
" Kupoteza mimba ya nne haikuwa rahisi , nililia kwa siku nyingi mno, na sikutaka kuzitizama nguo ambazo nilikuwa nimenunulia watoto wangu, kati ya kupoteza mtoto wa kwanza hadi wanne nilikuwa najiuliza je huyu mume wangu ananipenda bado? " Jane anasema.
Jane anasema kuwa mwamba mkuu umekuwa ni mume wake, kwani amesimama naye katika hali hii ya kupoteza watoto wake .
Baada ya kupoteza mtoto wao wanne alikaa kwa miaka kadhaa kabla ya kushika mimba tena.
Ni hadi mwaka uliopita aliposhika mimba yake ya tano.
Baada ya miezi mitatu ile mimba ya mtoto wa tano ilitoka. Kitu ambacho sio cha kawaida, Jane anasema, ni kuwa ule uchungu wa mwanzo aliokuwa nao ulikuwa haupo.
Mwanadada huyu anasema kuwa alianza kukubali hali yake na kuamua kumuamini Mwenyezi Mungu kumpa mtoto katika wakati mwafaka.

Chanzo cha picha, Jane Aller
Jane na mumewe wamehimilije ndoa ya miaka 12 na hali hii?
Kama mwimbaji Jane Aller anategemea mume wake kama mtayarishi na mwelekezi wa nyimbo zake.
Kutokana na hilo, wameletwa pamoja na hali yao ya kupenda muziki na pia hali ya huduma ya kuhubiri.
Kando na kuwa ni mke na mume, wanashiriki katika maoni na kazi zao za kila siku ambayo ni huduma ya uimbaji.
Mwanamke huyu anasema mume wake amekuwa nguzo kuu katika maisha yake hasa changamoto hizi za mimba kutoka .
Changamoto zimetokana na jinsi jamii inavyochukulia hali yake ila Jane anasema kuwa jamaa wa karibu kwa mfano mama mkwe wamesimama na yeye sana.
Na anapotoa mawaidha kwa watu ambao wanapitia hali hio anawaomba wasikate tamaa.
"Unajua kuna watu ambao wametengana kutokana na kukosa watoto kwenye ndoa , na hata wanapoingia kwenye ndoa mpya bado wanakabiliwa na changamoto hizo hizo," anasema.
"Ni muhimu kwa watu wanaopitia changamoto hizo kuwa na subira na kudumisha hali ya kupendana na kuvumiliana," Jane anasema.
Jane anasema maisha ni kama kuendesha baiskeli , ili mtu awe na usawa lazima aendelee kusonga mbele. Kwa hivyo mambo mazuri huja kwa watu ambao wanaendelea kuwa na imani wakati ambapo hakuna cha kutumainia.
Jane Aller na mumewe Donna wanaendelea kutumai kuwa wakati mmoja watapakata mtoto wao mikononi mwao.

Chanzo cha picha, Jane Aller
Mimba hutoka kwa nini?
Mimba kutoka pekee yake au kuharibika kwa mimba hutokea kwa kawaida kwa baadhi ya wanawake kote duniani.
Wakati mwingine hutokea mapema sana kiasi cha kuwa mwanamke hawezi kufahamu kuwa alikuwa mjamzito.
Maambukizi ya magonjwa ya zinaa, majeraha, vurugu, na mafadhaiko ya kiakili yanaweza kufanya mimba kutoka mapema.
Wakati mwingine pia mimba huharibika kwa sababu mwanamke mjamzito amekuwa karibu na sumu au kemikali zilizo na sumu. Si rahisi kujua kila wakati kinachosababisha uharibikaji wa mimba, lakini baadhi ya sababu zinaweza kuepukika.
Kuharibika kwa mimba wakati mwingine unaweza kuzuiwa kwa kutibu wanawake kutokana na maradhi na maambukizi na kuwasaidia kuepukana na sumu ya kemikali au maeneo ya hatari . Lakini wanawake wengine huwa na uharibikaji wa mimba moja baada ya nyingine, na huweza kushindwa kujua ni kwa nini.
Wanawake walio na historia ya uharibikaji wa mimba unaojirudia wanapaswa kupimwa na kutibiwa katika kituo cha afya kilicho na huduma za kipekee ili kutafuta sababu na kuwasaidia kubeba mimba hadi mwisho wa ujauzito.












